Laki moja waliofaulu kukosa kidato cha tano

Tuesday January 29 2019

 

By Elizabeth Edward, Mwananchi

Pamoja na kukua kwa ufaulu kitaifa wa mtihani wa kidato cha nne mwaka 2018, zaidi ya watahiniwa 170, 301 waliofaulu sawa na asilimia 47.5 hawatoweza kuendelea na masomo ya kidato cha tano katika shule za Serikali.

Hawa ni wale waliofaulu kwa kupata daraja la nne ambalo hutambulika kama daraja la ufaulu, ondoa asilimia 20.7 waliofeli kabisa.

Akitangaza matokeo ya mtihani huo wiki iliyopita, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Charles Msonde alisema watahiniwa wa jumla 322, 965 sawa na asilimia 78.38 walifaulu kwa kiwango cha daraja la kwanza hadi la nne.

Katika idadi hiyo ni watahiniwa wa shule 113, 825 sawa na asilimia 31.76 ndio waliopata daraja la kwanza hadi la tatu hivyo kujihakikishia nafasi ya kuendelea na kidato cha tano.

Kwa mujibu wa mfumo wa elimu nchini, mwanafunzi anaweza kuendelea na kidato cha akiwa na ufaulu wa angalau alama C katika masomo matatu.

Kwa sura hii watahiniwa hawa waliopata daraja la nne, wamekosa fursa hiyo kwa kukosa kigezo cha kuwa na angalau C tatu. Wapo wanaoweza kuendelea na kidato cha tano katika shule binafsi kwa sharti la kurudia baadhi ya mitihani ili kupata sifa stahiki.

Hawa watalazimika kutafuta njia nyingine za kuendelea na masomo ya juu. Makala haya yanatoa njia kadhaa mbadala zinazoweza kutumiwa na wanafunzi hawa kujiedeleza.

Rudia mitihani

Njia mojawapo rahisi ya kurudisha matumaini ya ndoto zako za kusoma inawezekana kwa wewe kuamua kurudia mitihani yako kwa mara nyingine. Mfumo wetu wa elimu unatoa fursa hiyo ya kurudia mitihani na ndio maana kuna utaratibu wa watahiniwa binafsi.

Soma ngazi ya cheti

Fursa nyingine iliyopo kujiendeleza ni kusoma fani mbalimbali zinazoanza kwa ngazi ya cheti. Ikumbukwe badhi ya fani elimu ya cheti inatosha kuwa kipimo cha mtu kupata ajira.

Kwa mujibu wa mfumo wa elimu nchini, kuna vyuo vingi vya kada ya kati vinavyotoa elimu mbalimbali za astashahada ya msingi, ngazi ambayo ni maalumu kwa wahitimu wa kidato cha nne na cha sita. Kutoka astashahada au cheti cha msingi, mwanafunzi anaweza kuendelea hadi ngazi ya cheti cha juu, stashahada na hatimaye kupata fursa ya kusoma elimu ya chuo kikuu.

Unaweza kufika chuo kikuu kwa kutumia njia hii ya kusoma. Vipo vyuo vikuu vinavyowakubali wanafunzi waliopitia mfumo huu. Vyuo hivi vina ithibati ya Baraza la Usimamizi wa Elimu ya Ufundi (NACTE).

Hata hivyo, ni vyema kutoa angalizo na vyuo vinavyotoa mafunzo kwa ngazi za cheti, kwani baadhi yao havina sifa na havitambuliki na NACTE.

Kabla ya kujiunga na chuo chochote, tafuta taarifa zake katika baraza hilo, ikiwamo kupitia wavuti wao wa www.nacte.go.tz

Jiunge na Veta

Fursa nyingine inayotumiwa na baadhi ya wanafunzi wanaoishia kidato cha nne, ni kusoma masomo ya ufundi katika vyuo vinavyosimamiwa na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA).

Wengi wamekuwa na mtazamo hasi na vyuo vya VETA wanasahau kuwa vyuo hivi vina msaada mkubwa kiajira na hata kujiendeleza zaidi kielimu. Zaidi ya yote wigo wa mafunzo ya VETA umekua na kuhusisha mambo mengi ya kiufundi ya kisasa na yanayolipa kiajira iwe ajira binafsi au ajira rasmi.

Hivi sasa VETA inaendesha kozi kama masomo ya madini, utalii, Tehama na mengineyo muhimu katika zama za sasa

Advertisement