NDANI YA BOKSI: Kifo cha Nyerere, sanaa na wanasanaa kibao

Samora Avenue. Nakatiza kijivuni utadhani mimi ni mkaazi wa Ikulu ya Magogoni. Mvua zinanyesha lakini haifanyi nisipige misele ‘tauni’. Kila sura mbele yangu ni ngeni. Nagundua wengi wametangulia mbele ya haki, majukumu yamewatinga au wamehamia makao makuu ya nchi kule Dom.

Achana na majengo, maua na usafi wa barabara. Kivutio kikuu cha Dar ni madem. Ewe binadamu uliye nje ya jiji hili usikubali mtu akudanganye kuwa madem wa Pasiansi au Isevya na Kantalamba ni sawa na wa Sinza au Keko Toroli. Dem wa Njiro au Sakina anayejiona mrembo zaidi, akifika Kurasini tu atajiona wa kawaida sana.

Nipo Daslama mjini ‘long time’ kitambo. ‘Levo’ za ‘Jenerali’ labda wewe ndo mgambo lakini nashindwa kuwazoea viumbe wa kike siku zote wananivuruga akili. Nikiwa nje ya Dar kwa wiki moja tu ninaporudi kuanzia Kiluvya naanza kuhusudu kila kiumbe cha kike.

Ndo hali niliyokuwa nayo Mtaa wa Samora kila dem nikimuona, ananishawishi nigombane na familia yangu, niwaambie nyumba yetu ya Mtwivira Iringa iuzwe pesa tugawane na mgao wangu wanipe nihonge madem. Mtoto kama Uwoya nitamshawishi kwa kipi? Pesa tu.

Brother Kim, wa Kim & The Boys. Mwanzilishi wa Yo Rap Bonanza, shindano la rap za Kiswahili enzi hizo. Uwe umekula chumvi nyingi katika game la Bongofleva ili uelewe. Ni Ruge wa enzi hizo aliishi nyuma ya Bilcanas, ukipita lazima ungemkuta. Utasimama akupe michapo ya mjini mipya kisha unaachana naye. Kim hatupo naye.

Kama Ruge, ambaye kwa mara ya kwanza Fiesta inafanyika bila uwepo wake sisikii neno fursa wala vionjo ambavyo angekuwepo tungesikia. Katika dunia ya sasa ambayo mastaa kibao wamezaliwa mwezi huu yaani ‘Team Libra’ akiwamo Jakaya Kikwete Rais Mstaafu, lazima Ruge angefanya kitu.

Dunia ya instagram vituko na maisha ya kasi kama msafara wa Magufuli? Ngwair kamwe asingeacha haya yapite. Kuna ngoma zingehusika na maisha ya sasa lakini hayupo Mzee wa ‘Mikasi’ na ‘Kukesha kama CNN’. Dunia inapoteza watu wengi wenye akili ya kufikiri kupitia mashairi na midundo. Ngwair sanaa imelala naye pale Kihonda.

Wakati tunaadhimisha miaka ya 20 kifo cha Nyerere unajua kama Vivian na Complex wana miaka kama 13 bila uwepo wao? Amina Chifupa miaka kama 11 tangu alipoamua atuache. Vipaji katika umri mdogo vimetuacha. Kuna Sharo milionea na Kanumba, wana miaka saba bila uwepo wao na sisi.

Tangu aondoke Kanumba na Sharo milionea kuna kipya kipi? James Dandu ana miaka mingi ardhini toka aondoke kwa ajali, wazo lake la tuzo za muziki, nalo limekufa. Hakuna tuzo tena si watayarishaji muziki wala wanamuziki wote wapo tu wanatazamana.

Steve 2K Msela wa Tanga ambaye kisu kiliondoa uhai wake miaka kadhaa nyuma. Vipi kuhusu John Mjema na ‘Wachumba wake 30’? Pia usisahau Mzee Small, King Majuto, wote hawapo. Waliotuongezea siku za kuishi tukitanua mbavu na mapafu kwa vicheko.

Sam Wa Ukweli na ‘Prodyuza’ Pancho Latino. Kuna Swahiba wetu Jebby, hatunaye kama ambavyo YP wa TMK Wanaume Family, aliamua kusepa bila kutuaga. Tunapomkumbuka Nyerere wana sanaa tusimsahau Mzee Gurumo, Tx Moshi William, Seleman Mbwembwe, Maina na Mzee Kassim Mapili.

Banza Stone katuachia dunia yetu. Vipaji halisi vya muziki. ‘Mtoto wa Kiume’ Geez Mabovu, Mez B mwana Chamber Squard, Abou Semhando ‘Baba Diana. MCD aliyefanya tumba ziimbe na Amigolas. Vipi kuhusu yule kiumbe aliyefanya twende Twanga bila kupenda? Namaanisha Aisha Madinda.

Sanaa imepoteza wengi tangu Baba wa Taifa alipoaga dunia. Kuna sauti ya pande la mtu lililokwea hewani. Fundi wa kwaya na sauti yenye mkwaruzo, ambaye msiba wa Nyerere uligeuka sherehe kwa tungo zake tamu Kapteni John Komba. Katuachia urithi mzuri wa sauti kila tunapoadhimisha kifo cha Mwalimu.

