Kuna fursa kilimo cha parachichi

Muktasari:

  • Nchini Tanzania, zao la parachichi hulimwa zaidi katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe, Katavi, Rukwa, Ruvuma, Kilimanjaro na Morogoro.Wadudu wanaoshambulia zaoNzi wa matunda, funza wa matunda, kobe wa majani na minyoo fundo wa miziziMagonjwa yanayoshambulia zao: kutu ya majani, kuoza kitako cha tunda, kuvu, minyoo fundo na minyauko (fusari, bakteria na baka.Soko la parachichi: Hivi sasa bei ya tunda moja la parachichi sokoni inaanzia Sh 500 hadi 1,500Faida

Mahitaji ya parachichi hapa nchini yamekuwa yakiongezeka kwa kasi tofauti na miaka ya nyuma.

Hii imetokana na kuwepo kwa kampuni za zinazosafirisha nje ya nchi matunda haya pamoja na kuwapo kwa viwanda vya kutengeneza mafuta kutokana na parachichi.

Kuna viwanda vya wawekezaji, ambavyo hununua na kupeleka parachichi nje ya nchi na vya

wajasiriamali wanaosindika mafuta ya parachichi pamoja na vikundi vidogo vya wakulima.

Aina za parachichi zimegawanyika katika makundi mawili ambayo ni kienyeji na kisasa.

Parachichi za kienyeji ni nzuri, ingawa za kisasa ni nzuri zaidi kwa ajili ya biashara.

Aina za parachichi za kisasa

Parachichi za kisasa ni pamoja na Hass, Fuerte, Ndabal, Booth, Etinger na Waisal. Aina hizi za parachichi hupendwa sokoni kwa kuwa zina kiasi kikubwa cha mafuta au siagi.

Hass na Fuerte: Aina hizi hukomaa mapema. Huchukua miezi sita kukomaa mara baada ya kutoa maua. Parachichi hizi zina mafuta mengi, zina ukubwa wa gramu 250 hadi 750 na soko lake ni kubwa.

Ndabal: Aina hii ya parachichi ina matunda makubwa ukubwa wa gramu 800 hadi kilogramu moja. Huchelewa kukomaa kwani huchukua miezi minane mara baada ya kuchanua.

Waisal na Etinger: Aina hizi za parachichi huvumilia ukame na huchukua miezi minne hadi mitano kukomaa.

Uoteshaji wa mbegu za parachichi

Mbegu za parachichi za kisasa mara nyingi hushindwa kumudu magonjwa wakati wa uotaji. Wakati mwingine hazioti, hivyo inabidi kupandikiza kwenye pandikizi za kienyeji.

1.Hatua ya kwanza, unahitajika kukusanya mbegu za kienyeji kutoka kwenye miti mama yaani parachichi zilizokomaa na kuiva.

2.Andaa udongo wa kupandia. Udongo huu ni vyema ukakusanywa kutoka msituni na kuuchanganya na mboji au samadi iliyoiva, majivu, mchanga na maranda au makapi ya mpunga.

Katika mchanganyiko huo, uwiano wake uwe debe moja la mchanga, udongo debe mbili, mboji debe mbili, maranda debe moja na majivu moja ya sita ya mchanganyiko wote.

Changanya kwa pamoja huku ukinyunyizia maji kidogokidogo, kisha jaza kwenye viriba vyenye upana wa inchi nne na urefu wa inchi sita.

3.Otesha mbegu moja moja katika kila kiriba na hakikisha mbegu unayootesha imekauka vizuri na umeondoa maganda. Mbegu hii huchukua wiki moja hadi tatu kuota, na mwezi mmoja au zaidi mpaka kuwa na uwezo wa kubebesha (ili shina la mche liweze kuwa imara). Hakikisha mche umefikia unene wa kalamu ya risasi na urefu wa futi moja.

Ubebeshaji

•Chukua vikonyo kwenye miti iliyoanza kuzaa na vikonyo hivyo viwe na ubora. Hakikisha vikonyo vimepata vijicho vinavyoanza kuchipua.

•Hakikisha unatoa majani ili kupunguza upotevu wa maji.

•Anza kubebesha miche na zingatia unene wa mche na vikonyo viwe na uwiano sawa.

Kuna njia kuu mbili za ubebeshaji wa miti ya parachichi ambazo ni ubebeshaji wa juu ya mche na ubebeshaji wa pembeni ya mche. Njia zote mbili ni nzuri na hazina tofauti wakati wa kubebesha.

Mashimo ya kupandia

Andaa mashimo kwa ajili ya kupandia mapema sana kabla ya mvua za

mwanzo kuanza. Umbali wa mche na mche uwe ni mita sita na mita sita mstari hadi mstari.

Hii ni kwa sababu mche hupanuka, hivyo huhitaji nafasi ya kutosha. Upana wa mstari na mstari uwe ni futi mbili na kina cha shimo kiwe na urefu wa futi mbili (sentimita 60 kwa sentimita 60).

Katika shimo, changanya udongo na mbolea ya samadi kiasi cha debe moja hadi mbili. Anza kupanda miche shambani mapema mara tu baada ya mvua kuanza kunyesha.

Matunzo

Hakikisha unapalilia mara kwa mara, ili kuondoa magugu yasiweze kuua miche.

Kama ni wakati wa kiangazi, hakikisha unamwagilia maji ya kutosha ili udongo uweze kuwa na unyevu wa kutosha wakati wote.

Upuliziaji wa dawa ni muhimu ili kukinga magonjwa ya ukungu na wadudu kama vile inzi weupe, kimamba wekundu na wengineo.

Mara nyingi miparachichi haishambuliwi na wadudu wala magonjwa hivyo upuliziaji unahitajika kufanyika pale panapokuwa na ulazima au kwa kiwango kidogo.

Kila mwaka miti mikubwa na midogo itakapotoa maua, miche nayo itatoa hivyo hakikisha unayaondoa maua hayo. Mara nyingi mavuno ya miparachichi ya kisasa huanza baada ya miaka mitatu tangu kuandaa mche.

Soko

Soko la parachichi kwa sasa limekuwa sana, kutokana na upelekaji wa matunda haya nje ya nchi pamoja na usindikaji wa bidhaa zinazotokana na parachichi. Hivi sasa bei ya tunda moja la parachichi sokoni inaanzia Sh 500 hadi 1,500.

Unaweza kuwasiliana na mtaalamu wa kilimo kwa namba: 0625 369 147

Makala kwa hisani ya mtandao wa mkulimambunifu. www.mkulimambunifu.org