Kwa baadhi ya wastaafu nchi haina tatizo, kwa wengine yapo kibao

Muktasari:

  • Mazungumzo yote ya wastaafu unaweza kuyaweka kwenye makundi mawili; upande mmoja hii nchi inakwenda vizuri na hakuna matatizo kabisa. Upande wa pili, matatizo yapo, tena makubwa. Hata hivyo, wastaafu wote katika hoja zao za makundi mawili, walikiri kwamba ipo kazi nzuri inatekelezwa na Rais Magufuli.

Nimepata kuona na kusikiliza ushauri wa viongozi wastaafu wa Tanzania kwa Rais John Magufuli walipohudhuria mkutano ulioitishwa Ikulu, Julai 3, mwaka huu. Viongozi hao ni waliohudumia mihimili yote mitatu ya dola; Serikali, Bunge na Mahakama. Vilevile Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Mazungumzo yote ya wastaafu unaweza kuyaweka kwenye makundi mawili; upande mmoja hii nchi inakwenda vizuri na hakuna matatizo kabisa. Upande wa pili, matatizo yapo, tena makubwa. Hata hivyo, wastaafu wote katika hoja zao za makundi mawili, walikiri kwamba ipo kazi nzuri inatekelezwa na Rais Magufuli.

Februari mwaka huu, watafiti wa Taasisi ya Brookings, Marekani, walitoa ripoti waliyoiita “The challenges of problem solving in a divided country” kwa tafsiri ya ‘Changamoto za utatuzi wa matatizo kwenye nchi yenye mgawanyiko’. Kwamba kuna ugumu wa kupata ufumbuzi wa matatizo ikiwa kuna mgawanyiko.

Mathalan, wastaafu wengine walimsifia tu Rais Magufuli, wengine pamoja na kusifia, waliona ulazima wa kuyasema matatizo wanayoyajua. Wastaafu wote hao wanaishi Tanzania, kila mmoja ana macho, masikio na hisia zilizo hai. Kwa maana hiyo, mshauriwa anaweza kujiuliza mbona wengine wamempongeza tu na wachache wamemweleza matatizo?

Je, waliomweleza kuhusu matatizo ni kweli yapo au wanamwonea wivu? Swali hilo hufuatiwa na hili; kwa nini na waliopongeza tu hawakuona hayo matatizo yaliyosemwa na wenzao? Ni hapo unapata mantiki ya ripoti ya Brookings, kwamba mgawanyiko wa mapokeo na uwasilishaji ni changamoto ya utatuzi wa matatizo.

Hata wewe binafsi ukiita watu 10 wakushauri, saba wakikusifia tu na kukwambia huna tatizo lolote, kisha watatu wakikosoa mwenendo wako kuwa siyo safi, unaweza kujiuliza wale saba wote mbona hawakuona yaliyosemwa na watatu? Ni hapo hisia kwamba watatu wanakuonea wivu huweza kujitokeza.

Ni tofauti na washauri wote 10 au wengi zaidi wakwambie makosa yako, inakuwa rahisi kujiuliza; kwa nini wote waone tatizo hilohilo? Ni kweli kwamba asiyetaka ushauri haishiwi hila na anaweza kuukana ukweli anaoambiwa na kila mtu. Hata hivyo, ndani ya nafsi yake atakuwa akikaa peke yake nafsi itamsuta.

Hivyo, mtazamo wa jumla ni kwamba Rais Magufuli alifanya jambo jema kuwaita viongozi wastaafu ili wafanye mashauriano. Alifanya vizuri zaidi kutobagua, aliwaalika mpaka wale ambao wapo tofauti kiitikadi, mfano mawaziri wakuu wa zamani, Fredrick Sumaye na Edward Lowassa ambao wamehamia Chadema.

Hata hivyo, kitendo cha baadhi ya wastaafu kuzungumza kana kwamba hakuna matatizo na wengine wakayasema waziwazi si jambo lenye heri kwa nchi. Vilevile kitendo cha wengine kuzungumza kwa uangalifu mno mpaka kushindwa kueleweka vizuri, hakikuwa kizuri, maana Rais Magufuli mwenyewe ndiye aliwaita. Na bila shaka alitaka kusikiliza ushauri wao na siyo mapambio.

