Kiko wapi kipimo halisi cha utendaji wa wabunge, wawakilishi kisiwani Pemba

Muktasari:

Ni katika muktadha huu wananchi hao wanalala na kuamka wakisubiri maendeleo na huduma ya bora za afya na upatikanaji wa maji safi na salama.

Ni kwa imani tu, wananchi wa Pemba wana matumaini kwamba siku moja nyota ya matumaini itachomoza na kung’arisha maisha yao, kwamba kupata maendeleo waliyoyasubiri kwa miaka mingi.

Ni katika muktadha huu wananchi hao wanalala na kuamka wakisubiri maendeleo na huduma ya bora za afya na upatikanaji wa maji safi na salama.

Pemba, ni kisiwa kilichobeba jina kubwa katika ukanda huu wa Afrika Mashariki kutokana na sifa yake ya uzalishaji wa karafuu, zao ambalo linategemewa kwa kiasi kikubwa na Serikali ya Zanzibar katika kuingizia pato la kigeni, lakini hali ya wakulima bado ni tete kimaisha.

Unaweza kujiuliza utete wa hali hiyo unatokana na nini wakati kisiwa wenyewe ni kidogo na chenye wakazi wasiofika hata laki tano, kwa mujibu wa sensa watu na makazi ya mwaka 2012?

Ni tafakuri ya aina hii ndio iliyotawala kichwani mwangu na kuamua kufunga safari hadi kisiwa cha Pemba ili kujua ni kwa namna gani wabunge na wawakilishi, licha ya wajibu wa Serikali, wao wanatekeleza majukumu ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Upatikanaji wa huduma muhimu

Ukifika Pemba utakaribishwa na kundi la kina mama wakiwa na ndoo za maji kichwani. Hata kwa macho tu, katika baadhi ya maeneo utaona kwamba maji yale si safi

Masikini, maji yaliyogeuka rangi na kuwa kahawia yalikua yamejaa kwenye ndoo hufuatwa umbali mrefu kutoka katika makazi yao.

Khadija Said, mkaazi wa Wambaa kwa Azani anasema wanatumia karibu mwendo wa dakika 50 kutoka majumbani mwao hadi lilipo bwawa ambalo huchota maji kwa ajili ya matumizi yao.

Anasema maji hayo yanayoonekana si safi na wakazi wa mijini hawawezi kuyatumia hata kunawa mikono, ila kwao wameyazoea kwa miaka mingi tangu waishi kwenye eneo hilo zaidi ya miaka 60.

Mize Said ni miongoni mwa wakazi wa eneo hilohilo, anasema upatikanaji wa maji kwao bado kitendawili kisichoteguliwa vizazi kwa vizazi hadi leo hii.

Anasema katika umri wake wote wa miaka 40 tangu kuzaliwa kwake hadi sasa anafahamu eneo hilo kuwa na shida ya maji bila ya kutatuliwa huku kadhia kubwa ikiwemo pia upatikanaji wa maji yenye chumvi kwa baadhi ya maeneo wanapochimba visima.

Hata hivyo, Mize anaamini kuwa wenye mamlaka katika kisiwa hicho hawajashindwa kutatua changamoto hiyo isipokua kujisahaulisha kwao ndilo jambo linalowaletea shida wananchi.

Kauli ya Mize inaibua haja ya kuwafuatilia wabunge na wawakilishi na wanaosimamia mifuko ya maendeleo majimboni katika wilaya hiyo ya mkoani.

Mkurugenzi wa Baraza la Manispaa katika wilaya ya mkoani, Rashid Abdalla Rashid anasema pamoja na kuwapo mifuko hiyo ya majimbo manne katika eneo lake, hali bado hairidhishi kimaendeleo.

Anasema miongoni mwa sababu zinachangia hali hiyo ni uwajibikaji mdogo wa wabunge na wawakilishi majimboni mwao jambo ambalo kwa kiasi kikubwa ndio sababu ya matatizo yasiokwisha.

Imani ya Rashid ni kwamba wabunge wengi husahau wajibu wao mara baada ya kuchaguliwa na kuhamisha makazi yao kutoka maeneo yao halisi na kuhamia Unguja au Tanzania Bara, jambo ambalo linawasahaulisha matatizo ya wananchi.

Mkurugenzi huyo anasema ukosefu wa wataalamu katika kamati nyingi za maendeleo za jimbo pia ni sababu za kutokuwapo mabadiliko ya kimaendeleo.

Alisema katika kisiwa cha Pemba ni jambo la kawaida kuona wajumbe wa kamati hizo za maendeleo jimboni ambao hawakufika hata kidato cha nne, lakini kwa ushabiki tu ndio wameteuliwa.

