Kwa CCM hii, yajayo hayatawafurahisha

Muktasari:

  • Si kwenye vyumba vya habari, viwanja vya michezo na vijiwe vyote muhimu kama Hananasifu, Leaders Club, Lumumba wala Kata ya 14 Temeke. Sioni vikundi vya watu waliozoea kutajataja majina ya wanachama wanaotaka nafasi katika uchaguzi ujao.

Ikiwa bado miaka miwili na miezi michache kufanyika tena Uchaguzi Mkuu, sioni yale makeke ya awamu ya pili, tatu na nne ya vikundi uchwara ndani ya CCM vilivyokuwa vinaundwa na wanaowania madaraka.

Si kwenye vyumba vya habari, viwanja vya michezo na vijiwe vyote muhimu kama Hananasifu, Leaders Club, Lumumba wala Kata ya 14 Temeke. Sioni vikundi vya watu waliozoea kutajataja majina ya wanachama wanaotaka nafasi katika uchaguzi ujao.

Awamu tatu zilizopita kabla hii ya Ngosha Mwanawane, ilikuwa uchaguzi ukiisha tu safu mpya ya uchaguzi ujao ndani ya CCM inaanza kuundwa. Uchaguzi unaisha hapohapo yanaanza kutajwa majina ya wagombea wa uchaguzi ujao.

Leo ni miaka mitatu kimyaa. Hata tetesi tu hatusikii kuwa 2020 Ilala ataendelea Mussa Zungu au Jerry Silaa? Hakuna mipango, kampeni za wazi wala kificho. Ndivyo ilivyokuwa awamu ya kwanza chini ya Mwalimu Nyerere. CCM kuna utulivu ambao haukuzoeleka kwa miaka 30 iliyopita.

Unapokuwa maeneo ya kujidai kwa mfano ukitoa Sh10,000 baa na kuagiza bia moja, unaonekana ‘Don flan’ hivi, lakini ukitoa hiyo noti kwenye daladala unaonekana msumbufu. Hii inaitwa muktadha.

Ukivaa gauni refu la kitenge kanisani na kusuka twende kilioni kichwani, unaonekana una maadili ila ukivaa gauni kama hilo klabu na kichwani umesuka mabutu unaonekana mshamba. Hii inaitwa utambuzi.

Ukigombea uongozi kwa nguvu ya pesa unaonekana mzalendo uliyeweka kando utajiri wako ili uwatumikie watu, ukigombea kwa maneno matupu bila umatemate unaonekana unataka ukatajirikie madarakani. Hii inaitwa ubongo tifutifu.

Kuna makada wengi sana mitandaoni, ambao hujiona wameendelea sana kiakili, kifikra, wataalamu wa kudadisi, kuhoji, kuponda na kufafanua matamko ya watawala au mawaziri wao. Hawa tunawaambia yajayo yatawachefua.

CCM ya Dk John Magufuli inakuja na utaratibu mpya kwa wagombea kupitishwa na Kamati Kuu kabla ya uchaguzi wa kura za maoni. Ole wenu mlioweka makazi ya kudumu mitandaoni na kuipinga pinga tu mipango ya chama na serikali.

Siwafichi hata kama mnajua wacha niwafahamishe wake, mahawara, au wafuasi wenu wanaovutiwa na maneno kerefu, mnayounda kwa vidole kupitia mfumo wa ubongo katika kupingapinga tu.

Yajayo yatawachefua

Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally, amezungumza na gazeti moja la kila wiki, na kueleza kuwa, ndani ya CCM wameboresha mfumo wa kutafuta wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani. Ukiishi kwa kukariri uongozi ndani ya CCM ya sasa utausikia runingani na mitandaoni.

Kwa sasa wanachama watakaojitokeza kuomba kuteuliwa kuwania nafasi hizo, orodha yao itawasilishwa kwanza Kamati Kuu ya CCM, huko watachujwa na kubaki wachache bora zaidi kwenda kupigiwa kura za maoni

Hii itawasaidia katika dhana ya umoja ndani ya chama na utii kwa wanachama, kwani kwa muda mrefu kuna tatizo kwa baadhi ya makada kuonyesha utovu wa nidhamu. Hii iliwafanya makada hao wanufaike binafsi na upinzani kama yaliyotokea 2015.

Kufanikiwa kwa chama siyo mpaka uwepo wa demokrasia kubwa ndani yake. Hata kuwe na demokrasia kuliko ya mbinguni ambayo Mungu karuhusu uhuru wa kumfuata yeye au shetani. Kama makada hawana utii ndani ya chama hakuna maana ya mafanikio.

Upingaji sana wa waziwazi ndani ya chama, kunamjenga zaidi mpingaji ambaye ni mwanachama huku akidhoofisha zaidi chama chenyewe. Kwa wale wa magharibi wa pua ndefu siyo tatizo, lakini kwa Bara la Afrika utiifu ndani ya chama ni bora zaidi kuliko ukubwa demokrasia.

Kwa miaka mingi sana kwenye hili Chadema wamefanikiwa sana. Kwa matukio mengi ndani ya chama chao wanaonekana wako mbali sana katika utiifu kuliko CCM ya kabla ya Magufuli. Ilifika wakati mwenye pesa na mtandao mkubwa ndani ya chama akawa na nguvu kuliko chama.

Hili iliwatesa sana CCM 2015 wakati wa kuchuja na kutangaza rasmi wagombea pale Dodoma. waziri mkuu za zamani, Edward Lowassa alikuwa na nguvu sana, nguvu ambayo CCM ya Jakaya Kikwete ilimuacha aitengeneze taratibu. Akafanikiwa. Akawasumbua. Na ndio chanzo cha mipango na maamuzi haya.