Ukizisikiliza hoja za Sumaye na Lowassa pamoja na uwasilishaji wao, unagundua kwamba walikuwa na kitu walichotaka kufikisha, lakini wakatekwa na uangalifu, kwa hiyo wakajielekeza zaidi kuchagua aina ya maneno ya kutamka na matokeo yake kushindwa kugusa kitovu cha maudhui waliyolenga.

Hapo ndipo pa kujiuliza, Lowassa na Sumaye walishindwa nini kugusa kitovu cha maudhui? Kumekuwa na maneno mengi kuwa Rais Magufuli ama hashauriki au watu wanamwigopa. Sasa anawaita mwenyewe mumshauri, badala ya kwenda moja kwa moja kwenye kiini, wakazunguka mpaka kupoteza msingi wa hoja yenyewe.

Ushauri wa dhahabu

Kwa kifupi Sumaye hakueleweka kabisa ingawa baadaye amejitetea kuwa ujumbe wake ulikatwa. Kwa kilichosikika ni kama alikuwa anajaribu kujenga upatanishi, kwamba Rais Magufuli na viongozi wengine wa CCM, wachukulie uamuzi wake kuhamia Chadema ni faida ya CCM na nchi kwa jumla. Je, hicho ndicho Watanzania na Chadema walipenda amshauri Rais katika nafasi ya dhahabu?

Jaji Mkuu mstaafu, Augustino Ramadhan alitoa ushauri wenye hadhi ya kuandikwa kwa wino wa dhahabu. Alisema amani ni tunda la haki. Kwamba utoaji haki ukizingatiwa, amani itajitengeneza yenyewe na kwamba haki isipokuwepo, amani ya nchi itatetereka.

Ramadhan aligusia msemo wa Waingereza kwamba unatakiwa kuwa makini na matumizi ya fedha ndogo, fedha nyingi zitajichunga zenyewe. Kwamba lazima kuchunga mambo madogo kisha yale makubwa yatajichunga yenyewe.

Hoja ya Jaji Ramadhan ni kuwa Serikali lazima itende haki ngazi zote. Kusiwe na kupuuzwa kwa mambo madogo yenye kuhusu haki za watu. Kama haki itakuwa ikitendeka kwa usahihi, amani yenyewe itajitengeneza. Jaji Ramadhan alimtaka Rais Magufuli yeye mwenyewe atende haki kisha wasaidizi wake wafuate.

Ukisikiliza hoja ya Lowassa, unaona kwamba alikusudia kusema alichosema Jaji Ramadhan. Lowassa alitaka amani iliyopo iendelezwe. Alikusudia kusema isichezewe. Hakuwa na mfano wa kueleza kuhusu sababu ya yeye kuonya kuhusu mazingatio ya amani. Tofauti ya Lowassa na Jaji Ramadhan ni uwasilishaji tu.

Ushauri mwingine wa dhahabu ulitolewa Jaji Mkuu mstaafu, Barnabas Samatta. Yeye pamoja na kuunga mkono hoja ya Jaji Ramadhan, alitaka mambo mazuri yenye kutekelezwa na Rais Magufuli, yawe ndani ya utawala wa sheria. Akaeleza pia kuwa isiwe tu sheria, bali sheria nzuri.

Samatta alitaka miswada inayopelekwa bungeni kutazamwa mara mbili kuhusu utekelezaji kama haipoki haki za watu. Alisema utawala wa sheria lazima uzingatie haki. Alieleza kwamba kuna matamko ya viongozi akiyasikia hubaki akijiuliza mwenyewe, sheria ziko wapi? Kwa jumla pamoja na utawala wa sheria, Samatta alionya kuhusu sheria mbovu.

Unapoichukua kauli ya Samatta kuhusu uwepo wa sheria mbovu, unaoanisha na Sheria na kanuni za maudhui ya mitandao na ile ya Huduma za vyombo vya habari, ambazo zinalalamikiwa sana na wadau kwamba zinaminya uhuru wa kutoa maoni, vilevile zinapoka uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari.

Unapozungumzia utawala wa sheria, msingi mkuu ni Katiba. Shughuli za kisiasa, mikutano ya hadhara na mikusanyiko mingine ya kijamii, imeruhusiwa ndani ya Katiba. Hata hivyo, mwaka 2016, Rais Magufuli alipiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano ya kisiasa mpaka wakati wa kampeni.

