Kangomba inavyozuia fursa lukuki katika korosho na mazao mengine

Wakulima wakijaza korosho kwenye kiroba baada ya kuzifikisha ghalalani .Picha ya maktaba.

Muktasari:

Ukiwauliza wakulima wengi wataeleza kuwa wanunuzi wa kangomba ndio waliowasaidia wakati familia zao zilipokuwa na matatizo ya kiafya, walipohitaji fedha kwenda kuhani kilio, kupeleka watoto jando au kuwacheza unyago watoto wao wa kike.

Watanzania wanaofuatilia sakata la korosho tangu lilipoanza na linavyoshughulikiwa na Serikali, wanaweza kulitazama kwa mawazo hasi kuwa huenda likaathiri uzalishaji wa zao hilo. Wanafikiria hivyo kwa kuwa wanunuzi waliokuwa wakitumia mfumo usio rasmi (kangomba) walikuwa wadau wakubwa wa wakulima hao.

Wanunuzi wa kangomba walikuwa wakianza kujipenyeza kwa wakulima kwa kuwapatia fedha za kujikimu wakati korosho zao zikiwa hazijakomaa na kabla ya kuanza kuvunwa.

Ukiwauliza wakulima wengi wataeleza kuwa wanunuzi wa kangomba ndio waliowasaidia wakati familia zao zilipokuwa na matatizo ya kiafya, walipohitaji fedha kwenda kuhani kilio, kupeleka watoto jando au kuwacheza unyago watoto wao wa kike.

Wengine watasema kuwa kangomba ndio waliowapa fedha za kugharamia sherehe zao za komunio, kipaimara au ubatizo wa watoto wao. Haya ni machache katika mengi yaliyokuwa yakichukuliwa kama mwanya kwa kangomba kutanguliza fedha kwa wakulima.

Kwa kuwa wakulima husukumwa na shida, wakati ule huwa hawaoni madhara ya wanachokifanya. Kwa mfano hawaoni wanunuzi wa kangomba wanavyowadhulumu kwa kununua korosho zao kwa bei ndogo.

Hawaoni kuwa kwa kuuza korosho zao kwa bei ndogo uwezo wao wa kuhudumia mashamba unakuwa mdogo na kwa sababu hiyo uzalishaji huzidi kupungua mwaka hadi mwaka.

Pia, hawaoni kuwa malipo wanayopata kutoka kwa kangomba yanakuwa hayana tija kwani hata matumizi ya fedha hizo huwa ni mabaya na yasiyo na tija kwa familia.

Serikali mwaka huu ilipopiga marufuku mfumo wa kangomba na kuamua kununua korosho kwa bei halali, wakulima wameweza kuuza korosho kwa Sh3,300 tofauti na wengine waliouza korosho zao kwa wastani wa Sh1,700 mpaka 2,000 kwa wanunuzi wa kangomba.

Moja ya hasara za kangomba ni wakulima wengi kupunjwa kwa sababu wanunuzi hawatumii vipimo sahihi kuhakiki uzito badala yake upimaji ulikuwa ni wa kukadiria. Vilevile ubora wa korosho umekuwa wa chini kwa sababu wakulima hawana motisha ya kulinda ubora kutokana na bei ndogo wanayolipwa.

Mkakati wa kubangua korosho

Wazo la kubangua korosho limepata hamasa zaidi baada ya kuangalia uhalisia wa faida itokanayo na ubanguaji wa zao hilo badala ya kuuza zikiwa ghafi. Kwa hesabu za haraka mbanguaji anahitaji kilo tano kupata kilo moja ya korosho iliyobanguliwa. Hiyo inamaana kuwa Serikali itatumia Sh16,500 na kama itauza kwa wastani wa Sh20,000 kwa kilo moja ya korosho iliyobanguliwa hivyo faida ya Sh3,500 itapatikana. Hii inaonyesha kuwa korosho iliyobanguliwa inalipa na ikiwa mkulima atauza korosho zilizobanguliwa atapata Sh4,000 kwa kila kilo ambayo haijabanguliwa.

