Kuuchekelea ufisadi ni kuidhihaki kodi yako mwananchi

Sunday April 14 2019

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali,

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Profesa Mussa Assad akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, alipokuwa akitoa ripoti za ukaguzi kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2018. Picha ya Maktaba. 

By Rashid Abdallah

Siri iliyo wazi! Mataifa mengi ya Afrika baada ya ukoloni kumaliza, yameendeshwa na viongozi wazawa katika mifumo mibovu ya kiutawala, kadhalika kiuchumi.

Hao wanaong’ang’ania madaraka hawataki kuondoka hadi raia waingie barabarani. Ni mfano hai ya mifumo mibovu ya kiutawala kwa demokrasia ya kupokelezana madaraka.

Afrika kubaki ndio bara masikini zaidi duniani. Ni mfano mzuri wa mifumo mibovu katika uchumi wa mataifa yetu. Yaani hamkani hali si shwari!

Mataifa ya Afrika yana matatizo yanayo shabihiana. Hata ukiiangalia ramani ya ufisadi duniani kutoka kwa mashirika mbalimbali. Daima Afrika haibaki salama katika tatizo hilo sugu linalokwamisha maendeleo yake.

Na siku hizi Afrika haiumizwi na Wazungu tena. Kwa asilimia kubwa inaumizwa na Waafrika wenyewe. Kama panya wanaolimeng’enya jahazi lao wakati wa safari.

Hivi karibuni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Mussa Assad ametoa ripoti yake mbele ya waandishi wa habari makao makuu ya nchini, Dodoma.

Ni ripoti inayotamanisha sana, kwa sababu hali bado si nzuri katika taifa hili. Kwa wazalendo, inatia hofu na kuogopesha. Ila hatupaswi kukata tamaa.

Rais John Magufuli alionekana kuingia na kasi ya kupambana na aina zote za ufisadi, ikiwemo wafanyakazi hewa, upotevu na matumizi mabaya ya pesa za umma, upigaji dili na mambo mengine mengi.

Matarajio yetu hali ingekuwa nafuu, kama ni ufisadi basi ungepungua kwa kasi ya ajabu. Ila ripoti ya CAG inaonyesha bado kuna safari ndefu ya kimapambano hadi taifa litoharike na hayo yote. Kama kuna kupungua kwa ufisadi basi ni kwa mwendo wa kobe.

Na tatizo linazidi kuwa kubwa unapogundua, kumbe baadhi ya Watanzania wana shida ya kiuelewa kidogo kuhusu tafsiri pana ya wafanyakazi hewa, matumizi mabaya ya pesa, upigaji dili, mishahara hewa na mfano wa hayo.

Wapo wanaodhani; kwa mfano kukiwa na malipo hewa katika Jeshi la Polisi, maana yake pesa ya Jeshi la Polisi imetumika vibaya. Wakati tafsiri sahihi ni kwamba pesa ya walipa kodi, yaani Watanzania ndio imetumika vibaya (imeliwa).

Nilichokiona katika mitandao ya kijamii baada ya ripoti hii kutoka, ikiwa ni miongoni mwa maoni ya Watanzania, ndicho kiliniacha kinywa wazi. Wengine wanachekelea, au wanatoa maoni yanayoashiria hilo ni tatizo linaumiza Serikali au taasisi zinazohusishwa na huo ufisadi.

Ripoti ya CAG haipaswi kuwa kicheko kwetu. Hizi pesa ambazo zinapotea katika hizo taasisi za umma, zinatoka katika kodi zetu. Kuuchekelea ufisadi kwa sababu umefanyika katika taasisi unayoihesabu ni wapinzani wako kisiasa au kiutendaji. Ni sawa na kuidhihaki kodi yako mwenyewe.

Ukisikia CAG kabaini CCM haijawasilisha NSSF makato ya Sh3.74 bilioni ya wanachama wake au Chadema ilinunua gari jipya aina ya Nisan Patrol kwa Sh147.5 milioni, lakini lilisajiliwa kwa jina la mwanachama badala ya Bodi ya Wadhamini.

Hivi vyote ni vyama vya siasa vinavyopokea ruzuku kutoka serikalini. Ruzuku zinazowasaidia kuendesha mambo yao, ikiwemo hiyo kununua Nisan na mambo mengine. Ruzuku hazitoki mbinguni ila zinatoka katika migongo ya Watanzania.

Myororo wa pesa katika nchi hauanzi kwa Serikali. Unaanza na wewe mlipa kodi, ndio kisha iende serikalini, halafu itumike katika mambo yanayohitajika. Ukielewa hivyo, unapata kung’amua kumbe pesa yako ndiyo inayoharibiwa, inayopigwa dili na kutumika visivyo.

Nitakupa mfano huu mwingine. Ripoti ya CAG pia ilisema Tume ya Uchaguzi Tanzania (NEC) ilinunua mashine za BVR 8,000 lakini mashine 5,000 kati ya hizo zilikuwa haziendani na mfumo uliotakiwa hivyo kuisababisha Serikali hasara ya mamilioni ya shilingi.

Pesa zinazotolewa na Serikali kusimamia uchaguzi, hazikaguliwi kutoka mfuko wa Rais au mawaziri wake. Bali ni kodi za wananchi ndio zimeathirika. Hivyo ndivyo tunapaswa kuwa waelewa wa hili tatizo.

Ufisadi humuumiza zaidi raia katika namna yoyote ile. Ikiwa pesa zitaliwa na wachache au zitashindwa kufanya lililokusudiwa. Mwananchi ndio muhanga.

Inapokuja kesi ya kufichuliwa madudu kama haya, Watanzania tunapaswa kuuweka mbali ushabiki wa vyama vyetu vya kisiasa. Serikali ni mpangaji na msimamizi tu ila pesa hasa zinatoka kwetu.

Tunapaswa kuwa na uchungu nazo. Sio kutupiana vijembe au kuchekelea katika mitandao kwa misingi ya vyama. Hilo halitotusaidia hata kidogo.

Naamini utawala huu chini ya Rais Magufuli, umedhamiria kidhati kupambana na ufisadi. Ni wajibu wetu kumuunga mkono katika lile zuri analokusudia kulifanya. Yasiyo mazuri binafsi nitakuwa wa kwanza kumkosoa ama kukaa naye mbali.

Hata kama ufisadi umekuwa na kumea chini ya utawala wa CCM, hilo halitofuta ukweli kwamba wanaoumia sio wafuasi wa CCM pekee, ni sote.

Na yeyote anayeamua kupambana na ufisadi, ni wajibu kumuunga mkono bila kujali msimamo wake wa kisiasa. Maanake ni kuokoa pesa zetu, sio pesa za chama fulani.

Ushabiki wetu wa mitandaoni uishie kwa Simba - Yanga, Diamond - Alikiba ama Ronaldo - Mesi. Huku kwengine tubaki kitu kimoja. Mungu ibariki Tanzania.

Advertisement