Kiswahili ni fursa lakini kinaendelea kuchafuliwa nasi wenyewe - 2

Sunday January 13 2019Freddy Macha

Freddy Macha 

Jumapili iliyopita tulitoa mifano miwili ya makosa yanayoharibu Kiswahili. Matumizi ya “kuweza” yasivyofuata kanuni za kisarifu na pia kuchanganya herufi L na R. Kuandika au kusema leri badala ya reli, mathalani....

Tulikubaliana kuwa ingawa Rais na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo wamesisitiza Kiswahili kimeorodheshwa kuwa lugha ya kumi (kati ya 6,000 duniani) bado wahusika wa lugha hii tunakibatilisha.

Leo tuangalie vipengele vingine vitatu.

Cha kwanza ni Kiswanglish.

Kati ya waumini wakuu wa mseto huu wa Kiingereza ni Wachagga wenzangu (wa nje na ndani) wanaodai Kiswahili hakijitoshelezi msamiati. Hivyo hujibiidisha “kukopa” kutoka kwenye Kiingereza. Kasumba kuwa Wazungu watukope misamiati. Kiingereza ni lugha. Si Uzungu. Uzungu hauna maana ya maendeleo. Wazungu ni wanadamu kama sisi wenye kila aina ya matatizo. Wenzetu wa lugha nyingine kubwa ( Kispanyola, Kireno, Kifaransa) hawana kabisa tabia hii ya kukopa kwa Kiingereza, Kichina au Kiarabu. Ni sisi tu. Usipokopa Kiingereza unajiona hujazungumza vizuri.

Tatizo pia ni vijana wa kizazi kipya (“Millenials “ kwa Kimombo) sasa hivi wana matatizo makubwa kilugha.

Mwaka jana nililumbana na mmoja wa Mabloga wakubwa nchini akadai lugha ya siku hizi si kama ya zamani. Kosa kubwa sana. Wakati wenzetu wanasonga mbele kuendeleza lugha zao, wakati wageni wanasomea Kiswahili na kukifundisha Mexico, Ujerumani hadi China sisi tunajipiga sime mguuni tukidai hatuna haja ya kufuata masharti. Kwa Mtanzania Kiswanglish kinamchuja uwezo wake wa kuzimanya lugha hizi mbili sawasawa. Ni sawa kwa Mtanzania anayejua Kiingereza na Kiswahili fasaha kutumia. Ila kwa kizazi kipya kisichofundishwa au kujifunza Kiswahili sawasawa ni madhara tosha. Wapo watakaopiga kelele mbona Kenya wanaongea Kiswanglish? Na Kenya ndiyo inaongoza kwa kukitangaza Kiswahili katika muziki (nyimbo maarufu za Kiswahili zinazojulikana duniani zimetungwa na Wakenya).

Lakini wenzetu wanachapa Kiingereza vizuri. Wanasoma vitabu zaidi yetu. Nairobi sasa hivi inaongoza soko la uuzaji vitabu vitamu na vizuri vya Kiswahili. Wakenya ninaoishi nao London ni wachunguzi sana wa Kiswahili na Swahili Hub ni mtandao unaoendelea kukua haraka kuhimiza azma ya lugha hii.

Tatizo la pili ni wageni, mwaka 1993, kampuni maarufu ya sinema za Kimataifa, DisneyWorld, ilitoa mchezo wa makatuni yaliyotunga hadithi Tanzania (Serengeti na kuuita “Lion King”). Walipokosa wimbo wa Kiswahili toka Tanzania wakatumia Jambo Jambo wa Bendi ya Uyoga toka Mombasa. Leo wimbo unaitwa “Hakuna Matata.” Hawa weupe wakaubatiza wimbo huo upya. Ukizungumza na wageni (hata Waafrika) watasema Hakuna MATA-RA. Hiyo MATA-RA imetokana na matamshi ya Kimarekani. Hapo inaonyesha ukimwachia mgeni akutangazie kitu chako anavyokuharibia.

Hapa tumalizie kwa kusisitiza tena -Fursa.

Leo ukitaka kujifunza lugha yoyote nenda You Tube. Vipo tele. Lakini ni vingapi vya Kiswahili? Na ni Watanzania wangapi tunaofundisha? Ndiyo wapo. Lakini wengi wanaofundisha vizuri ni toka Kenya, au Wazungu walioishi (au wanaoishi Tanzania)....na Waswahili wanaozungumza lugha hii kwa ufasaha ni wachache. Hatuioni fursa, tunalalamika njaa.

Tuamke, tusome. Tumekalia bahari, almasi na mali tele!

Advertisement