NDANI YA BOKSI: Konde Boy ana wakati mgumu katika himaya ya Mondi, Kiba

Kina nani wamechagua upande kwa hawa masela? Kina Belle 9 na wengineo wapo. Lakini wapo kama hawapo. Wanafunikwa na vivuli na si ubora wa hawa masela wa Tabata na Madale. Angalau fujo za Konde Boy zinatowesha udwanzi huu. Lakini ukweli ni kwamba bado homa ya virusi hivi inaranda mitaani.

Ni kama Messi na Ronaldo vivuli vyao vilifubaza nyota ya Iniesta na wenzake. Walipotakiwa kuwa wachezaji bora wa dunia wakakosa ndicho kilichotokea kwa Kiba. Konde Boy ana wakati mgumu sana kwa mazingira mengine.

Kuna time hawa jamaa wanakata stimu kinoma noma. Na si wao binafsi, bali wale wafuasi wao. Hao ndio tatizo. Ni kama Simba na Yanga kwenye soka hakuna kujali uwezo wala ubora wa kipaji cha mtu. Wanaegemea mahaba na ushabiki tu. Wa Kiba haoni jema zaidi ya baya la Mondi, na wa Mondi haoni heri zaidi ya shari kwa Kiba.

Sharti kuu ni wa Mondi kusimama naye hata kwenye ubwege wake, na wa Kiba kusimama naye hata kwa ulofalofa wake. Wameamua kuwa hivyo kama ambavyo walivyo wale masela wa Msimbazi na Jangwani. Yaani kufa na tai shingoni.

Wakati wa uhai wake Ruge Mutahaba. Iliaminishwa kuwa baadhi ya wanamuziki wanapitia wakati mgumu kwa kukosa maelewano naye. Kwamba waliokosana naye walipitia wakati mgumu kwa maana yeye ndiye aliyekuwa injini ya muziki Bongo. Hakupaswa kupingwa wala kubishiwa na hawa mayoyoo wa muziki. Yawezekana ilikuwa kweli. Lakini tangu atuachie hiki kidunia kisicho na aibu wala hofu ya Mungu kuna unafuu wowote kwa wasanii? Hakuna. Hakuna.

Kuna tatizo zaidi ya kile tulichoaminishwa juu ya Ruge. Gemu lina makando kando mengi kutokana na hofu ya maisha kwa baadhi ya wadau wa muziki. Kuichukia kazi au nafsi ya mtu ni dalili na alama tosha ya hofu ya maisha. Furahia maisha.

Kwa siku za karibuni Mondi na Kiba wamekuwa na kazi za kawaida, lakini kwa kuwa ‘wamejibrandi’ kwa upinzani wao pekee, watu wanaishia kuwashindanisha.

Wakati zamani wazee wetu walibomoa bendi moja ili kwenda kujenga nyingine. Hii leo mashabiki hawataki uwepo wa wanamuziki wengine nje ya Mondi na Kiba. Konde Boy ana wakati mgumu sana kwa mazingira haya.

Darassa, Young Lunya, Young Killer, Country Boy au unataka kusema Dogo Aslay? Huwezi kuwa serious kama hata kina FA waligeuka watazamaji. Gemu kwa miaka kumi hii limeundwa kupitia mbavu za hawa Wamanyema wawili wa Dar. Inakera kiaina kwa wenye ndoto na haya makitu.

Mondi kuna vituo vya redio havipigi ngoma zake. Ruge hayupo. Sitaki kuamini huko aliko bado anatoa mwongozo wa nani nyimbo zao zipigwe au zisipigwe. Kuna tatizo zaidi ya tulichoaminishwa juu ya Ruge. Ben Pol alikosa tuzo ya wimbo bora kwa ngoma ya ‘Moyo Mashine’. Wafuasi wa Simba na Yanga za kwenye muziki waliamua. Ndivyo ilivyo kwa Barnaba na wenzake kukosa jeuri mbele ya hawa jamaa. Tunakosa fursa ya kushuhudia ubora wa Marioo na wenzake.

Zamani msanii aliyeshikilia namba moja muda mrefu kwenye top ten redioni alikuwa na baraka tele za kugonga kopi pale kwenye viambaza vya wadosi Kariakoo. Waliamini kuwa wimbo unaopigwa kila wakati kwenye redio ndo dili. Wakafanya wasanii wawe watumwa na ‘stafu’ wa redio. Kuanzia mtangazaji mpaka mfagizi wa ofisi, hata dereva tu wa kiredio fulani akanyenyekewa.

Kiasi cha pesa anachoingiza mtu, kinaenda sawa na kiasi cha hofu moyoni. Tajiri ana hofu ya kuibiwa, kufilisika pamoja na kuzidiwa uwezo.

Kadiri pesa inavyozidi kufunga ndoa na sanaa ndivyo matatizo yanavyojimegea nafasi kubwa ya utawala wake kwenye utandu wa sanaa ya muziki. Namna wasanii na watu wa kukuperuzi huko youtube ni jukumu zito kama maisha ya wodi ya wazazi. Madogo wanahaha kututia ndimu kutafuta ‘vyuuzi’. Kifupi tuwasamehe.

