NDANI YA BOKSI: Kwa alikofikia Jokate, Bongo Movie shtukeni

Saturday October 5 2019

 

By Dk Levy

Yes! Napenda madem wazuri. Dunia hii unataka nipende nini. Soka? Ndiyo napenda soka, naachaje kutopenda ufundi wa Pep Gardiola na maajabu ya pasi za KDB? Na siwezi kuacha kuhuzunika na mbinu za Unai Emery. Wenger alifanya watu tupende soka la pasi na ufundi mwingi. ‘Soka la huba’ badala ya makombe.

Vurugu za utatu mtakatifu wa Salah, Mane na Firmino pale Anfield. Lazima ugeuze shingo lako na kugeuka shahidi wa maajabu ya mbinu za Klopp na jitihada za wale madogo watatu. Wanahadaa na kushambulia kwa kasi mpaka upuuzi wa tekinolojia ya video inapoteza mwelekeo. Haiwezi kuona ‘ofu saidi’.

Movie? Ndiyo nahusudu sana filamu. Naachaje kulipenda tabasamu la Angeline Jolie anapoigiza mahaba. Kicheko cha Vivica Fox anapoigiza kama kahaba? Na siwezi kuacha kuumizwa na matokeo ya filamu za Bongo Movie. Ray anaposhindwa kuendelea pale alipoachwa na mwanae Steven? Siyo Nyerere namaanisha Kanumba.

Kinachoendelea Bongo Fleva. Madogo wanadondosha mijengo na ndinga hatari. Wanaingiza pesa nyingi kwenye akaunti, kuliko madem wanaowaingiza kwenye mageto yao. Naanzaje kushangaa maigizo ya video ya Wema Sepetu akizawadiwa gari na shosti yake Aunty Ezekiel?

Ushawahi kumshuhudia Tundu Lissu akisisitiza jambo bungeni? Lazima utahusudu siasa. Ndivyo ilivyo unapomuangalia Polepole akikufafanulia ubora wa siasa za utawala huu. Na huwezi kuacha kuumizwa na ujinga wa wajinga wanaopinga kila kitu. Na ubwege wa mapimbi wanaosifia kila kitu. Lazima ujue Usimba na Uyanga upo mpaka kwenye maisha halisi.

Kupuuza siasa ni kuruhusu vichaa wakuamulie maisha yako ya kila siku. Kujifanya hufuatilii siasa ni kuacha kesho ya watoto wako itengenezwe na wasiojitambua, wajinga na wendawazimu. Mimi nafuatilia siasa kwa sababu ya kesho ya taifa langu. Ukiona mtu anapuuza siasa na wanasiasa ujue hana akili timamu. ‘Mwehu’.

Advertisement

Kuna wakati Bongo Movie walituaminisha kuwa, mrembo anafaa kuwa staa wa filamu. Kanumba na wenzake wakawa wanakusanya ‘Mamiss’ waliopitwa na wakati na kuwaingiza kwenye movie. Wakiona dem mzuri yupoyupo tu mtaani akidanga, wakambeba na kumpa ‘sini’.

Mashabiki wa Bongo nao wakawa wanawafuata wao. Si wanawapenda mastaa wao? Wakaaminishwa filamu nzuri ni yenye warembo. Mrembo kutoka Uyui Tabora. Kilema Moshi. Kihesa Iringa. Kihonda Moro. Chamwino Dodoma. Usagara Tanga na Mwakibete Mbeya. Akaamini urembo ni daraja la kuwa Nora au ‘Lulu’ Elizabeth Michael.

Zikaanza kuuzwa video za komonio, kipaimara na ‘besidei’ ambazo tuliambiwa kuwa ni filamu, kisa tu kwenye ‘kava’ kuna sura ya mrembo wa haja. Ukizama kuangalia ndani unagundua ni matakataka. Utadanganya watu mara moja lakini siyo siku zote. Mwisho filamu zetu zikaanza kupuuzwa. Hili ndilo tatizo halisi.

Mwelekeo wa Bongo Movie ukaanza kutoweka njiani. Hawakujali tena ubora na kipaji. Wakatazama kope bandia, mapoda, mawigi na vigodoro. Wakawatenga kina Thea. Wakamuweka kando Johari na kumtosa Monalisa, wakamsusa Monalisa na kumpuuza Bi Mwenda na kuwakumbatia mamiss. Kumbe urembo ni ndugu na uwezo wa akili. Walipoona wamepata sifa za kibwege katika filamu wakajiaminisha kuwa urembo wao unaweza kuwaweka daraja la kwenda Bungeni Dodoma na kutupangia sheria na mambo ya taifa letu. Wakavamia siasa kama wanavamia madanga ya kwenye bendi za dansi. Hili pia ni ajabu la dunia.

