Karama: Mpinzani wangu Ulaya alinifanyia umafia nje ya ulingo

“Wiki iliyopita tuliona safari ndefu ya Karama kutoka Tanzania kwenda Jamhuri ya watu wa Czech ilivyokuwa ngumu, lakini alipambana hadi kushinda pambano hilo la ubingwa licha ya kufanyiwa vituko na mpinzani wake nje ya ulingo wakati wa kupima uzito ili kumtoa mchezoni.

“Niliruka kwa furaha baada ya jaji kunitangaza bingwa, ukumbi mzima ulinywea hawakutarajia kipigo nilichompa bondia wao, nilirejea nchini na kukaa muda mrefu bila kupata pambano la kutetea ubingwa wangu,” anasema Karama. Karama alikuwa gumzo kila kona alipogoma kutetea ubingwa huo katika pambano lililopangwa kufanyika Ujerumani.

“Nilikaa na ubingwa muda mrefu bila kuandaliwa pambano la kutetea, lakini kabla sijatetea promota Don King alinitaka nicheze na Francis Cheka pambano lisilokuwa la ubingwa.

Anasema pambano na Cheka lilipangwa kufanyika Morogoro, hivyo kwa kuwa ngumi ndiyo kazi yake hakutaka kukwepa baada ya Don King kumfuata.

“Niliposaini mkataba wa pambano hilo, ndipo Mlundwa (Emmanuel) ambaye ndiye alinitafutia pambano la Czech alinitaka nikacheze Ujerumani kutetea ubingwa.

“Sikuona sababu ya kwenda kucheza Ujerumani, kwani siku ya pambano na Cheka ndiyo siku pambano la Ujerumani lilikuwa lifanyike, nililetewa mkataba wa dola 500 ambayo kwa wakati ule dola ilikuwa bado iko chini.

“Wakati kwenye pambano na Cheka nililipwa milioni sita kwa mazingira ya kawaida, hata angekuwa mwingine angeangalia maslahi yake kwanza, hivyo sikuona sababu ya kuwa na mkanda bila pesa,” anasema Karama.

Francis Cheka

Bondia huyo anasema katika maisha yake ya ngumi hakuna bondia aliyekuwa akimsumbua kama Cheka kutokana na uhodari wake wa kusukuma makonde ulingoni.

“Alicheza vizuri ulingoni hivyo ili kumpiga lazima ujipange kweli kweli, katika maisha yangu ya ngumi sikuwahi kupata bahati hiyo ni mara moja tu tulitoka naye sare zaidi mapambano yote niliyocheza naye nilipoteza.

Magereza

Karama ambaye alianzia ngumi za ridhaa kama baadhi ya mabondia wengi wa ngumi za kulipwa, anasema kilichomuingiza katika ngumi ilikuwa kusaka ajira kwenye jeshi la Magereza lakini mambo hayakwenda vizuri.

“Tulichukuliwa katika timu ngumi ya Magereza Mbeya kabla ya kuhamishiwa Dar es Salaam, lengo lilikuwa tupewe ajira Magereza lakini mambo hayakwenda sawa. Anasema baada ya kukosa ajira alirudi mtaani na kuanza kucheza ngumi katika klabu za mtaani kabla ya kujichanganya na mabondia waliokuwa wazoefu kwenye ngumi za kulipwa na hapo ndipo safari yake ya kucheza ngumi ilianza.

Anasema pambano lake kwanza katika ngumi za kulipwa alitoka sare na Pascal Ndomba Oktoba 2, 2005 kabla ya kuchapwa na Rashid Matumla Aprili 16, 2006 kwa KO pambano ambalo lilifanyika kwenye Ukumbi wa Royal Zambezi mkoani Mbeya.

Hata hivyo, kwa mara ya kwanza bondia huyo alishinda Oktoba 24, 2006 alipomchapa Matthews Mwape kwenye Ukumbi wa Royal Zambezi kwa TKO na hapo ndipo safari yake ya ubingwa ilianza.

Bondia huyo mzaliwa wa Mbeya ni kocha wa ngumi, ana rekodi ya kushinda mapambano 25 (14 kwa KO), amepigwa mara 19 (11 kwa KO) na ametoka sare mara tatu tangu mwaka 2005 alipojitosa katika ngumi za kulipwa.