Kilimo cha nanasi safi, tatizo soko

Muktasari:

  • Wakati wa msimu wake, aghalabu kila genge hutokosa tunda hili. Vijiwe vya wachuuzi barabarani navyo huongezeka. Ukiona hivyo ujue msimu wa mananasi umewadia.

Japo sasa yameanza kupungua sokoni, lakini ufikapo msimu wake, lazima utambue kuwa sasa ni wakati wa mananasi.

Wakati wa msimu wake, aghalabu kila genge hutokosa tunda hili. Vijiwe vya wachuuzi barabarani navyo huongezeka. Ukiona hivyo ujue msimu wa mananasi umewadia.

Hata hivyo, uzalishaji wa zao hili una sura mbili ya kicheko na huzuni. Kicheko ni pale mkulima anapovuna matunda ya kutosha shambani baada ya safari ya zaidi ya mwaka ya tunda hilo kukua na kukomaa shambani.

Huzuni ni pale mkulima anapokuwa na mzigo mkubwa wa matunda hayo, lakini akakwazika kuyauza ama kwa kukosa soko kabisa au kupata soko analohisi litamlalia kimaslahi.

Kisa cha Mwajuma Mbwana

“Niliwahi kujuta, kwa nini nalima mananasi, na hii ilitokana na zao hili kukosa soko, kwani mananasi mengi yaliharibika kwa kuoza kutokana na kukosa wateja, lakini baadaye nikajipa moyo kuwa acha niendelee tu kulima maana ndio zao langu la kibiashara ninalolitegemea huku kwetu Chalinze,” anasema Mwajuma Mbwana.

Mwajuma ambaye ni mkulima wa mananasi, kutoka eneo la Kiwangwa, Chalinze mkoani Pwani, anafafanu kuwa mwaka 2017, hakupata faida yoyote ya zao hilo, kutokana na mananasi kuwa mengi hali iliyosababisha mananasi yake kuoza kwa kukosa wateja.

Anabainisha kuwa licha ya mananasi kuwa na faida nyingi katika mwili wa binadamu, bado zao hilo halina soko la uhakika.

Anasema yeye alianza kulima mananasi mwaka 1993, na moja ya changamoto inayowakabili wakulima wa zao hilo ni uhaba wa masoko ya uhakika hali inayochangia baadhi yao kukata tamaa ya kuendelea kulima zao hili.

Anafafanu kuwa gharama za kilimo cha mananasi ni kubwa ukilinganisha na bei wanayouzia kwa sasa, ambapo mteja akienda shambani anauziwa nanasi moja kwa bei ya Sh 250 hadi 300, kwa nanasi moja.

“Wateja ni wa kugombania, hivyo mananasi mengi kuharibika kutokana na wateja kuwa wachache” anabainisha.

Anasema changamoto nyingine ni uhaba wa viwanda vya kusindika zao hilo, kwani viwanda vinavyonunua zao hilo ni kiwanda cha Sayona na Bakhresa, ambavyo hata hivyo hawawezi kununua mananasi yote kwa sababu ni mengi na wao wakitoa oda, wakulima wanagombania kupeleka kiwandani na wakati mwingine unakuta foleni ni kubwa hadi mananasi yanaharibika.

Anasema mananasi yake huuza viwandani kwa bei ya kutupa ya kuanzia Sh 325 hadi 400 kwa kilo moja.

Jinsi fedha inavyotumika kulima nanasi

Mwajuma analima heka moja kila mwaka, na kwa kawaida nanasi linachukua miezi 18 tangu linapolimwa hadi kuvunwa.

“Mimi nilianza kwa kulima heka moja ya mananasi ambayo ukipiga mahesebu kwa hii heka moja unatumia gharama zaidi ya Sh milioni moja, ambayo ni maandalizi ya shamba, vibarua wa kupanda na kupalili pamoja na mbolea,”anasema.

Anafafanu kuwa heka moja ya mananasi inaingia miche ya 15,000 na kila mche huwa ananunua kwa Sh 50, ukiondoa gharama nyingine kama usafiri na nyinginezo.

Mwajuma anaeleza kuwa mbali na fedha ya kununulia miche, pia anatakiwa hulazimika kutoa Sh 300,000 kwa ajili kumlipa kibarua ambaye husafisha shamba kwa maana ya king’oa visiki.

“ Pia natakiwa nitoe Sh 60,000 kwa ajili ya kulimiwa na trekta halafu tena natoa Sh 150,000 kwa ajili ya kupandiwa kitaalamu “anaeleza na kuongeza:

“ Baada ya miezi sita, unatakiwa kumwaga mbolea katika shamba hilo na hapo angalau unatakiwa uwe na mifuko nane ya mbolea yenye ujazo wa kilo 50, kila mmoja, japokuwa unatakiwa kuweka mbolea hadi mifuko 12, kwa heka lakini sio mbaya kama utaweka mifuko nane ya mbolea,’’ anasema.

Mwana mama huyo anafafanu kuwa, baada ya kulima mananasi, mkulima anatakiwa kupalilia mara tano, kwa msimu mzima hadi kuvunwa.

“Pesa inavyotumika ni kubwa sana, mifuko tu ya mbolea inagharimu Sh 380,000 wakati kibarua anayepalilia heka moja kwa awamu zote tano unatakiwa kumpa Sh 400,000, ndio maana wakulima tunalalamika, gharama za kilimo cha nanasi

Mkakati wa Serikali

Mkurugenzi Msaidizi kutoka Idara ya Maendeleo ya Viwanda, Mhandisi Elli Pallangyo, anasema moja kati mkakati iliyopo ni kukutana na wafanyabiashara wenye viwanda vya kusindika vinywaji kwa ajili ya kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo la wakulima.