Karama: Mashabiki wawili tu walinipa ubingwa wa dunia nje

Monday February 18 2019

 

By Imani Makongoro, Mwananchi [email protected]

Katika mchezo wa soka shabiki anahesabika kama mchezaji wa 12 uwanjani, vivyo hivyo kwenye michezo mingine, umuhimu wa mashabiki unahitajika, lakini ilikuwa tofauti kwa bondia Karama Nyilawila alipokwenda kuzichapa kuwania ubingwa wa dunia wa WBF.

Nyilawila ni miongoni mwa mabondia wachache nchini ambao wametwaa mikanda ya ubingwa wa dunia wakiwa nje ya nchi, baadhi ni Ibrahimu Class na Rashid Matumla.

Nyilawila alitwaa ubingwa wa dunia wa WBF baada ya kumchapa Kreshnik Qato wa Jamhuri ya watu wa Czech aliyekuwa nyumbani kwenye ukumbi wa Arena Sparta, huko Prague Arena Sparta, Desemba 3, 2010.

Mashabiki

Bondia huyo anakumbuka namna alivyoondoka nchini ambapo hakuwa na kocha wala mtu wa kumsaidia ulingoni. Aliondoka yeye na begi lake la vifaa vya mashindano.

“Ilikuwa ni safari yenye changamoto kidogo, sikuwa na mtu yeyote wa kunisaidia kule, zaidi ya wale walionipokea uwanja wa ndege kule Czech na hao hao ndiyo walikuwa wasaidizi na mashabiki wangu siku ya pambano,” anasimulia Nyilawila.

Anasema kwenye pambano hilo, mashabiki zaidi ya 10000 walikuwa wamejaa ukumbini kati yao wawili pekee ndiyo walikuwa wakimsapoti, lakini wengine wote walikuwa upande wa mpinzani wake, ambaye alikuwa na mbwembwe ulingoni.

Pambano lenyewe

Tofauti na soka timu pinzani kutoka nje inapokuja kucheza nchini na Simba na Yanga, inapata mashabi, lakini kwa Nyilawila ilikuwa tofauti.

“Ukumbi ulikuwa umefurika, mashabiki wote walimshangilia Qato, isipokuwa wale wawili ambao walinipokea uwanja wa ndege walikuwa upande wangu,” anasema Nyilawila.

Anasema mashabiki hao ndio alipanda nao ulingoni na walikuwa upande wa kona yake, kazi yao ilikuwa kumuelekeza namna ya kujipanga na kumsaidia kumpa maji wakati wa mapumziko.

“Nilichokuwa nikisikia wakati wanacheza waliniambia ‘good Karama, ‘good’ jab Karama, kauli ile ilinifanya niamini kuwa nacheza vizuri, niliongeza bidii zaidi, nilitaka niwatulize mashabiki ukumbini ambao muda wote walikuwa wakimshangilia mpinzani wangu.

“Ilipoanza raundi ya pili, taratibu kelele za mashabiki wa mpinzani wangu zilipungua ni raundi ndiyo iliyoanza kuonyesha taswira nani atashinda”, anakumbuka bondia huyo.

Anasema alikuwa na uwezo wa kukwepa mashambulizi na kujibu mapigo ambapo kila ngumi ambayo aliirusha ilifika kwa mpinzani wake na ilikuwa ya pointi.

Atwaa ubingwa

Katika ngumi ni nadra bondia anayecheza ugenini kushinda kwa pointi tena pambano la kuwania ubingwa wa dunia, lakini kwa Nyilawila iliwezekana.

Jaji namba moja Dusan Hecko alitoa pointi 117-111 kwa Nyilawila, jaji namba mbili Bernd Heynemann alimpa karama pointi 118-110 na jaji namba tatu Leszek Jankowiak alitoa ushindi wa pointi 116-112 kwa Nyilawila.

Mwamuzi Bela Florian alimtangaza Nyilawila kuwa bingwa kwa pointi za majaji wote watatu, kitendo ambacho anadai hakutarajia.

“Nilijikuta naruka juu ya ulingo kwa furaha ukumbi wote ulinywea nilifurahi hadi machozi yalinitoka,” anasema baada ya kuibuka mbabe mbele ya mpinzani wake.

Advertisement