Kazi yetu ni moja tu, kugawana timu za kushangilia

Muktasari:

  • Alhamisi ya wiki hii (Juni 14), Fainali za Kombe la Dunia 2018 zitaanza rasmi na kumalizika Julai 13 mwaka huu huku timu 32 zikiwania kutwaa ubingwa wa dunia.

Kila mara zinapofanyika Fainali za Kombe la Dunia ni kawaida yetu Watanzania kuchagua timu za kushangilia kwani timu yetu ya Taifa haijawahi kufuzu kushiriki fainali hizo tangu zilipoanza 1930.

Alhamisi ya wiki hii (Juni 14), Fainali za Kombe la Dunia 2018 zitaanza rasmi na kumalizika Julai 13 mwaka huu huku timu 32 zikiwania kutwaa ubingwa wa dunia.

Mechi zitaanza siku hiyo pambano la wenyeji Russia kukwaana na Saudi Arabia lakini timu za Afrika, Misri na Tunisia ni siku ya pili yake.

Fainali hizo kubwa, za pekee na za aina yake kwa timu za taifa, hufanyika mara moja kila baada ya miaka minne, mara ya mwisho zilifanyika Brazil mwaka 2014, na Ujerumani ilitwaa taji baada ya kuichapa Argentina bao 1-0 katika mechi ya fainali kwenye Uwanja wa Maracana.

Baada ya kumalizika kwa fainali hizo za dunia huko Brazil, watu wengi tulitarajia Tanzania, pia itaanza mikakati ya muda mfupi na mrefu kuhakikisha tunafuzu kushiriki fainali za 2018 na 2022.

Hata hivyo, hilo halikufanyika na tukajikuta tunatolewa mapema katika hatua ya kufuzu kushiriki fainali za 2018, na wala hatuna programu za kuhakikisha tunafuzu Fainali za Dunia 2022!.

Siku zote hakuna kinachoshindikana wala njia ya mkato, kinachotakiwa ni kuanza programu za muda mrefu sasa, kwani programu ya miaka minne ingawa ni kipindi kifupi, walau inaweza ikatusaidia kufikia malengo yetu ya kufuzu 2022.

Kucheza Kombe la Dunia kunahitaji mipango, malengo na maandalizi ya wachezaji kwa muda mfupi na muda mrefu, lakini siyo kufanya maandalizi kwa hisia au maandalizi ya zimamoto.

Hatuwezi kufuzu kama hatuna dhamira ya dhati kufikia malengo hayo. Tunatakiwa tuandae wachezaji vijana wa umri tofauti wenye vipaji wanaoweza kushindana katika kiwango cha juu.

Kama ni mtu unayefuatilia wachezaji wetu wa Tanzania wanapocheza mechi mbalimbali za kimataifa, lazima utabaini wachezaji wetu wa kizazi hiki wanakosa mambo matatu.

Mambo hayo ni akili ya mchezo, mwili sahihi na stamina. Wachezaji wanatakiwa kutumia akili nyingi kutoa pasi na kupokea mpira, kufunga mabao, kuzuia, kushirikiana, kukokota mpira, kupiga mashuti, kuusoma mchezo kwa haraka, kutumia mipira iliyokufa, kujiamini na kufanya uamuzi wa haraka.

Wachezaji wetu wanatakiwa pia kuwa na stamina itakayowawezesha kuwa na nguvu na kasi hali itakayowawezesha kucheza soka la kuvutia na kuuzungusha mpira kwa haraka uwanjani katika mpangilio wa hali ya juu.

Vilevile wachezaji wetu wanatakiwa kuwa na miili ambayo imefanyishwa mazoezi kwa ajili ya kupambana ili kupata ushindi.

Hali hiyo itaonyesha wachezaji wanaotambua umuhimu wa vipaji vyao na kutunza miili yao.

Ukiacha hayo mambo matatu, pia wachezaji wetu wanatakiwa kujua umuhimu wa kujituma, uzalendo na kulipigania taifa, kuacha ubinafsi na kushirikiana kutafuta ushindi kwa lengo moja.

Mimi huwa naamini hakuna kinachoshindikana chini ya jua, kwa hiyo bado naamini ipo siku Tanzania itafuzu kucheza Kombe la Dunia, lakini siyo kwa mipango hii tuliyonayo hivi sasa!.

Ni lazima kujifunza kutokana na makosa tunayofanya mara kwa mara, kwani bila kufanya hivyo hakuna linaloweza kufanikiwa na fainali hizo za Kombe la Dunia zitaendelea kuwa ndoto kwetu.

Dah, nitafanyaje sasa, Tanzania haipo, kwa hiyo kama ilivyo kawaida yetu, kuanzia wiki hii tutaanza kugawana timu za kushangilia katika Fainali za Kombe la Dunia 2018 zinazofanyika Russia.

Mimi nitazishangilia Morocco, Brazil na Ufaransa..., wewe utashangilia timu zipi?.