Kwanini unapaswa kula boga kila siku?

Friday May 10 2019

 

By Hadija Jumanne

Boga ni tunda litokanalo na mboga za majani zinazojulikana kwa jina la majani ya maboga.

Tunda hili lina protini inayosaidia kupambana na magonjwa yatokanayo na fangasi katika mwili wa binadamu.

Maboga yana kiwango kikubwa cha potasiamu na alikalini, hivyo ukila kila siku husaidia kuzuia saratani na husaidia kuleta nafuu kwa watu wanaoumwa kichwa.

Mtaalamu kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe (TFNC) Elizabeth Lyimo anasema pia mbegu za maboga zina protini na madini ya chuma, kopa, manganizi na zinki.

Hata hivyo, anasema baadhi ya watu hawajui faida ya boga mwilini.

Lyimo anasema juisi ya boga lililochemshwa ni nzuri kwa watoto wenye umri wa miezi sita na kuendelea.

“Katika mlo wa mtoto jaribu kumsagia kiasi kidogo cha boga lililochemshwa vizuri, angalau mara moja kwa siku,” anasema Lyimo.

Protini iliyopo kwenye boga, hutibu pia michubuko inavyotokana na mkojo au nepi pamoja na matatizo mengine ya kiafya, huku ikizuia aina 10 za fangasi hasa Candida Albicans ambayo ni hatari.

Pia, anazitaja faida za ulaji wa maboga na mbegu zake katika mwili wa binadamu akisema maboga hupunguza mafuta kwenye mishipa ya damu.

Anasema ulaji wa mara kwa mara wa mbegu hizo huzuia ugonjwa wa kiharusi, mshtuko wa moyo na husaidia ufanisi wa utumbo mkubwa kufanya kazi vizuri.

Kwa muda mrefu, maboga yamekuwa yakitumika sana katika tiba za kiasili kama kutibu kisukari, shinikizo la damu, kiasi kikubwa cha mafuta mwilini na saratani katika nchi za China, Korea, India, Yugoslavia, Argentina, Mexico na Barazil.

Advertisement