Ukimuona Mr Blue Kabyser, kuna kivuli cha mtu nyuma ya mafanikio yake. Namuongelea Roy Bukuku. Mikono na akili yake ilituzalishia kiumbe hiki pendwa kwenye ‘gemu’ la Bongo fleva. Roy alifanya nywele za P Funk Majani, zisichanike kwa kitana wala chanuo kila alipoachia ngoma. Alikuwa fundi na nusu.

Wako wengi wanasanaa walioondoka tangu Mwalimu atuache. Hata yeye alikuwa mwana sanaa ndo maana kila shirika na idara nyeti za umma zilikuwa na bendi ya muziki zikiwamo Bima, Polisi, Uhamiaji, JKT, DDC, ‘Tankati’ Alamsi, Vijana Jazz, Nuta baadaye Juwata ambao leo mnawaita Msondo.

Kabla sijatokeza Posta kupitia uchochoro wa jengo la Rita. Napigiwa honi kwa fujo, nakunja ndita kama Prof Jay na honi za Vicky. Nataka nigeuke na kufoka mara nahema juu juu. Kumbe ni mchizi wangu mmoja wa kitambo toka tunakimbizwa na Afande Masawe pale Jitegemee. Natabasamu.

Baada ya salamu na honi za magari nyuma yake yenye haraka zaidi. Ananiomba anipeleke ninakoenda. Sikusita nikajitoma ndani ya ndinga. Stori nyingi huku mioyo na bongo zetu zikichangamshwa na sauti ya Nandy. Naanza kumsifia Nandy kibwege bwege tu.

Kibwege kwa sababu sisifii muziki wake. Nimejikita kwenye idara ya urembo wake na kishepu flan hivi. Mwana kama hanielewi hivi, nami nampuuza kutonielewa kwake naendelea na kubwabwaja sifa kibao kwa mtoto Nandy. Kwamba mbali ya urembo pia kana akili sana.

Alionyeshwa njia na jamaa kama walivyoonyeshwa kina Mwasiti, Recho, Vumilia, Nandy, Ray C na wengineo. Lakini Nandy anabaki kuwa alama sahihi ya mtu aliyekariri njia na kunyooka nayo. Mchizi wangu simuelezi hayo. Nilijikita kwenye eneo moja tu kwamba nakaelewa kale kamanzi.

Achana na wanaosubiri mtu asepe mbele za haki ndipo wamsifie kibwege. Mie nasifia ‘ini advansi’. Ndo maana siendi kwenye shoo zake. Najijua mizuka yangu. Sitaki yajirudie yale ya mwaka 2005, uzinduzi wa albamu ya Twanga Pepeta pale Diamond Jubilee. Kuna tukio lingine niliwahi kulifanya pale Sheraton. Kizazi cha Kikwete mnaita Serena. Uzinduzi wa albamu kadhaa toka Smooth Vibes. Sasa THT. Stara Thomas, Fina Mango wa tatu simkumbuki. Wakati huo Jide kishakuwa mkubwa akijitegemea shoo zake. Ray C alikuwa ‘prizenta’ tu pale Clouds.

Moja kati ya shoo zilizobeba lundo la totozi za mjini, walikuwa wengi kuliko nyasi za bustanini pale Serena. Hata ungeingia bila kupaka hata ‘Deodoranti’ ungetoka unanukia manukato.

Wakati namsifia Nandy jamaa hakunielewa. Alianza kuhisi labda kabeba kichaa, lakini aliaminishwa na pamba zangu. Yeye alikuwa na gari mimi pesa za gari kama lake niliwekeza kwenye pamba na viatu nilivyotupia mwilini. Nampendaje Nandy? Aliuliza akishangaa, akiamini simuwezi kwa lolote.

Ikabidi nimchane mshikaji aache uboya. Kwamba ndoto ya kiume hufikiria kumzuzua dem yeyote unayemzimia. Huhitaji kuwa tajiri kuzuzua dem si jambo kubwa vile. Wengi hushindwa kwa sababu wanatumia mbinu zilizopitwa na wakati ama mitindo ambayo haikubaliki.

Kama hujiamini wewe mwenyewe ama unajiona huwezi kumfurahisha mwanamke. Je unatarajia mwanamke akupende? Kama unataka kumzuzua dem jiamini kama mwanaume. Njia rahisi ni kupendeza, marashi ya kunukia, na kuwa nadhifu. Kuwa mcheshi. Kama una kipawa cha ucheshi ama kumfanya dem avutiwe nawe basi ni silaha kubwa. Ukijua huyu ndiye unayemzimia katikati ya lundo la madem. Cha kufanya ni kumuangalia machoni mpaka aone aibu ya kukuangalia. Kufanya hivi kunavuta ‘atensheni’ yake. kutaka kujua kwa nini? Atataka umsemeshe au akusemeshe. Usitumie mbinu hii kibwege kila mara na kila sehemu. Mwingine waweza kumuogopesha na kukuona punguani, hayawani, zuzu, bwege, tutusa, taahira, mbumbumbu, karai, pimbi. Au mshirikina wa kimkurabita.