Kibamba: NEC ilazimishe vyama kuteua walemavu

Wednesday March 13 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba , Deus Kibamba ameishauri Tume ya ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuweka mkazo kwa vyama vya siasa kuwa na wagombea wenye ulemavu.

Alisema jambo hilo likiwa kigezo cha kupitisha orodha ya wagombea wa chama husika itahamasisha vyama kuwakumbuka watu wenye ulemavu.

Kibamba aliyasema hayo wakati akitoa mada kuhusu wanawake na siasa kwenye kongamano la Jukwaa la wanawake wenye ulemavu Tanzania lililoandaliwa na Mfuko wa Asasi za kiraia (FCS).

“Sasa hivi hakuna sheria inayolazimisha walemavu wawepo kwenye ngazi ya maamuzi, hata kama suala hili halijafungwa ifikie wakati wapewe kipaumbele kwa kuwa wapo wanaoweza kufanya makubwa na mazuri kuliko hata wazima.

“Ikitokea siku moja mimi nimekuwa mwenyekiti wa Tume ya uchaguzi katika nchi hii nisingepitisha orodha ya wagombea inayoletwa na vyama vya siasa bila kuwepo walemavu,” alisema.

Alisema ni muhimu kuwa na kigezo maalumu kwa vyama vya siasa ambavyo vinategemea kupitishwa orodha ya wagombea wake na tume kuweka mchanganyiko wa wagombea utakaohusisha walemavu.

Mwenyekiti wa jukwaa hilo, Nuru Awadh alieleza kuwa bado wanawake wenye ulemavu wanakabiliwa na changamoto lukuki zinazochangia kuwafanya washindwe kusonga mbele.

Alizitaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni jamii kutokuwa na imani nao na kuonekana hawawezi hasa katika kipindi cha chaguzi.

Nyingine ni wanawake wenyewe kutojikubali na kujirudisha nyuma katika masuala ya msingi kwa madai wa hali zao.

“Tunatathmini tunakoelekea na nafasi yetu kama wanawake wenye ulemavu, ni muhimu kwetu kuamka na kuacha unyonge tukapambane na wengine bila kujali hali zetu,” alisema Awadh

Advertisement