‘’Majimbo ya wenzetu yamekusanya wataalamu wa kila aina wa kuandika miradi, sisi huku Pemba ni nadra sana kukuta watu wenye mfano huo na ndio maana kila mtu husubiri fedha za Bunge ili zilete maendeleo lakini hakuna hata mmoja anayeweza kuandika miradi na kumpatia mbunge wake,” anaongezea Rashid.

Pamoja na hayo, Rashid anasema mfumo wa kisiasa katika kisiwa hicho bado ni tatizo kubwa ambapo wananchi wanaamini zaidi vyama vyao kuliko maendeleo.

Anasema iwapo ukiitisha mkutano kujadili maendeleo kwenye maeneo husika, unaweza kukutana na watu kumi lakini mikutano ya kisiasa wananchi ndio wanayojazana kwenda kusikiliza.

Kilio cha aina hii hakipo tu kwa wananchi wa Shehia ya Wambaa pekee, bali yapo katika maeneo mengine ambayo yamekuwa yakikosa huduma muhimu kwa wakati muafaka.

Kwa kawaida kila kiongozi wa chama cha siasa, awe mbunge au mwakilishi, kabla ya kuchaguliwa huweka wazi ahadi na vipaumbele vyake, pamoja na kunadi ilani ya chama chake cha siasa.

Jambo la kujiuliza ni wanasiasa hao baada ya kuchaguliwa hutekeleza ilani ya vyama vyao na kukamilisha ahadi walizotoa?

Mbunge wa Mtambile Mkoa wa Kusini Pemba, Massoud Abdalla anasema yeye hujitahidi kufanya yale yaliyo ndani ya uwezo wake kila wakati unaporuhusu, licha ya kukiri kuwa zipo changamoto mbalimbali katika utekelezaji huo.

Anataja changamoto hizo kuwa ni pamoja na kiasi kidogo cha fedha za mfuko wa majimbo zinazotolewa kila mwaka ambacho hakitoshi kuwaletea wananchi maendeleo ya msingi.

Kwa mfano, anasema Wilaya ya Mkoani inapata Sh103 milioni kila mwaka huku wilaya hiyo ikiwa na majimbo manne, tena makubwa, jambo ambalo alidai haliwezi kutatua changamoto zote za wananchi, bali kuzipunguza.

Anataja baadhi ya miradi ambayo imetekelezwa katika mwaka huu kuwa ni uezekaji wa majengo ya skuli ya sekondari kengeja na kufikisha umeme katika kijiji cha Mwanda na Mgonange katika jimbo la Mtambile.

Kwa upande wa jimbo la Kiwani alitaja ujenzi wa pekee kisima cha maji huku jimbo la Mkoani wananchi wakifaidika na ujenzi wa barabara katika Shehia ya Tironi ambapo jimbo la Chamgani wamepata umeme katika eneo la Mawini.

Miradi hiyo imegharimu zaidi ya Sh103 milioni huku baadhi ya miradi ikishindwa kukamilika na kukosekana kwa fedha mbadala.

Kwa kawaida kila chama cha siasa visiwani hapa ikifika muda wa kunadi sera zake huweka wazi ilani ya vyama yake lakini je, wabunge na wawakilishi wanafuatiliwa na vyama vyao katika utekelezaji wake?

Dk Shein avunja ukimya

Katika mazingira kama hayo ya kuhakikisha viongozi wa vyama vya siasa wanafuata ilani za vyama vyao, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein anasema chama hicho hakitakua tayari kuwarudisha tena wabunge na wawakilishi wanaoshindwa kutekeleza wajibu wao majimboni.

‘’Mimi nikiwa kama makamu mwenyekiti nitahakikisha fomu ya mbunge au mwakilishi asiyewajibika kwa wananchi wake jina lake halipiti na fomu nitaichana,” anasema.

Utakumbuka kuwa kwa miaka mingi kwenye ardhi ya Zanzibar Chama cha Wananchi (CUF) ni chama ambacho kimekuwa kikitoa ushindani mkubwa kwa chama tawala kila baada ya miaka mitano ya uchaguzi mkuu na hufaidika na kupata wabunge na wajumbe wengi wa baraza la wawakilishi, ambao huwakilisha kwenye vyombo vya kutunga sheria katika majimbo yote ya Pemba.

Hata hivyo, swali lakini la kujiuliza je, viongozi wao wana kawaida ya kufuatilia utekelezaji wa ilani ya chama kwa wabunge wao?

Mkurugenzi wa habari uenezi na uhusiano wa umma wa CUF, Salim Bimani anajibu swali hilo akisema chama hicho kimekua kikifuatilia utekelezaji wa majukumu ya wabunge kwa kila hali inaporuhusu na wamekuwa wakiwakumbusha wajibu wao kila baada ya muda.

Anasema iwapo baadhi ya wabunge hawatekelezi ilani ya chama si kwa maagizo ya chama hicho, bali hufanya hayo kwa matakwa yao wenyewe na wananchi waliowachagua hupima utendaji wao.