Katibu Mtendaji wa Basata aeleza undani wa tozo, adhabu na tuzo

Saturday December 8 2018

Mwandishi wa Mwananchi Nasra Abdallah (kulia)

Mwandishi wa Mwananchi Nasra Abdallah (kulia) akifanya mahojiano na Katibu Mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza. 

By Nasra Abdallah,Mwananchi [email protected]

Moja ya taasisi za Serikali ambazo hazikauki midomoni mwa wadau wa sanaa na utamaduni ni Baraza la Sanaa la Taifa(Basata).

Kukua kwa muziki na kutanuka kwa njia za mawasiliano kumechangia kuiamsha taasisi hiyo kuwa mstari wa mbele kuusimamia.

Pia, aina ya maisha ya wasanii wengi ikiwemo yale ya kujitangaza kwa kutumia vituko au ugomvi, maarufu kwa jina la “kutafutaKick”, yameifanya Basata kuwa kazini kila kila mara kujaribu kulinda maadili na utamadani wa Mtanzania.

Baadhi ya wasanii ambao waliiingia katika mgogoro na baraza hilo ni Roma Mkatoliki, Nay wa Mitego, Diamond Platnumz, Gigy Money na Rayvanny.

Pamoja na changamoto hizo, yapo mengine ambayo Basata imekuwa ikifanya, kama kuendesha semina na jukwaa la kila Jumatatu kwa ajili ya kuwakutanisha wasanii kuzungumzia mambo yanayohusu tasnia, kama changamoto na namna ya kuzitatua.

Hata hivyo, yapo mambo ambayo watu wamekuwa wakijiuliza kuhusu kazi zinazofanywa na baraza , changamoto wanazopitia bila ya kupata majibu.

Katika makala haya, baadhi ya maswali hayo yanajibiwa na katibu mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza wakati akihojiwa na jarida la Starehe.

Basata imelaumiwa sana kuhusu kanuni mpya zinazolipisha wasanii na waandaaji wa matamasha tozo zinazofikia Sh5 milioni, kiasi cha waziri husika, Dk Harrison Mwakyembe kulazimika kufanya vikao na wasanii kusikiliza maoni yao.

Wasanii hao wanasema sheria hiyo imekuja wakati Basata haichangii lolote katika kazi zao, ikiwaacha kama watoto yatima.

Lakini Mngereza anasema tozo ya Sh5 milioni ni kwa ajili ya kampuni na si wasanii na kwamba ni kwa faida yao.

“Hata hivyo, mambo hayo yameanza kufanyiwa kazi kwa waziri kukutana na wasanii kupokea maoni yao na sasa tayari lipo wizarani na hazitatumika mpaka hapo waziri atakapotangaza,” alisema Mngereza.

“Unajua marekebisho ya sheria au kanuni yana hatua ndefu kidogo. Pamoja na waziri kupokea mapendekezo, bado itabidi kuyapeleka kwa mwanasheria na ayaridhie. Hivyo, bado tunasubiri na vyovyote itakapoamuliwa jamii itataarifiwa.”

Hata hivyo Mngereza anasema wakati baadhi wakiwa wanalalamika, wasanii wengine wamekuwa wakifanya kazi pasipokuwa na mikataba, hivyo kanuni hiyo ya tozo itakuwa na faida si tu serikali bali na msanii mwenyewe.

Anasema kutumika kwa kanuni hizo pia kutasaidia kuangalia mikataba waliyoingia kama ni sahihi, yaani kuhakikisha pande zote mbili zinafaidika.

Kilimanjaro Music Award kufufuka

Mngereza pia alizungumzia suala la kudorora kwa matamasha ya kutuza wasanii yaliyokuwa yakifanywa na taasisi binafsi, akisema ukimya huo umetokana na ukweli kwamba kuendesha tuzo si lelemama.

“Ni kitu chenye gharama kubwa,” alisema Mngereza.

Hata hivyo, anasema kuna mpango wa kurejesha baadhi, kama Tuzo za Kilimanjaro (TKMA) na kwa sasa wanasaka mdhamini.

Tuzo hizo, zilizokuwa zikidhaminiwa na Kilimanjaro Premium Lager, zilianzishwa na msanii wa Bongo Fleva anayeitwa Cool James lakini alipofariki waendeshaji wakabadilika hadi zilipochukuliwa na Basata na baadaye kutoweka.

Mngereza alisema kuyumba kwa tuzo hizo kulitokana na mdhamini kujitoa.

Miss Tanzania imeonyesha mwanga

Kwa upande wa mashindano ya warembo, Mngereza anasema pamoja na udhaifu uliojitokeza katika shindano la Miss Tanzania, anaona anaona matumaini yakirudi baada ya kuchukuliwa na mrembo wa zamani, Basila Mwanukuzi.

Anasema Basata imeridhika na kilichofanywa na Basila kupitia kampuni yake la The Look, baada ya mshindi kukabidhiwa zawadi yake na pia hakukuwepo na malalamiko dhidi ya mshindi.

Kuhusu shindano jingine la Miss Utalii, ambalo liliwahi kuvuta hadi shindano la dunia hapa nchini, Mngereza alisema muandaaji bado hajafanyia kazi makosa aliyoyafanya na mpaka sasa hajaonyesha nia ya kurudi.

Awaonya wanaotafuta ‘kick’

Kuhusu Basata kufungia baadhi ya nyimbo kutokana na kutofuata maadili, Mngereza alisema huwa wanawaita wasanii wenye nyimbo hizo kuongea nao, lakini wengine hujipakazia.

“Utaitwa kwa kufuata kanuni na taratibu na mimi naahidi kusimamia sheria na hakuna tutakayemuonea. Lakini kwa wale wanaojitangazia tumewaita kwa lengo la kutafuta kiki, aache,” alisema.

Advertisement