Kadi za elektroniki kudhibiti ulaji, uanachama hewa CCM

Wanachama na wafuasi wa Chama cha CCM wakiwa kwenye mkutano wao wa chama .Picha ya maktaba

Muktasari:

  • Kutokana na mfumo huo, CCM waliohojiwa wanasema mfumo huo mpya utakomesha na kumaliza malalamiko hayo kwa sababu wanachama wataweza kutambuliwa.

Dar es Salaam. Zaidi ya miezi mitano imepita tangu CCM ianze kuandikisha wanachama wake kwa mfumo wa kielektroniki utakaohakiki idadi yao na mapato yatokanayo na kadi.

Kupitia mfumo huo mwanachama anatambuliwa kwenye mtandao tangu shina, tawi, kijiji, kata, wilaya na mkoa anakotokea.

Halmashauri Kuu ya CCM katika kikao chake cha Desemba 13,2016 ilitangaza kufanya uhakiki wa wanachama na jumuiya zake ili kujua idadi sahihi ya wanachama, shughuli inayoendana na utoaji wa kadi za kisasa za kielektroniki ili kuwa na udhibiti, usahihi na kuondoa wanachama hewa. Miaka ya nyuma kulikuwa na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wanachama wakilia kuwapo kwa wanachama hewa ambao mara nyingi walikuwa wanajitokeza kipindi cha uchaguzi ili kupitisha wagombea.

Kutokana na mfumo huo, CCM waliohojiwa wanasema mfumo huo mpya utakomesha na kumaliza malalamiko hayo kwa sababu wanachama wataweza kutambuliwa.

“Ni mfumo wa kisasa unaokiongezea heshima chama chetu na wanachama wake kwa sababu sasa hivi ukishaandikishwa unajulikana mahali uliko na shughuli unazofanya,” anasema Alitidisia Kahwili, mwanachama wa CCM, Wilaya ya Ilala. Katibu wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya itikadi na uenezi CCM Zanzibar, Catherine Peter anakiri mfumo huo ni kiboko ya wanachama hewa ambao mara nyingi hujitokeza kipindi cha uchaguzi kwa nia ya kupiga kura au kuomba kuchaguliwa kwenye uongozi.

“Pia, mfumo huu utawabana wanachama wasio lipa ada, fikiria wana CCM tupo wengi lakini watu hawalipi ada? Tunataka kujua mapato yetu ya ada yakoje? Haiwezekani tupo wengi lakini wanaolipa wachache? Tunaweza kujijua maendeleo yetu kupitia haya masuala ya kielektroniki,” anasema Peter.

Katibu wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Zakharia Mwansasu anasema kupitia mfumo huo wanachama wataweza kulipa ada moja kwa moja kwenye akaunti ya ada ya CCM kwa kutuma kupitia mitandao ya simu zao.

“Kwa hiyo suala la ulipaji wa ada za wanachama litakuwa rahisi zaidi na wanachama watalipa popote walipo tofauti na mfumo wa zamani ambao walikuwa wanalazimika kusafiri hadi katika ofisi za watendaji kulipa,” anasisitiza.

Mwansasu anasema kila mwanachama anapolipia ada, jina lake linasoma moja kwa moja mtandaoni na fedha hizo kuingia kwenye akaunti moja ya ada kabla ya kugawanywa kulingana na katiba ya CCM inavyoelekeza.

Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Raymond Mwangwala anasema mfumo huo utarahisisha utendaji wa kazi wa chama hicho si tu katika kulipa ada, katika kuhakikisha na kukusanya taarifa za chama.

Anasema kwa namna kadi hiyo ilivyotengenezwa inaweza kusaidia katika maeneo mengine mengi ikiwamo suala la manunuzi.

“Kwa hiyo wanaCCM waendelee kujitokeza wajiandikishe kwa sababu, faida ni nyingi mno.” anasema.

Katika uandikishaji, Mwangwala anasema wanachama wengi wamehamasika na wanajitokeza kwa wingi.

“Kundi la vijana ni kubwa zaidi kutokana na uwezo wao mkubwa katika kutumia vifaa vya kidigitali zikiwamo simu kwa hiyo tunaendelea kutoa elimu, wajitokeze,” anasema.

Mwagwala anasema suala la uandikishaji ni endelevu na kadiri siku zinavyosogea ndivyo wanachama watakavyokuwa wakiondoka kwenye mfumo wa kizamani.

Katibu wa CCM wa mkoa wa Dar es Salaam anasema mpaka sasa wamefanikiwa kuandikisha zaidi ya wanachama 68,000 kati ya 444,890 waliopo kwenye mkoa huo, lengo likiwa kuwafikia wote.

Katibu wa CCM Wilaya ya Pangani Mkoa wa Tanga, Charles Charles anasema katika wilaya hiyo bado hawajaanza kuandikisha, lakini zoezi hilo litaanza karibuni.

Kwa upande wa Mkoa wa Ruvuma, Katibu wa CCM mkoa huo, Jimson Mhagama anasema wanaendelea kutoa elimu kwa wanachama ili kuharakisha uandikishaji huo unaoendelea.

Pamoja na mambo mengine, anasema mfumo huo utaleta mapinduzi ndani ya chama hicho kwa sababu utaondoa urasimu katika suala la ulipaji wa ada.

“Mtu hata akiwa nyumbani ana uwezo wa kulipa ada yake ya uanachama bila usumbufu wowote,” anasema.

Ili mwanachama ajiandikishe ni lazima awe na kadi ya CCM ya awali na kitambulisho kinachotambuliwa na Serikali kikiwamo cha uraia, kura au hati ya kusafiria.

Kwa upande wake, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Wilaya ya Iringa Mjini, Edwin Bashir anasema mfumo huo utakiongezea chama hicho mapato kwa sababu ulipaji wa ada.

“Mfumo huu rekodi ya wanachama inakuwa kwenye ‘database’ moja hivyo unaweza kupata taarifa za mtu yeyote yule kutoka mahali popote Tanzania ukajua ni mwanachama au kiongozi,” anasisitiza.

Hata hivyo, Mwangwala anasema changamoto pekee inayojitokeza kwenye shughuli hiyo ni uelewa kwa baadhi yao kwa kuamini kwamba mara tu wakijiandikisha, wanaweza kutupa kadi za zamani.

“Kwa sasa zinatumika kadi zote ya kisasa na ile ya zamani, kwa hiyo tunaendelea kutoa elimu kwa wanachama wetu na wito wangu kwao wajitokeze,” anasisitiza Mwangwala.