Jokate akili nyingi. ‘Ofu kozi’ malezi bora pia yalichangia. Hakuacha urembo na uwezo wake wa ubunifu na uigizaji, kiwe kigezo cha kuwa mtu fulani kwenye taifa. Mngoni yule wa Peramiho sijui Mbinga kama si Madaba akazingatia kitu kinaitwa shule kwanza kabla ya huu upuuzi mwingine. Ndo maana hii leo yuko pale alipo. Umeelewa?

Urembo hauwezi kukufanya uwe mtu fulani kwenye jamii yako. Elimu pekee inaweza kukupa kila kitu duniani. Jokate ni sehemu ya Bongo Movie na Umiss pamoja na mitindo nchini. Lakini si urembo, mitindo wala uigizaji uliomfanya awe mtawala wa Kisarawe leo. Elimu chanzo kikuu cha kuwa alipo.

Elimu ndio ndoa pekee isiyo na talaka. Mtaji pekee usio na hasara, nguzo pekee isiyoweza kupata ufa kwa tetemeko lolote. Elimu ndio urithi bora zaidi duniani. Leo hii Jokate yuko vizuri kwa kipato na heshima.

Mastaa wetu wa filamu hawana ya darasani wala mtaani. Ndo maana hawajui hata chanzo cha kutoweka kwa soko la kazi zao.

2006. Nyayo za Jakaya katika sakafu za Ikulu ya Magogoni. Hajauzoea urais, maarufu kuliko yeyote kwa wakati huo.

Wasichana wawili warembo kweli kweli pale Diamond Jubilee, walikuwa wakipigana vikumbo kila mmoja anataka kuwa Miss Tanzania kumrithi Nancy Sumari. Wakati huo Miss Tanzania lilikuwa tukio kubwa sana.

Huku kuna Wema Sepetu kule kuna Jokate Mwegelo. Leo hii Jokate kamuacha Wema peke yake. Wema anajitazama kwenye kioo akiwa na hukumu inayofanya asipate nafasi aliyonayo mwenzake.

Wema ule wakati wa kubaki peke yako umewadia. Muda haujawahi kumuacha mtu salama na si rafiki.

Filamu na urembo kwa kina Wema na wenzake wakati ule. Ilifanya warembo waamini kuwa urembo unaweza kukupa kila kitu duniani. Leo urembo wa Jokate na DAS wa Ilala, Charangwa, unafanya watu waamini urembo bila elimu huwezi kuwa mtu fulani kwenye jamii. Urembo si kigezo cha U-DC wa Jojo wala U-DAS wa Charangwa pale Ilala.

Kuelewa au kutoelewa ni tatizo sana. Tatizo ni kubwa kuliko watu wanavyofikiria. Kwa hatua tuliofikia ya usugu wa tatizo ni vigumu kupata tiba mbadala. Yaani Tanzania na Watanzania wenyewe kiakili wanahitaji kuzaliwa upya. Ama kubatizwa upya, tena ubatizo wa Kisabato wa kuzamishwa kwenye maji mengi.

Nafuu pekee tuliyonayo ni kuwekeza katika kizazi kijacho, kwa watoto wetu. Wafundishwe tulipotoka. Wafundishwe tulipokosea. Waelezwe kwa uwazi wajue kwa nini sisi hatuwezi kuchukua hatua kuifanya Tanzania, ama sisi kama raia kuwa wakazi wa nchi ya neema ili wafanye mapinduzi ya fikra na maamuzi. Sisi tumeshindwa.

Hatuwezi kuubadili mfumo unaotengeneza umasikini kila siku. Tumeshindwa kwa maana ya kushindwa. Unapoona msichana anajua Kiingereza vizuri kama Wema Sepetu, halafu anashindwa kuelewa wapi alipokwama. Hilo ni tatizo kama taifa si mtu binafsi. Wema ni taasisi ana marafiki, mashabiki, ndugu na wafuasi.

Wema ana wafuasi zaidi ya milioni tano insta. Idadi kubwa kuliko wasomaji wa magazeti yote nchi hii. Lakini wote hao hawajui la kufanya kumsaidiWema.

Ukitazama ulichonacho, utahisi una zaidi. Ukitazama unachokosa hutokuwa na zaidi. Maisha ni ukitendacho. Huwezi kubadili maisha bila kubadili fikra. Changamoto ni maisha, na kukabiliana nazo ndio maana halisi ya kuishi. Maisha hayapimwi kwa idadi ya pumzi tuivutayo, hupimwa kwa idadi ya hatua za pumzi zetu.

Advertisement