UCHAMBUZI: Kiongozi asiyetaka upinzani ni ‘mpinga Mungu’

Maandiko ninayoyaamini mimi, wewe na viongozi wa dini walioenda Ikulu hivi karibuni yanatutaka tumsujudie Mungu mmoja muumba mbingu na ardhi. Na tusiabudu miungu mingine.

Zaidi tunajulishwa kuwa Mungu ni mwenye wivu. Anapenda kuabudiwa na kusifiwa yeye tu. Tusitaje bure jina lake. Na usisahau neno ‘’heshimu mamlaka mlizopewa duniani. Na pia Mungu wetu tumeelezwa ni mkali.

Kwa kufupi Mungu hapendi upinzani kabisa. Sasa kama kuna kiongozi hapa duniani ambaye hataki upinzani, ujue anataka ‘umungu’.

Yaani yeye ndiye mpinzani rasmi wa Mungu kwa kutaka ‘umungu’. Kiongozi asiyetaka mawazo mbadala, maana yake anataka asujudiwe, asifiwe na kuogopwa yeye tu. Kutotaka upinzani maana yake hataki tuabudu ‘miungu’ mingine.

Unakuta kiongozi anataka asifiwe tu. Kama ambavyo Mungu anatueleza tumuabudu na kumsifu. Kiongozi asiyetaka upinzani hukerwa na wanasiasa au wanahabari wanaothubutu kumkosoa au kusifia wapinzani wake. Anataka asikilizwe na asifiwe yeye tu. Wapo wanaowaita majina mengi mabaya ila mimi viongozi wa hivi nawaita wapinzani wakuu wa Mungu.

Ni wapinzani wa Mungu kwa kutaka ‘umungu’ wakati Mungu katuonya tusiabudu na kusujudia miungu mingine. Ni ‘miungu’ wanaotaka kupindua mamlaka ya Mungu duniani. Wanapenda kuwapa mamlaka na nguvu kubwa wasaidizi wao. Kwa maana ileile ya heshimuni serikali mlizopewa duniani. Basi nao wanatulazimisha tuheshimu na kuwaogopa wasaidizi wao kiserikali.

Mungu anatuasa kuwa usitaje bure jina la bwana Mungu wako. Sasa viongozi wasiopenda upinzani, wanakasirika sana kutajwa majina yao bure au kwa jambo ambalo siyo rafiki masikioni mwake au kwa wafuasi wake.

Kwa mfano kiongozi akikosea hataki akosolewe au kuelekezwa. Kwa sababu hataki kutajwa bure jina lake bila kulipamba na kulisifu kwa nyimbo na pambio za kutosha.

Ndiyo maana viongozi wasiopenda upinzani au kukosolewa na kutaka kusifiwa kila hatua, huishia pabaya. Kwa kuwa laana wanayopata haitoki kwa wapinzani wao, bali kwa Mungu ambaye hapendi uwepo wa ‘miungu’ wengine. Kiongozi anayetaka kusujudiwa tu, kupambwa tu, kusifiwa tu, na kutopingwa, huyo anataka ‘umungu’ na Mungu ni mkali. Lazima atamnyoosha tu.