Kauli za majaji Samatta, Ramadhan zifanyiwe kazi

Wednesday July 11 2018

 

Hayati Lord Denning (1899-1999) ambaye alikuwa Jaji wa Uingereza, aliwahi kusema kuwa yanapotolewa madaraka makubwa kwa vyombo vya dola kuna hatari kubwa kwamba yanaweza kutumiwa vibaya.

Jaji Denning, mwanamapinduzi aliyepanua mtazamo wa mahakama nyingi za Jumuiya ya Madola alitoa kauli hiyo akisisitiza umuhimu wa utawala wa sheria kwa watawala.

Nimefarijika sana nilipowasikia majaji wakuu wastaafu, Barnabas Samatta na Augustino Ramadhan wakitembea na maneno ya Jaji Denning kutokana na uwepo wa viashiria visivyo vya afya nchini.

Majaji hao ambao wametumikia taifa hili kwa uadilifu mkubwa, walitoa ya moyoni katika kikao alichokiitisha Rais John Magufuli kati yake na viongozi wakuu wakiwamo marais wastaafu.

Kikao hicho kilichofanyika Ikulu Julai 3,2018, mbali na marais wastaafu, kilihudhuriwa pia na mawaziri wakuu wastaafu, maspika wastaafu na majaji wakuu wastaafu.

Jaji Samatta alienda mbali zaidi na kueleza kuwa shughuli zote zinazofanyika nchini ziwe za kiuchumi au zozote zile, ni lazima ziwe ndani ya utawala wa sheria na ni lazima ziambatane na haki kwa raia.

“Mie wakati mwingine ninapotizama TV na kusikia baadhi ya viongozi na amri wanazozitoa hasa Ma-DC (wakuu wa wilaya) najiuliza wakati mwingine sheria iko wapi,” alisema.

Nimeamua kuwanukuu wasomi wetu hao pamoja na Jaji Denning kwa sababu nchini mwetu kuna viashiria vingi vya kukiukwa kwa misingi ya utawala bora na utawala wa sheria.

Mfano mzuri ni wa wiki iliyopita ambapo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola alipoagiza kushushwa cheo kwa ofisa mmoja wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Mbeya.

Kwanza yeye sio mamlaka yake ya nidhamu lakini kubwa ni kwamba huwezi kumwadhibu mtu mwingine kwa kosa la jinai lililotendwa na mtu mwingine tena bila hata ya kusikilizwa.

Jambo ambalo limenifanya nipate kizunguzungu zaidi ni hatua ya Waziri kuwaagiza wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kutumia ilani ya CCM kutekeleza majukumu yao badala ya sheria.

Katika kipindi cha miaka miwili sasa, tumeshuhudia matukio ya ajabu ya wateule wa Rais hasa Ma-DC, wakitumia vibaya madaraka yao kuwaweka mahabusu viongozi na wananchi kwa saa 48.

Baadhi ya maamuzi yanayofanyika kwa kuwapendeza watu fulani ambao bila kufanya hivyo itakuwa hasara ya kisiasa, unakuta sheria inawekwa pembeni na siasa inachukua mkondo wa sheria.

Wakati mwingine, maamuzi yanafanywa kwa woga kukidhi mahitaji ya kisiasa ya wakati husika, na sio kwa kuheshimu sheria ambayo haipindi haki wala wajibu. Tukiacha hali hii iendelee ni hatari sana.

Dhana kwamba ni vema watu watawaliwe na sheria imeanza zamani za kale. Mwaka 1760, Mfalme wa Babylon, Hammurabi alitengeneza sheria za nchi yake na kuzipa uzito mkubwa.

Aristotle aliyekuwa mwanafalsafa wa Kigiriki aliyeishi zaidi ya miaka 2,000 iliyopita, naye alitamka maneno haya: “Utawala wa sheria ni bora kabisa kuliko utawala wa mtu binafsi”.

Malalamiko tunayoyasikia leo ya kuzuiwa kwa mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa, ukiukwaji wa haki za binadamu, utesaji na utekaji wa watu yote msingi wake ni kukiukwa kwa utawala wa sheria.

Tangazo la Umoja wa Mataifa la mwaka 1948 kuhusu haki za binadamu linatahadharisha kwamba watu wanaweza kulazimika kuasi ili kupinga dhuluma, maonevu na ukandamizaji.

Haya hutokea mahali ambapo utawala wa sheria haupo na ni wazi kwamba utawala wa sheria unapotoweka, matokeo yake ni machafuko, fujo na maasi na hili ndilo Jaji Ramadhan analiona mbele yake.

Pengine ndio maana, Jaji Ramadhani anasema Serikali iangalie haki na ikishafanya hivyo amani itajiangalia yenyewe.

Serikali ya CCM chini ya Rais Magufuli itambue kuwa imebeba dhamana kubwa ya amani ya nchi hii na ni wao pekee watakaoamua kama Tanzania iendelee kuwa kisiwa cha amani ama la.

Advertisement