Kiswahili kinakua duniani wakati sisi wenyewe tunakiharibu

Sunday January 6 2019Freddy Macha

Freddy Macha 

Kheri za 2019 zikufikie ewe unayepitia safu hii. Nakupa shukrani kwa kuendelea kuthamini gazeti letu la Mwananchi na wachapakazi wote wanaolitoa kila kukicha. Na leo Jumapili, tukumbushane thamani ya Kiswahili chetu.

Rais John Magufuli na Waziri wa Habari , Utamaduni, Sanaa na Michezo Harrison Mwakyembe, wamesisitiza nafasi ya Kiswahili duniani.

Kiswahili ni lugha ya kumi kati ya 6,000.

Hiyo ni hadhi ya juu sana ukizingatia kuwa Tanzania ni chimbuko na si nyingi za Kiafrika zilizo kwenye orodha.

Ndiyo maana Rais akaamua kuwa anatoa hotuba zake kwa Kiswahili ingawa anafahamu lugha kadhaa za kigeni.

Hapo hapo tuzingatie kuwa wakuzaji wa Kiswahili siyo tu sisi wananchi wa Afrika Mashariki na Kati bali pia viongozi, wanahabari, wasanii, waalimu na wataalamu mbalimbali.

Karibuni wale tunaotakiwa kukiimarisha Kiswahili tumekuwa tukikichezea na kukizorotesha. Mwaka 2002 Umoja wa Mataifa ulikiweka Kiswahili nafasi ya saba ya lugha zinazokua haraka duniani.

Leo tuangalie mifano miwili ya udhoofu na ubovu wa wanasiasa, wanahabari, wasanii na waalimu. Ni kawaida siku hizi kusikia wazungumzaji hadharani wa Kiswahili wakisema : “Waziri fulani ameweza Kusema” au “fulani ameweza kuwaambia wananchi”...Hapa tutoe msisitizo wa neno kuweza. Neno hili ni kitendo. Huelezea maumbile, mwondoko, kazi, shughuli nk. Kiingereza ni “verb”...

Katika Kiswahili kitendo huanzia na neno KU : kuimba, kusoma, kuangalia, kutafuna, kusafiri nk.

Neno kuweza lina matumizi mawili. Mosi kuwa na muda wa kufanya jambo. Mathalan iwapo mtu alikuwa mgonjwa, au alitingwa na kazi hakujibu simu yako, na sasa kaweza kutimiza kitendo alichokuwa akisubiriwa akifanye. Hapo tutasema “Fulani alikuwa mgonjwa sasa anaweza au ameweza kuja kazini.”

Maana ya pili ya kuweza ni kumudu, kufanikiwa, kudiriki kufanya jambo. Hii maana ya pili ndiyo huchezewa sana. Wakati watangazaji wa redio, mablogi au You Tube wanaposema “Waziri ameweza kuwaambia watu wachape kazi...” Wanarudia neno mara mbili. Hakuna haja ya kusema “Waziri ameweza kuwaambia...” maana neno kuwaambia lenyewe ni kitendo kinachojitosheleza.”Waziri amewaambia wananchi wachape kazi...” Inajitosheleza.

Tatizo la pili linalozidi kuharibu kabisa Kiswahili ni lafudhi.

Uchanganyaji wa L na R. Tatizo kubwa sana.

Vyombo vya habari na mitandao jamii, kusema abali badala ya habari au leri...kinyume cha reli.

Karibuni utetezi umedai tatizo sababishwa na lugha za kikabila. lakini mbona Kiswahili ni lugha ya kibantu? kwani zamani hakukuwa na makabila? tofauti ya zamani na sasa ni kuwa hatujali tunavyoitumia lugha. wanahabari huria na baadhi ya wanasiasa na wataalamu tunalipua mambo ili kionekane na kuvutia – umaarufu, fedha za haraka haraka na kutafuta maslahi bila nidhamu. Tabia hii inaonekana pia ughaibuni ambapo kizazi kipya hakijali sana desturi za usafi, kuzungumza kwa heshima hata maadili.

Kiswahili ni fursa kiajira. wenzetu Waingereza waliijenga (na wanaendelea kuiimarisha) lugha yao kupitia vitabu, majarida, sinema, sanaa, fasihi, ukoloni, biashara, ualimu nk. sisi lazima tuuige mfano huo maana leo Kiswahili ni uchumi na uzalendo.

Advertisement