Kitunguu saumu huzuia fangasi ukeni, kinywani

Wengi tunajua kitunguu saumu ni mojawapo ya viungo vinavyotumika kuongeza harufu nzuri katika chakula na pia huleta hamu ya kula.

Hata hivyo, hatujui kwa undani faida zilizopo katika kitunguu hicho.

Kama ulikuwa hujui, jifunze sasa; kitunguu saumu husaidia kuzuia maambukizi yatokanayo na bakteria, baadhi ya virusi na fangasi hasa katika utumbo, mapafu na sehemu za ukeni.

Mtaalamu wa masuala ya lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC), Elizabeth Lyimo anasema vipo vitunguu saumu vya rangi nyeupe, zambarau na pinki na vyote vina ubora sawa.

Lyimo anasema mbali na faida hizo, kitunguu saumu pia husaidia kuyesha chakula na kuzuia kuharisha.

Anasema kiungo hicho kinazuia maambukizi yatokanayo na fangasi kwenye kinywa kutokana na viambata vinavyopatikana kwenye kitunguu saumu ambavyo ni allicin, vitamini C, Vitamin B6 na manganese.

Unaweza kuandaa kitunguu saumu kwa ajili ya kusaidia kutuliza vidonda vya koo kwa watu wenye maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU).

Mahitaji:

Chukua punje nne za kitunguu saumu, maji kikombe kimoja, na sukari au asali.

Namna ya kuandaa:

Menya na katakata kitunguu, tia kwenye maji yanayochemka, acha kichemke kwa dakika kumi. Epua, funika na acha ipoe, kisha ongeza asali au sukari kwa ajili ya ladha.

Matumizi:

Kunywa kikombe kimoja kutwa mara tatu.

Makala haya yameandikwa na mwandishi wa gazeti hili Hadija Jumanne anayepatikana kwa barua pepe [email protected]