Karl Lagerfeld: Mbunifu aliyeishi katika dunia yake

Kifo cha mbunifu Karl Lagerfeld hakikuushtua ulimwengu kama zilivyokuja taarifa za kwamba sehemu ya utajiri wake itakwenda kwa paka wake, Choupette.

Mbunifu huyo kiongozi wa kampuni ya Channel, alifariki dunia Februari 19 akiwa na umri wa miaka 85.

Lagerfeld mwenye asili ya Ujerumani atakumbukwa kwa kuleta mapinduzi ya mavazi akiwa na kampuni za Channel na Fendi.

Staa huyo aliyeleta mapinduzi katika kampuni ya Channel mwanzoni alipoanza kuitumikia mwaka 1983, mara zote katika miaka ya hivi karibuni alitambulika kwa miwani ya rangi nyeusi, soksi za mikono na nywele ndefu nyeupe.

Alitambulika kama mwanaume pekee katika ulimwengu wa mitindo ambaye mwonekano wake unajulikana (The most recognizable man in fashion).

Maiti yake kuchomwa kimya kimya

Mwili wa Lagerfeld utachomwa katika sherehe ya kimya kimya kama alivyoagiza na nusu ya majivu yake yatachanganywa na ya mpenzi wake Jacques de Bascher aliyefariki mwaka 1989.

“Ninataka mwili wangu uchomwe na majivu yangu baadhi yachanganywe na ya marehemu mama yangu, Choupette (kama atakufa kabla yangu) na mengine yachanganywe na ya Bascher,” alisema katika moja ya mahojiano aliyofanya hivi karibuni.

Mara kadhaa Lagerfeld alisisitiza kutaka majivu yake yachanganywe na ya mpenzi wake huyo aliyefariki kwa ugonjwa wa Ukimwi.

Utajiri

Mbunifu huyo mwenye utajiri unaokadiriwa kufikia dola za Marekani 200 milioni alisema atampa urithi huo paka wake Choupette huku akisema hata hivyo ana fedha za kutosha kuwarithisha watu wake wa karibu.

Mwingine atakayerithi mabilioni ya Lagerfeld ni Hudson Kroenig, mtoto wake wa ubatizo ambaye mara nyingi ameonekana akiongozana naye katika maonyesho.

Hudson mwenye umri wa miaka 10 ni mtoto wa mwanamitindo Brad Kroenig ambaye amefanya kazi na mbunifu huyo kwa miaka mingi.

Brad alimuomba Lagerfeld asimamie ubatizo wa mtoto wake na tangu hapo amekuwa kipenzi chake.

“Msijali kuna hela za kumtosha kila mtu,” alisema huku akikiri kuwa kuna wakati hurusha fedha dirishani kwa kuwa hakuzipenda.

“Si kwamba nina mabilioni kwenye akaunti yangu, huwa ninazitumia kwa kutoa zawadi na kuwanunulia marafiki, zikiwa nyingi sana nasimama dirishani nazitupa chini watu waokote,” alisema.

Kuhusu familia yake

Mara zote mbunifu huyo hakupenda kuzungumzia kuhusu familia yake isipokuwa dada yake anayeishi nchini Marekani akisema hawana ukaribu wowote.

“Ni kama undugu wetu umekufa miaka mingi lakini sijali,” alisema.

Kuhusu kuacha alama alisema asingependa kukumbukwa kwa lolote na mara zote alikataa kuandika kitabu kuhusu maisha yake.

“Natamani siku ya kufa ikifika nipotee tu, sitaki kuagwa, sitaki kuonekana.