KALAMU HURU: Kumbe kuna wabunge hawataki wafanyakazi waongezwe mishahara

Japo Bunge halionyeshwi moja kwa moja lakini hicho kidogo tunachokiona kinatosha kuzua mjadala mpana.

Zamani tulikuwa tunashuhudia mijadala mikali kutoka kwa wabunge wa chama tawala na wale wa kambi ya upinzani, lakini tangu matangazo ya moja kwa moja yalipozimwa, tumeishia kubahatisha vipande vya matukio bungeni.

Moja ya kipande kilichovuma hivi karibuni ni hoja iliyotolewa na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Ruth Mollel kuhusu nyongeza ya mishahara akisema watumishi hawajawahi kuongezwa mishahara tangu awamu ya tano iingie madarakani.

Mollel, katibu mkuu wa zamani wa Utumishi, alisema mbali na nyongeza inayowekwa na mwajiri (Serikali), kuna ile ya lazima kisheria (statutory annual increment), nayo haijatolewa.

Mollel alitoa hoja hiyo wakati Bunge lilipokaa kama Kamati kupitisha bajeti ya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma kwa mwaka 2019/2020.

Baada ya hoja hiyo, Naibu Spika Dk Tulia Ackson aliwahoji wabunge kwa sauti kuona kama kuna wengi wanaoafiki hoja hiyo ijadiliwe, lakini kwa maoni yake wasioafiki walishinda na hoja ikaishia hapo.

Kwa muda mrefu, pamoja na kuwa kura za sauti zipo kikanuni, kumekuwa na mjadala juu yake kuwa kiti cha spika kinaweza kuona/kusikia walioshinda ni kundi hili na mtu mwingine akaona kinyume chake.

Pamoja na kwamba hoja ya wafanyakazi kuongezwa mishahara imepigwa chini, lakini si kweli kwamba wafanyakazi hawajaongezwa mishahara kwa zaidi ya miaka mitatu?

Je, kuna sababu ya msingi inayoweza kutolewa kuhalalisha wafanyakazi wasiongezwe mishahara hata ile ya kisheria?

Hoja kama hiyo iliwahi pia kutolewa na aliyekuwa Mbunge wa Kakonko mwaka 2017, Kasuku Bilago (marehemu) ambaye alihoji sababu ya Serikali kushindwa kutoa nyongeza ya kisheria ya mishahara. Hoja hii imeendelea kujirudia na huenda ikaendelea kusumbua.

Tumemsikia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera uratibu wa Bunge, Jenister Mhagama akisema maslahi ya wafanyakazi ni pamoja na barabara nzuri, huduma bora za afya, maji na umeme. Baada ya mipango hii ya uchumi, hivyo Serikali itatekeleza nyongeza ya mshahara.

Kwamba, kwa kuwa wafanyakazi kama wananchi wengine wanapata mahitaji muhimu kama maji, elimu, chakula na mengineyo na mishahara yao kwa wakati, basi ndiyo inatosha?

Je, hiyo miradi hiyo itarejesha mikopo na kuzaa faida baada ya miaka mingapi hadi nyongeza ya mishahara ipatikane?

Pengine tungetarajia wabunge bila kujali tofauti zao, wangelisemea hili bungeni ili Serikali itafute ufumbuzi, pamoja na kuwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo ni muhimu.