Kanuni rahisi na zenye ufanisi za kukusaidia kuijenga ndoa yako

Kabla sijaenda mbali na kukuruhusu wewe msomaji kuzama ndani ya makala hii nadhani ni vema niliweke hili wazi kwamba njia hizi ninazozizungumzia si misingi ya ndoa. Misingi ya ndoa ni makala au somo lingine pia nililonalo ingawa labda kuna maeneo utaona kuna kufanana. Njia hizi ni baadhi ya zile ambazo wengi walishauriwa kuzitumia na zikawasaidia na kwa hiyo labda na wewe zinaweza kukusaidia kama wao. Hizi ni njia ambazo ni rahisi kuzielewa ingawa mara nyingine zinaonekana ngumu kuzitendea kazi. Pamoja na hayo yote bado njia hizi zimeonekana kuwa msaada kwa wengi.

Inaendelea kutoka wiki ya jana...

5. Jifunzeni kuiombea ndoa yenu

Nafahamu kabisa kuwa una imani yako inayopewa msukumo na dini yako lakini kwa vyovyote vile maana yangu ni kwamba hata kama mwanaume na mwanamke wanaweza kuishi pamoja na siku zikasonga bado umuhimu wa nyinyi wawili kuiombea ndoa yenu unabaki pale pale. Sisemi kwamba kama msipofanya hivyo ndoa itavunjika siku inayofuata, la hasha, lakini wale ambao wamekuwa wakiziombea ndoa zao wamekiri kuishi kwa furaha na misuguano michache sana kuliko wale ambao hawafanyi hivyo. Kuiombea ndoa si kuwaombea watoto ingawa watoto ni sehemu ya ndoa yenu. Unapoombea familia unawaombea na watoto ndani yake. Kuiombea ndoa kunayahusu mahusiano yako na mume au mke wako. Ziko nyakati utaomba kawaida na ziko nyakati utajikuta unalazimika kufunga ili kuomba kwa kina zaidi. Ndoa zetu hupitia nyakati ngumu sana mara nyingine na kwa hivyo msaada wa Mungu ni lazima. Usisahau kwamba ibilisi au shetani anajua fika kwamba akiivuruga ndoa yako amewavuruga wote, na ndiyo maana ukichunguza utagundua wapo ambao baada tu ya ndoa zao kuyumba au kuvunjika, maisha yao yalibadilika sana, watoto wakafarakanika, kazi na ajira zikayumba na hata afya zikatetereka. Kuwa makini sana kwenye hili.

6. Epuka kumkosoa au kumrekebisha mwenza wako hadharani

Jitahidi sana kutokumkosoa au kumrekebisha mume au mke wako mnapokuwa katikati ya watu wengine labda kiwe ni kitu chenye umuhimu mkubwa sana na ambacho hakiwezi kusubiri, mara nyingine unakimbilia kumrekebisha kwenye kitu ambacho wala hakuna anayejali marekebisho hayo au marekebisho hayo hayamfaidishi yeyote kwenye hao waliopo, sasa kama ni hivi, unamrekebisha ili nini? Kwa taarifa yako watu mlio nao wala hawatokumbuka kile alichokuwa anaongea mwenza wako ambacho ulihisi amekosea lakini wakati wote watakumbuka jinsi ulivyokuwa unamkosoa na kumrekebisha mwenza wako bila busara.

Wakati mwingine hata mnapokuwa peke yenu usikimbilie kwa kasi kumkosoa au kumrekebisha labda pale unapofahamu kuwa hata yeye unayemrekebisha ataelewa na kukubali marekebisho hayo. Kumbuka kwamba mara nyingi zile taarifa mnazokosoana au kurekebishana si za muhimu sana bali yale mahusiano yenu.