Kujiajiri ni fursa ya kuwa tajiri kuliko kuajiriwa

Friday December 21 2018

 

By Mpoki Mwaiswaswa, Mwananchi

Moja ya dhana potofu miongoni mwa vijana wengi ni kutafuta elimu kwa lengo la kuajiriwa.

Pengine hiyo inatokana na mfumo dhaifu wa elimu katika nchi zetu, haimjengei mwanafunzi mazingira ya kusoma ili kuelimika bali kusoma ili kujibu maswali ya mitihani kwa ufasaha!

Vijana wengi kuanzia ngazi ya elimu ya msingi, sekondari na hata vyuo vikuu, wamekuwa wakihaha kutafuta ajira serikalini mara baada ya kuhitimu masomo yao, badala ya kuitumia elimu waliyoipata kujiajiri wenyewe.

Ikumbukwe kuwa mfumo wetu wa elimu nchini unazalisha vijana wengi kila mwaka wanaoingia katika soko la ajira. Wengi ni watu wanaotafuta kuajiriwa, huku wachache wanaochagua kujitosa katika shughuli za ujasiriamali wakikumbana na vikwazo vingi ikiwamo wazazi wasioamini katika ujasiriamali, ukosefu wa mitaji, mrundikano wa kodi na masoko yenye ushindani yasiyotoa fursa sawa kwa biashara zinazoanza kukua.

INATOKA UK 21

Shughuli kuu za kiuchumi ambazo ni kilimo, uvuvi, ufugaji, uchimbaji wa madini na biashara ndogondogo zimekuwa zikifanyika kwa kutumia zana na elimu duni na mazingira yasiyo rafiki. Kwa hiyo kama kijana unapaswa kuyafahamu fursa tano muhimu katika kujiajiri.

Uhuru wa Kifedha

Huwezi kufikia mafanikio makubwa kiuchumi na kimaisha ikiwa bado utakuwa umeajiriwa na serikali, kampuni, taasisi au mtu. Watu wote waliofanikiwa katika biashara au shughuli zao binafsi ni watu walioamua kujiajiri na kuziishi ndoto zao.

Mo Dewji alikataa kuajiriwa alipohitimu masomo yake Marekani, na akaamua kurudi nchini kujiajiri na kutumia fursa zilizopo. Kwasasa ndiyo tajiri namba moja nchini.

Uhuru wa kutumia muda vizuri

Huwezi kutumia muda wako pamoja na fursa zinazojitokeza vizuri ukiwa umeajiriwa kwa kuwa vigezo, masharti na mkataba wa kazi vitakubana kufanya mambo yako binafsi. Hivyo ili uweze kutumia muda wako vizuri na unufaike na fursa mbalimbali zinazojitokeza huna budi kujiajiri mwenyewe ili uwe huru kufanya shughuli au biashara zako mwenyewe.

Watu wote unaowaona wamefanikiwa ni watu waliotumia vema muda na fursa zinazowazunguka.

Urahisi wa kufanikisha ndoto/malengo yako

Si rahisi kuweza kufikia ndoto yako na kutimiza malengo yako kama utakuwa umeajiriwa na hasa kama unafanya kazi isiyoendana na ndoto yako.

Kujiajiri ni mbinu rahisi na sahihi ya kukuwezesha kufikia ndoto yako na kufanikiwa malengo yako maishani.

Kama unataka kufanikisha ndoto uliyonayo huna budi kufanya kila namna kuhakikisha unafanikiwa kutimiza malengo yako ikiwa ni pamoja na kujiajiri.

Watu wote waliofanikiwa katika sekta mbalimbali ni watu walioamua kuvifanyia kazi vitu wanavyovipenda.

Kuelewa elimu ya fedha na kodi

Ukiwa mfanyakazi wa kuajiriwa maisha yako yote utakatwa kodi kwenye mshahara wako upende au usipende, lakini pia makato mengine yatakuhusu.

Hivyo, tambua kuwa kujiajiri ni njia na mbinu rahisi sana ya kuweza kuielewa elimu ya fedha na kodi vinavyofanya kazi. Wafanyabiashara wana fursa ya msamaha wa kodi kisheria ambayo watu wengi hawajui na huamua kuajiriwa wakiamini wao wako sehemu salama na huogopa kujiajiri kwa kisingizio cha mlundikano wa kodi.

Kwahiyo kujiajiri kuna fursa kubwa sana ya kuielewa pesa na kodi ili uweze kuendelea na kufanikiwa katika shuguli/biashara zako.

Kukutoa katika utumwa

Kuajiriwa kunakufanya ufanye kazi ili upate pesa, badala ya kufanya pesa ikufanyie kazi. Huo ndiyo tunaouita utumwa wa kazi, kwa kuwa wakati wote utafikiria kazi yako huku ukisubiri mshahara mwisho wa mwezi. Kujiajiri kutakusaidia kukutoa utumwani na kukufikisha kwenye uhuru wa kifedha, kina Mo Dewji, Bakhresa na wengine wote waliofanikiwa wana uhuru wa kifedha na wanaifanya pesa wanayoipata kutengeneza au kufanya kazi zaidi ili pesa iendelee kujizalisha zaidi.

Kwa ushauri na mafunzo zaidi kuhusu kujiajiri, ujasiriamali, biashara, kilimo biashara na fursa za kiuchumi tutembelee Facebook, Twitter, Instagram na WhatsApp kwa jina Elimika Ung’are’ 0655056758

Advertisement