Kudharau unyago kumepunguza wanawake kujiheshimu

Muktasari:

  • Mila na tamaduni hazikumzuia mwanamke kuongoza, ila zilimuandaa kuwa kiongozi bora kwenye jamii na familia yake

Imeelezwa kuwa masomo (manyakanga) kubadili ufundaji kutoka wa asili kuja wa kisasa kumechangia kuharibu misingi ya ndoa hususani kwa wanawake.

Miaka ya nyuma walikuwa wakimfunda mwanamke kwa kumuandaa kuhudumia familia yake na kuwa mfano bora kwa jamii, lakini mabadiliko ya maisha na kukua kwa utandawazi kumeondoa thamani ya suala hilo.

Mfundaji maarufu Anti Zulekha Mikidadi anasema kuwa tabia ya wazazi kuuchukua unyago au msondo ni kwa ajili ya watu fulani tena Waswahili umechangia kuifubaza jamii.

“Najua kipindi cha kufundwa wasichana wengi wanakuwa masomoni, lakini hilo halina maana kuwa wasipate hiyo ada muhimu kwa mustakabali wao.

“Kuna watu wamepotosha kuhusu mafunzo ya wasichana wakisema hili na lile lakini ukweli unabaki kwa anayepata mafundo hayo, msichana aliyepata miiko anatofautiana sana na yule asiyepata,” anasema Zulekha.

Zulekha anafafanua kuwa wapo masomo wanaoharibu maana nzima ya unyago kwa kuweka usasa na kutoka kwenye maadili, “Hao wamechangia kuudharaulisha unyago, wamekuwa na tamaa ya kutaka vitu vingi, kutunzwa na kuropoka hata mbele ya wasiojua maana,” anasema.

Hata hivyo Bi Khadija Mfaume anasema kuwa kwake unyago bado una nguvu ndiyo maana licha ya watoto wake kusoma nje ya nchi wakirudi huwapa miiko kwa kuwaitia wakubwa na kuja kusema nao.

“Zulekha ananijua, watoto wangu wa kike wote watatu wamesoma udaktari tena India na ni watu wa dini sana huwezi kuona nywele zao, lakini wanaporudi likizo na umri wa kuwapa mafundo ukiwa umefika huwa namualika.

“Nimefanya hivyo kila mmoja kwa wakati wake, bila sherehe wala mbwembwe kwa sababu lengo ni kuhakikisha wanaishi kwa kufuata mila na tamaduni,” anasema Bi Khadija.

Anasema kutokana na kuwapo maneno ya hapa na pale kuusema vibaya unyago hata binti zake walikuwa hawataki wakichanganya mambo hayo na dini, lakini aliwaelewesha wakaelewa.

“Nilishirikiana na wifi zangu kuwaelewesha kwa sababu hata baba yao hakubariki sana hadi alipopewa somo na dada zake, unyago hauna usomi kwa sababu tunaishi sote kwenye jamii vyeo,” anasema.

Anafafanua kuwa iwapo binti zake watajaaliwa kupata waume wa kuwaoa atawaita wazee waje kuwafunda kuwa wanandoa bora.

Anasema kwamba mwanamke kuolewa bila kuandaliwa kuna madhara makubwa ikiwamo kutomthamini mumewe wala yeye mwenyewe.

“Kuna wanawake hata haki zao za ndoa hawazijui kwa sababu hawajafundwa, sasa ukimwambia mtu hadi haki zinafundishwa kwenye unyago atakubishia wao wanawaza huko kunafundishwa mambo ya laana tu.”

Kwa upande wa mfundaji mahiri Chuma Suleiman maarufu Bi Hindu anasema kuwa maana ya unyago haijawahi kubadilika na haitawahi.

Anasema unaobadilika ni mtizamo na ndiyo sababu hasa baadhi ya wasichana na wanawake ukiwaona uhitaji kuambiwa kuwa wanahitaji kufundwa ili wajitambue.

“Hapa nilipo nafunda mwali na unajua nikianza kazi hii sikatizi nitafute siku nyingine tuzungumze vizuri kwa sababu haya mambo yanahitaji kituo, nasisitiza unyago una maana kwa mabinti wasioolewa na kwa wanawari wanaojiandaa kuingia kwenye ndoa,” anasema kwa ufupi Bi Hindu.

