USHAURI WA DAKTARI: Kwa nini baadhi ya wanaume wana matiti yaliyojaa?

Sunday April 7 2019Dk Shita Samwel

Dk Shita Samwel 

Kwa kawaida mwanaume ameumbwa kuwa na matiti madogo, ugonjwa wa wanaume kuwa na matiti makubwa kama wanawake huleta usumbufu hasa wa kisaikolojia kwa mwanaume husika.

Kuna hatua au makundi matatu katika ukuaji wa kawaida kwa mwanaume na huweza kuwa na matiti makubwa na baadaye huisha na kurudi kuwa ya kawaida.

Kundi la kwanza ni mtoto mchanga wa kiume, asilimia 60 hadi 70 huwa na matiti makubwa hii ni kwa sababu ya homoni ya ‘estrogen’ ya mama kwa mtoto, ambapo baada ya wiki mbili au tatu homoni hii huisha katika damu ya mtoto, hivyo matiti kunywea.

Kundi la pili ni katika kipindi cha kubalehe kwa mtoto wa kiume, asilimia 30 hadi 60 huota au hukua matiti kuliko kawaida, lakini hurudi katika hali ya kawaida kati ya umri wa miaka 16 hadi 18.

Kundi la tatu ni asilimia 50 ya wanaume wenye umri wa miaka 50 na kuendelea ambao huanza kuota matiti na kuwa makubwa.

Matatizo yanayosabisha kukua kwa matiti kwa mwanaume ni pamoja na shida katika vinasaba (genetic) vinavyohusiana na matiti, saratani mfano ya korodani, saratani ya mapafu au ya Ini au ya tezi dume.

Magonjwa mengine yanayosababisha kukua kwa matiti kwa mwanaume ni pamoja na kufeli kwa figo, magonjwa ya ini, matatizo ya tezi ya madini joto (thyroid) na kutokuwa na nguvu za kiume.

Dawa nazo huchangia kukua kwa matiti kwa mwanaume, mfano; dawa za kulevya, dawa zenye homoni za kike iwe za kunywa au za kupaka, pia dawa ya saratani na kadhalika.

Dawa nyingi zimechangia wanaume kuwa na matiti makubwa bila kutambua kwamba amekuwa akishika au kutumia kemikali hizo. Ukimwi pia una husiano na kukua kwa maititi kwa mwanaume.

Hivyo, kukua kwa matiti kwa mwanaume ni kiashiria kwamba kuna shida au ugonjwa katika moja ya viungo vya mwili wake, au matiti yake moja kwa moja. Ni vyema kwenda hospitali kufanyiwa uchunguzi wa kina, kujua ni ugonjwa gani unanyemelea.

Vipimo vya damu hufanyika kuangalia tatizo kwenye viungo mbalimbali, pia ‘ultrasaundi’ ya matiti au mamografu hufanyika, pia kipimo cha kufyonza sehemu ya titi na kupima maabara huweza kuhitajika, iwapo ni titi moja limevimba. Matibabu ya kukua kwa matiti ni pamoja na kutibu ugonjwa au shida ya awali, mfano kuacha dawa husika, kutibu saratani na kadhalika.

Advertisement