Kuelekea Uchaguzi Mkuu Malawi, wagombea wazee wachuana na vijana

Wednesday March 13 2019

 

By Deus Kibamba

Jumapili nilianza kuandika vioja vya Uchaguzi Mkuu Malawi. Nilieleza kuwa yapo mengi ambayo yanaonekana kuwa vichekesho na Nikahitimisha kuwa Watanzania ni lazima tuwe na hamasa ya kujua yatakayojiri nchini humo kwa sababu mbili: Kwanza, kuna idadi kubwa ya watu wetu nchini humo wakifanya kazi, biashara au kuishi na kuwa hata vifaa vingi vya matayarisho ya kampeni vinatokea Kariakoo, Dar es Salaam.

Kwa hali nilivyoiona nilipotembelea Malawi mwezi uliopita, nguvu ya Rais Mutharika iko zaidi katika maeneo matatu.

Kwanza, yeye ndiye Rais na kwa hiyo ana sauti, kauli na maamuzi juu ya rasilimali fedha na mali za nchi hiyo. Ukweli ni kwamba hata bajeti ya kuendesha uchaguzi ambayo Tume ya Uchaguzi ya Malawi (MEC) inahitaji kukamilisha zoezi hili kwa ufanisi inamtegemea sana Rais Mutharika.

Kwa tuliyoyaona Congo DRC na Zambia wakati fulani na hivi Karibuni, Rais anaweza kusema hatuna pesa za kukamilisha zoezi la uchaguzi na kwa hivyo mchakato huo usimame kusubiri wakati nchi itakapopata pesa.

Kwamba Rais Mutharirka anaendelea kuagiza rasilimali ziende MEC kukamilisha uchaguzi ni jambo la kumpa sifa. Pili, Rais Mutharika ana mamlaka na umiliki mkubwa wa vyombo vya habari vya ndani ya Malawi kuanzia radio, TV na magazeti machache yaliyopo.

Hilo nalo linapaswa kuwa jambo la kumpongeza Profesa Mutharika kwa kuamua kuviacha vyombo vifanye kazi yake bila kuvivuruga, kuvitishia wala kuvishambulia.

Mara kwa mara, magazeti na mitandao ya kijamii wamemchora na kumdhihaki Rais Mutharika na chama chake pasipo kutishiwa, kuonywa wala kufungiwa.

Hata waziri wake wa habari alipojitokeza katika siku za karibuni kuwakumbusha wanahabari kuhusu sheria inayokataza dhihaka kwa Rais, vyombo vingi viliandika na kumchora kuwa yeye mwenyewe ameleta dhihaka kwa wanahabari kiasi ambacho kimekuwa kama kioja kingine cha aina yake kati ya waziri na wanahabari.

Kwa hili, Malawi wanapaswa kuwa mfano mwingine wa kuigwa kuhusu uvumilivu wa kisiasa na kifikra. Kutofautiana kimawazo haipaswi kuwa uadui na huo ni msingi mkuu wa siasa za ushindani.

Jingine ni kwamba Rais Mutharika mwenyewe amepoteza mvuto kwa wananchi na amewaletea wapiga kura mgombea mwenza ambaye ni mgeni na mpya katika siasa za Malawi hadi wapigakura wanauliza Everton Chimuliranji ndo nini? Kinachompa Rais nafasi ni hulka ya Wamalawi kupenda wanachokijua kuliko wasichowahi kuishi nacho.

Kwa mfano, katika mitaa ya Lilongwe au Blantyre, yatosha tu kujua lugha ya Kichewa au Chichewa ili wananchi wakuone ni Mmalawi mwenzao. Wale tunaozungumza Kiswahili au Kiingereza mitaani tunahisiwa ni wageni, vibaka au nyonyadamu jambo linaloweza kukukosesha mengi.

Kama huwezi kutamka salamu ya Mlibwino au Mlibwanji, ningeshauri usiende Malawi wakati wa uchaguzi kama huu ujao mwezi Mei. Kwa asili, Wamalawi ni watu wakarimu, wapole na wastaarabu lakini wenye hofu na wasiwasi sana kwa mtu wasiyemfahamu.

Waingereza katika uchambuzi wao hupenda kuwaita Wamalawi kuwa ni ‘Conservative’ (wasiotaka mabadiliko). Hii inaweza kuwa sababu mojawapo viongozi wanaochaguliwa wemekuwa ni kutoka koo zilezile zinazofahamika tangu uhuru kama Hastings Kamuzu Banda; Joyce Banda; Bakili Muluzi; Atupele Muluzi; Bingu wa Mutharika; Arthur Peter Mutharika; yaani walewale.

Je, mwiko huu utavunjwa katika uchaguzi huu mkuu wa 2019? Yataka subira.

Kioja kingine katika uchaguzi wa Malawi ni kuhusu umri wa wagombea. Nilishuhudia nikiwa Blantyre wananchi wakijinasibu kuwa uchaguzi wa mwaka huu una wagombea wazee na vijana wakichuana katika kinyang’anyiro cha urais.

Nilipowahoji vijana ni nani nilitajiwa majina ya Makamu wa Rais, Saulos Chilima na Waziri wa Afya Atupele Muluzi. Hawa wana umri wa chini ya miaka 50 lakini hawawezi kwa namna yoyote kukidhi kuitwa vijana.

Kioja hiki kilinikumbusha wagombea wa urais katika uchaguzi Mkuu wa Tanzania mwaka 2005 ambapo Rais mstaafu Jakaya Kikwete alitajwa na vijana kuwa chaguo lao labda kwa kujua au kutojua kuwa hakuwa kijana kwa kigezo chochote kile cha kisheria, kisera au kiumri.

Jambo jingine nililojifunza Malawi na maeneo mengine yanayotuzunguka ni kwamba ujana au uzee barani Afrika ni suala la sura kung’ara au kukomaa zaidi kuliko umri.

Wagombea wengi wanaochukuliwa kama vijana si vijana kwa namna yoyote. Hata kikatiba wala kisheria, nchi nyingi za Afrika haziruhusu kijana kugombea urais kwa vile umri wa kikatiba ili uruhusiwe hata kupewa fomu ya urais ni kuanzia miaka 40. Ni kioja kuwa hakuna kampeni yoyote ya vijana wa Malawi au hata Tanzania kutaka umri wa mtu kugombea urais ushushwe hadi miaka 30 au 35. Hivyo ndivyo baadhi ya vioja kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Malawi 2019. Inshaallah nitakuwa Lilongwe wiki ya uchaguzi Mkuu unaofanyika Mei 21.

Deus M Kibamba ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo Cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB). Anapatikana kwa simu: +255 788 758581; email: [email protected]

Advertisement