Kwa upande wa Chausiku Salum maarufu Bi Chau anasema kuwa wazazi wakatae wakubali unyago ni zana bora ya binti kuishi katika maadili.

Anasema bila kuuliza wasichana anaokutana nao kazini, majumbani na mahali pengine hutambua huyu aliambiwa maana na huyu hakuambiwa kutokana na namna wanavyoendesha maisha yao.

“Kinachochangia kupoteza maana ya jambo hili ni hili neno uzamani...imekuwa kawaida kila kitu uzamani, leo hii waite wanaume 10 uwaeleze maana ya unyago nakuapia wao wenyewe wataomba wake zao wapitie walau siku moja.

“Hii inatokana na vibweka wanavyokutana navyo majumbani mwao, mwanamke haoni tena umuhimu wa mumewe kula chakula chake, mwanamke aliyekamilika hawezi kudanganya chakula amepika yeye ilhali amepika msaidizi kwa sababu mumewe atakuwa anakifahamu leo ni wanaume wangapi wanajua ladha ya chakula cha wake zao,” anasema na kuhoji Bi Chau.

Anasema kuna wanaolinganisha unyago na mbio za kutafuta maisha, ilihali ni vitu viwili tofauti.

“Hakuna nyakanga au somo atakayemfunda binti awe mvivu, ndiyo maana wanawari wa zamani walikuwa wanapimwa kwa kazi zao, aliyefundwa atakuwa analima, anatwanga na anajua kuhifadhi chakula kwa sababu alifundishwa, hivyo kazi au elimu havimzuii mtu kujitambua.

“Msingi wa unyago si wanavyofikiria watu wengine, msingi wake ni kumuandaa binti au mke mtarajiwa kuwa na tabia zinazolingana na maisha ya kawaida ya binadamu, ” anasema.

Anasema kwamba aliwahi kumwambia binti aliyeolewa siku si nyingi ampe singo, yule binti akamueleza hajui singo ni nini.

“Mke wa mtu hajui singo ni nini kwa maana hiyo mumewe anakwenda kusingwa kwenye masaluni ilhali angefanya mwenyewe hiyo kazi ndiyo maana ndoa zinakosa utulivu, ”anasema.

“Kuna siku nilikutana na mwanaume kwenye gari amevaa pete ya ndoa sikuwa na uhakika kama ameoa au laa, lakini kama ameoa nilimhurumia kwa sababu alikuwa na kucha kama mwewe kuashiria hakuna anayejua kuwa hata jukumu la kumkata kucha mume au kukatana kucha ni lao,” anasema Bi Chau mfundaji maarufu.

Anasema ameona kwenye mitandao watu wanasema kuhusu uchungu wa sikio, hayo ndiyo madhara ya kutothamini unyago ndiyo maana watu wanakuwa na taka sikioni kama nta ya asali.

Anawaasa wazazi kutowakabidhi mabinti wafundwe na mitandao ya kijamii.

Anafafanua kuwa kudharau mafundo kwa watoto kumesababisha kila wanachofanya wakianike kwenye mitandao kwa sababu hawana mwiko, hawajui cha kuanika wala kuficha, vyote wanaona sawa.

“Wapo wanawake wameolewa hawaoni shida kueleza wakiwa faragha na waume zao nini kinatokea, hayo yote wasingeyafanya iwapo wangepata miiko.

“Achaneni na mawazo ya ngoma, kutunzana, sijui dhana ya mafiga matatu, hizi ni anasa si lengo hasa la unyago na sidhani kama kuna nyakanga hufundisha hayo kama yupo anakosea sana,” anasema Bi Chau.

Naye (jina kapuni kwa heshima ya mkewe) anasema kuwa alimtafutia mkewe somo wa kumfunda miaka mitatu baada ya ndoa yao.

“Nilisafiri mkoa fulani, nikakuta mabinti wana nidhamu nilipouliza nikaambiwa wamefundwa, nikauliza kufundwa ndiyo nini nikaelezwa sikujiuliza niliporudi niliwatafuta wafundaji kwa ajili ya mke wangu.

“Hivi tunavyozungumza angalau amebadilika kwa sababu mambo yalikuwa hayaeleweki...sitaki kusema ilikuwaje lakini nataka ujue ilikuwa shaghala baghala, ”anasema.