Lawama hizi hazitasaidia kupunguza ajali barabarani

Wednesday October 31 2018

 

By Salim Said Salim

Golikipa namba moja wa timu ya Zanzibar na mchezaji wa mpira wa magongo na kriketi katika miaka ya 1960 na 1970, Mohamed Maulidi (Machaprala) pia aling’ara sana katika sanaa ya taarab kama mwimbaji na mpigaji ala.

Nyimbo nyingi za Machaprala aliyefariki miaka mitano iliyopita, zimeacha mafunzo makubwa ya maisha kwa jamii ya watu wa Zanzibar na mashabiki wa muziki wa taarab Afrika ya Mashariki.

Kila nikiusikia wimbo wake mmoja maarufu wa ‘lawama …lawama….lawama ….’ hukumbuka lawama na maapizo ya laana wanayopata askari wa kikosi cha Usalama Barabarani Visiwani.

Kama wapo watu wa idara, taasisi au kikundi cha watu Zanzibar ambao wamegeuzwa kama kiti cha sinema au gari ya daladala kwa kila akataye tiketi hukaa basi ni trafiki.

Kila apendae kulaumu basi wa kwanza huwasakama kwa lawama na wakati mwingine kwa lugha ya matusi.

Ikitokea unamsikia mtu anawapongeza hawa jamaa wanaovalia sare nyeupe kama yange yange, basi huwa kama kupatwa kwa jua au mwezi.

Hapana ubishi wapo baadhi yao waliokubuhu kwa jeuri, ufedhuli, uonevu na kujiingiza katika vitendo vya rushwa; pia wapo askari wengi wa kikosi hiki wanaofanya kazi zao kwa uadilifu mkubwa, upole, uungwana uliotimia na pia kwa kuzingatia sheria.

Wapo madereva wanaofanya makosa madogomadogo ambao husamehewa na kupewa onyo, lakini hili inaonekana jamii haitaki kuliona. Kichotafutwa ni lawama… lawama.. lawama.

Katika siku za hivi karibuni pamekuwepo na ongezo la kutisha la ajali mijini na vijijini na kupelekea watu wengi kupoteza maisha yao na wengine kupata ulemavu.

Sababu kubwa ni madereva kutozingatia sheria kwa kuendesha vyombo vya moto kwa mwendo kasi, hata katika maeneo hatari, magari ya abiria kujaza watu kama dagaa katika mikebe na magari ya mizigo kupakia mara mbili au zaidi ya uwezo wake.

Siku hizi ni kawaida kupishana na baiskeli tatu au nne katika masafa mafupi nyakati za usiku na wanaoendesha wakiwa hawana taa za mbele wala nyuma na wamevaa nguo za rangi nyeusi au buluu.

Anapotokea askari wa Usalama Barabarani kumhoji dereva wa daladala au kutaka kumfungulia mashtaka utaona watu wanamlaumu askari badala ya dereva na kondakta wake kwa kuhatarisha maisha yao, ya abiria na watumiaji wengine wa barabara.

Madereva wa magari makubwa yanayobeba mchanga, udongo au mawe wanayaendesha kama wana wazimu bila ya kujali njia zinatumiwa pia na wazee, watoto na watu wenye ulemavu.

Utaona gari linaendeshwa kwa mwendo wa kasi kama vile liko katika mashindano na akitokea abiria akafungua mdomo utasikia abiria wengine wanamsakama na kumwambia akitaka starehe akakodi taksi au anunue gari lake.

Abiria hawaoni kuwa maisha yao yapo hatarini na wanaona wanao wajibu wa kuwatetea dereva na kondakta wake.

Lakini makubwa zaidi humkuta askari wa Usalama Barabarani anapozuia hilo gari lisiendelee na safari na kumhoji dereva kwa nini amevunja sheria. Hapo tena utasikia lawama…lawama…lawama kwa hawa askari kama vile wao ndio waliofanya makosa na si dereva wala utingo.

Baya zaidi ni kwamba inapotokea ajali lawama huenda kwa hawa askari kwa kuruhusu gari lililopita mbele yao likiwa linakwenda mwendo kasi au limepakia abiria zaidi ya uwezo wake.

Masikini hawa askari. Sijui wafanye nini waonekane wanafanya jambo zuri na kuepukana na lawama …lawawa…lawama zisizokwisha.

Nafikiri Wazanzibari wanafaa kubadilika na badala ya kuwaona trafiki kama watu wanaostahiki kubebeshwa lawama kila wakati, waiangalie hali halisi na kuelewa kwamba kazi wanaoifanya wengi wao ni kunusuru maisha yao, ndugu na jamaa zao.

Ni vizuri kwa kila anayepanda gari kama abiria kukataa gari kuendeshwa kwa mwendo hatarishi kama gari linalobeba wagonjwa linaloharakisha kwenda hospitali ili kunusuru maisha ya mgonjwa.

Wakati mwingine na hasa nyakati za usiku utaona gari za daladala zinapakia watu mpaka juu ya bodi la gari na wengine, watu watano hadi saba, wananing’inia kwenye mlango wa magari ya mbao. Ni hatari tupu.

Akitokea askari kusimamisha utasikia kelele za abiria na wengine hata kuuliza…. hee mpaka saa hizi mpo barabarani, kama vile sheria zinawazuia askari kufanya kazi baada ya jua kutua au ni rukhsa kuvunja sheria za barabarani nyakati za usiku.

Wakati umefika, kama haujapita, kwa abiria kukataa kupangwa ndani ya daladala kama biskuti katika paketi au dagaa ndani ya mkebe.

Vile watu wanapaswa kuelewa ni haki yao kukataa dereva kuhatarisha maisha yao na ni haki yao kumtaka apunguze mwendo na hata kwenda polisi kumfungulia mashtaka ya kuhatarisha maisha yao.

Huu muhali walionao wa kuoneana haya kukosoana au kuridhia maisha yao kuchezewa utaendelea kuwaponza na kuendelea kupelekea watu wengi zaidi

kupoteza maisha na kuwa na ongezeko la watu wenye ulemavu.

Wazanzibari wasidhani wahenga ni wajinga waliposema “Kawia ufike”. Hii ilikuwa tahadhari kwa wale wanaopenda mwendo wa haraka katika safari zao.

Mantiki ya tahadhari hii tunaiona kila siku kwa ajali nyingi kutokea kwa sababu ya gari kuendeshwa mwendo kasi na kupelekea kutokea ajali.

Vilevile wasikubali gari kupakia abiria zaidi ya idadi iliyoainishwa kwa gari hio.

Wakati mwingine gari huteremsha abiria waliozidi ikikaribia kituo cha polisi na baada ya kupita kituoni hao walioteremka hupanda ili kuendelea na safari. Abiria wanapaswa kukataa mwenendo huu unaohatarisha maisha yao.

Advertisement