Kanuni rahisi na zenye ufanisi za kukusaidia kuijenga ndoa yako

Sunday January 6 2019Rr Chriss Mauki

Rr Chriss Mauki 

Wiki jana tuliona kanuni mbili rahisi na zenye ufanisi za kukusaidia kuijenga ndoa yako, leo tunaendelea na zinazofuata.

3. Jifunze kuzungumza lugha ya mapenzi ya mwenza wako

Fahamu kwamba mke au mume wako ana lugha yake moja ambayo ni maalumu kwa yeye kuonyesha au kuwasiliana kimapenzi. Lugha hii inakuwa mojawapo kati ya zile lugha tano ambazo labda unazifahamu au umewahi kuzisikia. 1. Matendo ya kusaidia “acts of service”. 2. Maneno ya kupongeza au kusifia “words of affirmation”. 3. Muda wa faragha “quality time”. 4. Zawadi “gifts”. 5. Mguso au kugusana “physical touch”. Kwa mfano, kama mume wako lugha yake ya mapenzi ni matendo ya msaada, unaweza ukamletea kadi zenye maneno matamu sana na zawadi nyingine nyingi lakini hatokuelewa wala kuhisi kupendwa hadi utakapoamua kumsaidia kuondoa mizigo yake aliyoiacha kwenye gari, au kumfutia viatu vilivyokuwa vimechafuka.

Kama mke wako na yeye lugha yake ni muda wa faragha, unaweza kumsaidia kuosha gari lake, ukamsaidia kumwaga takataka na hata kumfulia nguo zake lakini hatoona kitu chochote wala kuhisi mvuto wowote kwa ulichofanya mpaka utakapoamua kutafuta muda kidogo wa kukaa pembeni yake, ukimwangalia machoni, umemsogelea huku mnakunywa kikombe cha chai au kahawa. Hapo ndipo anaona umemjali sana na unampenda.

Mara nyingi lugha ya penzi ya mwenza wako sio ya kwako, kwa hiyo kuna umuhimu mkubwa sana wa kujifunza na kujitahidi kwa kufanya mazoezi ili kumudu kuongea na hata kusikiliza lugha yake.

Hapa naweka mkazo zaidi kwamba sio tu kuongea lugha yake bali hata kuweza kuisikiliza. Hii itakusaidia sana kwenye kuelewa nini anamaanisha na nini anapenda kifanyweje. Kwa kuongea lugha ya mwenzako unamgusa sana hisia zake na hivyo kuamsha penzi baina yenu. Kama ungependa kuzifahamu zaidi lugha hizi unaweza kutafuta kitabu cha mwandishi Gary Chapman.

4. Kamwe usijifanye unafahamu mawazo ya mwenza wako

Mara nyingi ni rahisi sana kudhania ya kwamba unayajua mawazo ya mume au mke wako, labda kwa sababu unafuatilia sana anavyofanya au kusema mara kwa mara na hivyo kila akifanya kitu unatoa hitimisho kwamba nia yake ilikuwa hii au ile na wakati wote unamhesabia kuwa amefanya kitu hicho kwa nia mbaya. Ni kweli kwamba mara nyingi mawazo yetu yana kuwa hasi zaidi juu ya yale wanayofanya wenza wetu kuliko kuwa chanya. Hii imesababisha hata mwitikio wetu kuwa hasi maana hata tafsiri tuliyokuwa nayo ni hasi. Wewe huwezi kuyafahamu mawazo ya mwenza wako na kwa hiyo usijifanye unajua. Mungu peke yake ndiye azichunguzaye nafsi na moyo na kuyajua yaliyo ndani. Hakuna mwanadamu kwenye uwezo huu.

Inawezekana kabisa, na ninakubaliana na wewe, labda umekuta hajafunga mlango wa uani au bafuni kama ambavyo hakuufunga jana na juzi.. Itaendelea

Advertisement