Kwako ni kwako hata kukiwa nje!

Saturday February 9 2019

 

Utawajua tu watu ambao wanagusa vile vyombo vyetu hata kama ni mara moja moja. Kuna mmoja alihoji wimbo wa kapuku aliyetangaza kumnunulia ndege mchumba wake wakati yeye hajawahi kumiliki hata guta. Hakuishia hapo, alihoji tena pale daktari wa muziki alipoaga kurudi nyumbani kwao Songea halafu akaendelea kuranda kwenye mitaa ya Sinza.

Wanamuziki ni watu wa ajabu sana. Vijana fulani waliojiita jina la Jimbo linaloongoza kwa “Uswazi” hapa nchini walisema “Nyumbani ni nyumbani hata kukiwa jalalani”. Walimkandia mwenzao aliyekimbia jumba la tope kwao na kwenda kuchezea “rimoti” kwa marafiki.

Lakini mimi nilishaingia kwenye wasiwasi: Kama ukiwauliza vijana hawa ni kwa nini wao waliicheza mitaa ya Uwanja wa Taifa na Chang’ombe Unubini badala ya kwao Msanga Ngongele na Kishumundu hutapata jibu zaidi ya “popote kambi”. Hivi kambini ndo nyumbani?

Hata hivyo nawapongeza vijana hawa kwa fikra chanya. Suala la “nyumbani ni nyumbani” halina mjadala. Kwako hata kukiwa madongo kuinama kuna thamani zaidi ya kwa jirani kwenye runinga na viyoyozi hadi maliwatoni. Hata kama kuna mbwembwe za aina gani!

Ukitaka kuamini ebu pata dharura itakayokulazimisha kulala kwenye nyumba ya wageni (wageni kweli au…?) Hakika asubuhi utaamka ukikifikiria kitanda chako nyumbani. Na utakapofika ni lazima utalala tena

Au pata mchongo uzamie nchi za mbele (a.k.a. mamtoni, majuu au nchi za watu) kwa miaka mitano tu. Aisee utajua kuwa ugonjwa unaoitwa “Home sick” ni hatari zaidi ya Kimeta. Yaani hujui unachoumwa lakini utawashwa kuanzia kidole cha mguu hadi unyweleni kama mtoto anayeumwa na usingizi. Ukifanya maskhara unaweza kurukwa na akili.

Binadamu analazimika kupumzika baada ya kufanya majukumu yake kila baada ya muda fulani. Anatumia nguvu na akili nyingi akiwa shuleni au kazini, hivyo hana budi kupata muda wa kupumzisha mwili na akili. Wapo wanaojituliza kila wiki, kila mwezi na kila mwaka.

Katika likizo ya mwaka ndipo umuhumu wa nyumbani unapokuwa mkubwa. Waajiri kwa kulifahamu hili hutoa pesa ya kumtosha mwajiriwa wao aende kuishi maisha mazuri ya asili yake, akale vyakula bora asilia, akanywe maji salama ya kisimani na akavute hewa safi isiyo na kaboni na akili yake ikajengwe upya.

Binafsi nakumbuka ulifika wakati nilikuwa nashindwa kusoma namba za vocha pale ninapoikwangua. Lakini nilipoenda likizo kwa mwezi mmoja tu niliweza kusoma maandishi madogo kwenye “novo” za Corgi Books. Hii ni moja ya faida za kurifreshi mwili na akili.

Katika maisha yetu ya sasa binadamu tunakwenda mbio kama upepo. Watu hasa tunaoishi Mijini tunaona muda unakimbia, nasi hatuna budi kukimbizana nao. Unaamka saa moja asubuhi, unafungua ofisi lakini ghafla unalazimika kuifunga kabla hata ya kufanya kile ulichokusudia.

Pamoja na kazi za kila siku, utapokea simu zaidi ya kumi za watu wanaokuhusu wakikutaka msaada wa kifedha, simu zingine kutoka kwa baba mwenye nyumba wako, mwenye fremu uliyopanga, mwalimu kutoka Shule wanazosoma wanao na dakitari mwenye Zahanati inayotibu familia. Unadhani walikukumbuka kwa salamu tu? Hapana. Mtoto wa kazi naye anadai LUKU imekwisha!

Kutokana na kichwa kuzingirwa na mambo yanayokizidi, mwili unatumia nishati za ziada kukipunguzia mzigo. Tena wakati mwingine mwenyewe unaamua kupata “angalau kamoja au tuwili twa barrrridi sana” ili urifreshi maind.

Hili nalo linakupelekea ukutane na bili ulizozikimbia wiki iliyopita. Kabla hujamaliza chupa ya pili mama watoto anakupigia kukutaka hela ya bajaji amkimbize mtoto wa dada yake Hospitali na mhudumu mpya anakuletea bili ya wadada wawili walioingia baada yako. Usiniulize mahusiano yenu.

Sasa badala ya “tuwili” inakuwa “tutano tu”!

Ndiyo maana nasema kupumzika ni lazima. Wayunani (Wagiriki) walijipangia kurudi kwao kila msimu wa Krismasi tena hata kabla ya sikukuu hiyo kuwapo. Wachagga nao wakaichagua siku kama hiyo kukusanyika nyumbani na kujadili changamoto na mafanikio yao. Wayahudi hukutana nyumbani katika msimu wa Pasaka.

Ngoma ilikuwa ni kwa Wajapani. Enzi zile ilikuwa ukimtajia Mjapani neno “likizo” ilikuwa ni zaidi ya kumtusi. Hawa jamaa hawakuwa wakitaka kupumzika kwa sababu waliamini kazi ndiyo maisha ya kila siku. Hawakuwa tofauti na wadudu mchwa.

Lakini jamaa wakaanza kudata mapema sana. Kuna wakati walianza kubomoa kile walichokijenga kwa nguvu nyingi sana, wakasingizia eti madhara ya mabomu yaliyopiga Hiroshima na Nagasaki yalikuwa endelevu. Walipowatazama Wachina wanavyoendelea kwa kasi nao wakabadili misimamo na kuanza kwenda likizo.

Sina maana kwamba mtu hatakiwi kufanya kazi za ziada, lakini kazi nyingi hazitakuwa na maana iwapo zitakuwa na ubunifu mchache. Mapumziko ya kutosha ndiyo chanzo cha ubunifu. Lala mapema baada ya kazi, tulia na familia siku za wikiendi na uende kijijini wakati wa likizo.

Miti inafanya kazi sana kama kusafisha hewa tunayovuta, kuzaa mboga, dawa na matunda, kutunza ardhi dhidi ya mmomonyoko na kadhalika. Baada ya mzunguko wake kukamilika nayo hupumzika kwa kupukutisha majani. Hujijenga upya na kurejea na nguvu mpya.

Advertisement