Kitu kilichopewa ruhusa ya kikatiba na sheria, maana yake hiyo ni haki. Kwa maana hiyo vyama vya siasa vinanyimwa haki yao. Jaji Ramadhan amesema haki hutunza amani. Samatta ametaka utawala wa sheria uambatane na haki. Kumbe sasa, ulikuwa ushauri mzuri unaozingatia umuhimu wa kuvipa haki vya vya siasa.

Hata hivyo, Spika wa Bunge mstaafu, Pius Msekwa alitetea uamuzi wa Rais Magufuli kuzuia mikutano ya kisiasa. Alisema ni sawa, kwani siasa zinapaswa kuhamia bungeni baada ya uchaguzi. Msekwa anasema hivyo akijua kabisa Katiba inatoa haki kwa vyama vya siasa kufanya mikutano ya hadhara. Hapo Rais Magufuli ashike lipi, la Samatta na Ramadhan au Msekwa?

Upo mshauri mzuri sana uliotolewa na Spika wa Bunge mstaafu na mwanamke pekee kuongoza moja ya mihimili mitatu ya dola, Anne Makinda. Yeye alitaka kuwe na amri za Serikali na si kila kiongozi akisimama anasema Rais kasema. alieleza hiyo haifai, Rais ni mtu mmoja.

Aligusia mgogoro wa kiwanda cha chai Lushoto kwamba unawaumiza sana wananchi. Makinda alimtaka Rais Magufuli kuingilia kati na kumaliza tatizo. Alisema Serikali haiwezi kuchukua shughuli za uendeshaji wa kiwanda hicho kupitia bajeti zake kwa sababu ya ukubwa wa gharama.

Alichokizungumza Makinda kinaonesha kuwa kuna mambo hayapo sawa, hivyo aliona aweke usahihi na kushauri hatua za kuchukuliwa. Rais wa Tatu, Benjamin Mkapa yeye aliamua kutetea chama chake (CCM), kwamba isemwe Serikali ya CCM siyo ya mtu fulani, kwani Rais Magufuli amepewa Urais na CCM.

Ushauri kwa wastaafu

Mstaafu hupaswa kuwa kioo cha waliopo kazini. Baada ya kutimiza wajibu wake kwa miaka, anakwenda nje ya ulingo. Ni kipindi ambacho anauona ubora wake na anayaona makosa aliyoyafanya.

Mtu anapokuwa kazini katika ofisi ambayo inampa madaraka makubwa, hutokea kujisahau. Zile nguvu za mamlaka aghalabu zinaweza kumchanganya na kumsababishia kutenda makosa akidhani ndiyo anafanya sahihi.

Wanaweza kuwapo wakosoaji wema lakini kwa nafasi yake akaona lengo lao ni kumharibia au shabaha yao ni kumbeza kwa kila anachokifanya. Ni kwa sababu hiyo hutokea kiongozi madarakani anakuwa na masikio madogo lakini mdomo unakuwa mkubwa. Kwamba anaongea zaidi kuliko kusikiliza.

Mamlaka humpa mtu jazba, maana ndani yake huwa kuna sauti ya ndani kwa ndani inayomnong’oneza mhusika kwa kumwambia yeye ndiye yeye. Ni sauti hiyo humfanya hata asiwazingatie wanaomkosoa.

Ni sauti hiyo “wewe ndiyo wewe” humfanya aliye ofisini kuona wanaomkosoa ni wenye wivu na madaraka yake, na wenye kutenda kinyume na matakwa yake ni wakaidi, hivyo huamua kuwaonyesha namna nguvu zake zilivyo.

Baada ya kutenda kisha kugeuka mtazamaji, ni hapo inakuwa rahisi kuwaambia wengine hasa waliopo dimbani kwa wakati husika kwamba jambo fulani ni kosa, kwani wewe kipindi chako ulilifanya na ulikosea.

Ni kwa sababu hiyo kwamba nchi nyingi, viongozi wastaafu au taasisi za umma na binafsi, wale watumishi waliotumika kwa muda mrefu na kustaafu, hutumika kama hazina ya ushauri pale mambo yanapokwenda ndivyo sivyo.

Mstaafu hata awe alitenda makosa kiasi gani kipindi akiwa dimbani, baada ya kuwa nje ya ulingo hutambua makosa yake, hivyo huweza kuwa mshauri mzuri. Hivyo, wastaafu wakati wote wakipata nafasi ya kumshauri Rais, wamshauri masuala ya kweli yenye kuisaidia nchi. Siyo kubabaisha maneno au kumpamba tu.