Ndo maana uhasama wa Mondi na Kiba una maisha marefu. Na hauna dalili ya kuisha kwa sababu unawanufaisha. Wakileta stori za kupatana wanajua itakula kwao. Wanatamani ‘gemu’ la kisirani chao liendelee kudumu kama chama tawala. Wale si mabwege wanajua wanachofanya bifu bila faida waliliacha kwa Dudu na Nice

Tuzo za ndani na nje ya nchi wamejimilikisha wao. Watu huanza kuwaongelea wao kuliko tuzo husika. Hata baadhi ya wanamuziki hugeuka kama mashabiki. Ndivyo ilivyo na haikwepeki. Pamoja na spidi ya Mondi kuwa kubwa zaidi ya mwenzake lakini analazimika kumsubiri kwenye maeneo kadhaa ili kuchangamsha gemu. Ndivyo ilivyo kwa Thea na Johari ni waigizaji maarufu lakini hawana karama ya kuishi midomoni mwa watu kama Uwoya au Wema. Na ndio sababu ya kuzidiana hata idadi ya wafuasi mitandaoni. Ustaa ni kitu kingine na kufuatiliwa kitu kingine tofauti. Ndio tofauti ya Dai, Kiba na wenzao.

Na hili jambo halijaja bahati mbaya, ni chakula kilichopikwa kikaiva. Lulu Diva ni mtoto flani, kapambana na kupata jina. Pamoja na yote hana nguvu ya ushawishi kuliko Gigy Money. Wakati Lulu Diva atakuvutia. Gigy utatamani kusikia au kuona analofanya. Iko hivyo. Walianza pamoja.

‘Gemu’ la sasa ni ‘kujibrandi’ tu. Ikibidi kujitwisha hata gunia la misumari ili ‘kutrendi’ tu. Dogo Janja kando ya Irene Uwoya lilikuwa muvi tamu na la kutishia tawala zingine. Tatizo hawakuendana. Matokeo yake watu waliwachukulia kimasihara na utani zaidi. Uwoya ni tani nyingi mno.

Sijajua bado Jux na Vanessa nani amem-push mwenzake. Ili bila shaka Jux ana jawabu mujarabu la hili jambo. Kuna muziki na myuziki. Umaarufu ni moja. Kuongelewa na kufuatiliwa sana ni jambo lingine zito. Monalisa ni maarufu lakini akiongozana na Lulu na kupita sehemu najua unajua nani ataangaliwa na kuzungumziwa sana.

Kurasa za insta zinawatia uchizi kwani huko ndiko makazi rasmi ya timu zao zisizo na kina Zahera wala Haji Manara wao. Uhasama wao umekuwa mwiba kwa wanamuziki wengine. Pamoja na ubora wa ngoma zao, hawana ushawishi wala mvuto wa kuongelewa na watu.

Ni mwendo wa mapichapicha tu. Leo Konde Boy yule pale. Ukianza kuhesabu kuanzia Mondi au Kiba. Atakayefuata kutoka wao ni Konde Boy. Utake usitake Harmo kishapindua meza na kukaa nyuma ya miamba hii miwili Mondi na Kiba. Ni suala la muda tu, mapicha yakiendelea usishangae Konde Boy akawa juu ya hawa watu. Muziki na mashabiki wa Bongo hawana mfumo wanaweza kumfanya mtu akawa namba moja kwa sababu tu ya utajiri na siyo uwezo na kipaji.

Unakumbuka wakati wa Mr Nice? Mkwanja ulimfanya awe juu ya wote lakini tukisimama katika ukweli hakuwa na uwezo mkubwa mbele ya Bushoke, Banana, TID, Chilla na wenzao. Lakini mkwanja ulimfanya avimbe. Afrika Mashariki na kati changanya na visiwa vyote vya jirani akawa yeye tu. Jina lake lilikuwa juu.

Ila hawa jamaa wawili wamebadili gemu na sasa mitandaoni wanazungumziwa wao hata wakifanya kitu cha ajabu.

Kibaya zaidi wasanii wengine wanapojaribu kuiga tabia za uendeshaji muziki wako wanaopotea kabisa. Kila mwanamuziki sasa anategemea kiki na mapichapicha ili atoke kisanaa badala ya uwezo wa kazi. Kuna wasanii wanatoa ngoma mpya lakini hazifiki mbali.

Harmonize hana muziki wa ajabu kumzidi Barnaba. Hana uwezo kumzidi Aslay na wengine wengi, anachofanya ni ‘kujibrandi’ kwa matukio. Uzushi mpaka ‘maeksi’.

Mashabiki wa mtandaoni wakikupenda unaweza kuambiwa Mobetto na Beyonce wote walikuwa wanamuziki duniani. Sasa wewe kaza mishipa ya shingo kama unafunga tairi ya trekta kwa kudhani muziki wa sasa unahitaji hasira kama enzi za kina Mika Mwamba.