Kutokana na taarifa mbalimbali kutoka kwa watalaamu wa korosho inakisiwa kuwa kwa wastani gharama za kuzalisha korosho ghafi ni Sh1,350 kwa kilo moja na inakadiriwa mkulima anaweza kuzalisha kilo 14 kwa wastani kwa mti mmoja wa mkorosho.

Ikiwa mkulima wa korosho atakubali kushirikiana na watalaamu ambao watafanyakazi ya kusimamia mashamba na kuyahudumia kitalaamu na kibiashara, mti mmoja wa mkorosho unaweza kuzalisha kilo 28 ikitegemea aina ya mkorosho. Hiyo inamaana kuwa mkulima anaweza kuongeza kipato chake mara mbili.

Tuseme baada ya mkulima kulipa gharama zote atapata faida kamili ya Sh6,000 kwa kila kilo moja na anamiliki ekari tano zenye mikorosho 200 (kila ekari miti 40) maana yake anapata kilo 5,600, ukizidisha mara Sh6,000 faida kwa kila kilo mkulima huyo atapata faida kamili ya Sh33,600,000 kwa mwaka. Hivi huyu anaweza kuwekwa katika kundi la maskini?

Mkulima huyu anaweza kupanua kilimo kikawa cha kisasa zaidi na kipato chake kuongezeka. Ongezeko la thamani litaongeza idadi ya viwanda na kufungua njia ya kujenga vingine vya kusindika mazao ambavyo vitaongeza ajira, kipato na kodi kwa Serikali.

Iwapo atasindika mabibo kupata juisi au kuchuja mafuta ya korosho ambayo nayo yana soko kipato kitaongezeka zaidi.

Sakata lililoibuka katika korosho mwaka huu limefungua pazia linaloonyesha jinsi gani Tanzania na watu wake walivyo matajiri ikiwa watajengewa uwezo na kuzalisha kwa wingi, ubora, kusindika na kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani.

Kangomba iko katika mazao yote ya wakulima nchini ikiwamo kahawa, pamba, mahindi, mpunga na ndizi ambapo wapo wafanyabiashara hununua mazao yakiwa shambani au yamevunwa lakini yakiwa hayajachakatwa hivyo kuuzwa kwa bei ya kutupwa.

Mwarobaini wa kangomba

Changamoto ya kupata fedha za kujikimu wakati wa kuandaa mashamba ambayo ndiyo hasa tatizo kuu linalowakabili wakulima litapatiwa dawa kwa kuunda vikundi vya kilimo biashara, ambavyo kupitia kilimo chao cha mseto na kwa kushirikiana na wadau wengine watakaotambuliwa na Serikali watazalisha, kusindika na kuuza bidhaa zilizoongezewa thamani.

Ndani ya vikundi vyao watakuwa na mfumo wa kuweka na kukopa ambao utawakopesha fedha za kujikimu na za kibiashara ambazo zitatolewa na vyombo vya fedha.

Wakulima washauriwe kuwa na miundombinu ya umwagiliaji iliyo imara, kuwa na bima za mazao ili kupunguza vihatarishi vinavyoweza kuathiri biashara zao. Ziko Benki ambazo zimeanza kutoa mikopo ya fedha za kujikimu kwa wakulima, licha ya kuwa riba zao zipo juu, lakini kwa mkulima anayeuza bidhaa zilizoongezewa thamani riba sio tatizo kubwa kwani gharama hiyo italipwa na walaji japo bei za bidhaa zitakuwa chini ikilinganishwa na bei za wachuuzi. Wakulima hao watakuwa na bei moja kwa msimu mzima na masoko yao yatalenga kujenga uhusiano kati yao na walaji.

Ni vema changamoto zitokanazo na kangomba katika korosho zichukuliwe kama fursa za kuangalia kwa undani kinachofanyika kwenye mazao mengine na kuhakikisha mfumo wa namna hiyo unaondolewa ili wakulima waweze kuzalisha, kusindika na kuuza mazao yaliyoongezewa thamani.

Mwandishi wa Makala hii ni Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Africa Rural Development Support Initiative (ARUDESI), anapatikana kwa simu 0715301494/0752110290