Dk Emmanuel Nchimbi, Adam Kimbisa na Sophia Simba wakajiona wako juu ya chama. Mbele ya Kikwete wakadiriki kupinga maamuzi ya chama hadharani kisa Lowassa kachinjiwa baharini. Hiki kilikuwa kiwango cha juu zaidi cha kukosa utiifu.

Sasa Katibu wa CCM, Dk Bashiru amewaonya makada wanaotumia mitandao kama sehemu za vikao vya chama. Na inadaiwa hata Mkuu wa Kitengo Cha Uenezi, Humphrey Polepole kapigwa marufuku kuposti mitandaoni tantalila zake. Kuna kitu kinaepushwa na kujenga mfumo bora.

Kwa jicho la kawaidani ngumu kugundua faida yake. Lakini hii itasaidia kubana viongozi wanaodhani ni maarufu zaidi kuliko chama. Katika hili Chadema walifanikiwa sana. Zitto Kabwe sasa yuko ‘bize’ na pambio za ACT Wazalendo baada ya kuoneshwa njia ya kutokea pale Chadema.

Mabadiliko yanayofanywa na CCM ya msingi. Yataondoa upinzani ndani yake. Upinzani uliotengeneza timu na taasisi ndani ya taasisi. Lowassa alikuwa Taasisi ndani ya Taasisi. Ndivyo ilivyokuwa kwa Bernard Membe, walikuwa na wanachama wao ndani ya wanachama wa CCM.

Miaka kumi yote mawaziri wako mbio na harakati za kupata nafasi ya kugombea urais badala ya kuwatumikia watu? Membe aliwaza urais zaidi kuliko wizara yake ya Mambo ya Nje na jimboni Mtama. Lowassa aliwaza urais zaidi ya uwaziri mkuu na Jimbo la Monduli.

Enzi za Mkapa

Pia, wakati wa Benjamin Mkapa kila waziri aliamini anastahili kuwa mrithi wake. Wakati wa Kikwete ndo balaa, kila mwanachama alijiona anafaa kuwa mrithi wake. Ulikuwa upuuzi uliopelekea mawaziri na makada akili iwaze kurithi uongozi wa juu kuliko utendaji kazi.

Huu uamuzi wa wagombea kupitishwa kwanza kwenye Kamati Kuu kabla ya kupigiwa kura, utaongeza nguvu ya maamuzi ndani ya chama na kurudisha utiifu kwa wanachama kama wakati wa Mwalimu miaka ya nyuma. CCM ilifikia sehemu ilikuwa kama mchezo wa watoto wa gombania goli.

Changamoto zake

Kila jambo unapoliboresha lina changamoto zake. Uamuzi huu pia lazima utawagharimu maana kuna watu kwenye kata na majimboni hujiona au wanachama huwatazama kama wao ni zaidi ya chama.

Yawezekana kukawa na mgogoro mkubwa mara baada ya kutekeleza hili ndani ya CCM. Kwani chama ni watu na watu wanatofautiana kimtazamo hasa wanapokuwa sehemu moja zaidi ya mmoja. Hamuwezi kuwa sawa wote lakini faida ni kubwa kwenye hili kuliko hasara.

Wakati wa Mkapa kutokana na kuacha mambo yaende kama yalivyo mwisho wa siku wanachama waliachiana makovu ambayo hayajafutika mpaka leo. Na wakati wa Kikwete chama kilipasuka na kumuachia Magufuli jukumu hili la kuweka mambo sawa.

Kutokana na kuacha watu wajijenge tu ndani ya chama, CCM ya Mkapa iliwafanya Watanzania waamini kuwa akitoka Mkapa, atafuata Kikwete kisha Lowassa. Akili gani hii? Tuliaminishwa hivyo na wapambe wao kila sehemu.

Walijijenga kwenye michezo. Burudani. Vyombo vya habari. Kwenye taasisi za serikali za binafsi mpaka zile za kidini. Kote huko walikuwa na wapambe waliowatangaza kwa mema tu. Hali hii ndiyo ilipelekea kila anayepumua aamini anaweza kusimama kama raia namba moja wa taifa hili.

Sasa ndani ya CCM mambo yamebadilika. Sakata la kontena 20 za vifaa vya ofisi za walimu Dar es Salaam, endeleeni kuongelea kama ni ujenzi wa chama. Kama inaua chama basi mtakaotangaza nia 2020 kumbukeni majina yenu yatapita Kamati Kuu kabla ya kupelekwa kwa wanachama.

Nape Nnauye na wabunge wote wa kusini na umoja wao wa kwenye sakata la pesa za korosho. Kama watataka tena kuongoza majimbo yao ili waendelee na kaumoja hako, waelewe tu kuwa majina yao lazima yatapita kwanza Kamati Kuu.

Makada na makomredi mtambuka wa Twitter na Instagram. Ambao huamini wako nje ya serikali kimakosa, ila wao ndio wenye akili kubwa kwa kukosoakosoa na kupinga maamuzi mengi kwa maandiko yao. Waelewe tu kuwa yajayo yatawachefua.

Naamini utaratibu huu utasaidia CCM kupata viongozi wasomi. Kwa maana nyingine 2020 wale wote waliohamia CCM kutoka upinzani wajiandae mapema kisaikolojia. Kwa mfumo huu mpya watapata taabu sana.

Yajayo yatawachefua.