Lijue tatizo la kukosa hedhi na jinsi ya kukabiliana nalo

Muktasari:

  • Nasema hivi kwa kuwa kibaiolojia hedhi ya kila mwezi, ni mchakato unaojiendesha wenyewe mwilini kwa ushirikiano wa mfumo wa homoni na ule wa uzazi bila ridhaa ya mwanamke, hivyo mwanamke akikosa hedhi kikamilifu, ni ishara ya tatizo aidha katika mfumo wa homoni au mfumo wa uzazi kwa ujumla ambako kunasababishwa na matatizo mengine kama nitakavyoeleza.

Ni dhairi kuwa, kukosa au kutopata hedhi ni tatizo linalowapata wanawake wengi siku za karibuni na kutokana na maswali ya wasomaji wa kila wiki nimeona nieleze ni nini hasa tatizo hili. Kwanza ifahamike, kukosa hedhi ni tatizo la kiafya hata lisipoambatana na maumivu yoyote lakini mwanamke hapaswi kulifumbia macho tatizo hili.

Nasema hivi kwa kuwa kibaiolojia hedhi ya kila mwezi, ni mchakato unaojiendesha wenyewe mwilini kwa ushirikiano wa mfumo wa homoni na ule wa uzazi bila ridhaa ya mwanamke, hivyo mwanamke akikosa hedhi kikamilifu, ni ishara ya tatizo aidha katika mfumo wa homoni au mfumo wa uzazi kwa ujumla ambako kunasababishwa na matatizo mengine kama nitakavyoeleza.

Tatizo hili kitaalamu linaitwa amenorrhea, hutokea mwanamke anapokosa hedhi mwezi mmoja na kuendelea.

Hivyo kwa mwanamke ambaye pia amekosa hedhi kwa miezi mitatu mfululizo, na kwa wasichana kuanzia miaka 15 hadi 18 ambao nao pia hawajaona mizunguko yao hedhi wapo kundi hili.

Sababu kubwa ya kukosa hedhi tuliyoizowea ni ujauzito. Kwa tafsiri ya kawaida ujauzito ni sababu asili ya kukosa hedhi. Kisayansi mwanamke hapati hedhi wakati wote wa ujauzito.

Sababu nyingine ni matatizo ya kiafya yanayojitokeza katika via vya uzazi na mfumo wa uzazi na kwenye mfumo unaoratibu homoni mwilini na ni muhimu kuwaona wahudumu wa afya ili kuchunguza matatizo haya.

Zipi sababu zinazochangia tatizo hili? Wanawake wengi wamekuwa na swali hili. Tatizo hili linatokea kwa sababu tofauti, baadhi yakisababishwa na aina ya maisha ya mwanamke kwa kutumia aina ya madawa, lakini pia uwepo wa matatizo ya kiafya.

Kwanza tatizo husababishwa na sababu za asili. Mwanamke anaweza kukosa hedhi kwa sababu za asili kama ujauzito, umri wa kupoteza uwezo wa kuzaa, umri mkubwa lakini imethibitika hata kunyonyesha pia kunasababisha tatizo japo kwa wachache.

Sababu nyingine ni matumizi ya baadhi ya njia za uzazi wa mpango. Mfano vidonge vya uzazi wa mpango vinachangia kuharibu utendaji kazi wa mfumo wa homoni na hivyo kukosa hedhi. Hivyo ni kawaida kwa baadhi ya wanawake wanaoutumia vidonge kupanga uzazi kukosa hedhi kipindi fulani. Hata baada ya kuacha kutumia vidonge hivyo, wanaweza kuchukua muda ndipo waendelee kupata hedhi.

Baadhi ya matumizi ya dawa za tiba ya magonjwa mengine pia yanachangia tatizo. Aina ya madawa yamethibitika kuwa na uwezekano wa kuvuruga mfumo wa homoni na hiyo kukosa hedhi kipindi fulani. Mfano dawa za magonjwa ya akili, saratani, sonona, shinikizo la damu na zile za aleji. Hivyo ni kawaida kwa mwanamke aliye kwenye moja ya tiba hizi kukosa hedhi.

Pia matatizo machache yanayojitokeza katika mfumo wa uzazi nayo huchangia. Wakati mwingine ndani yanaota makovu yaliyojitokeza baada ya kufanyiwa upasuaji au tiba ya aina yoyote kuondoa vimbe zilizojitokeza kwenye mfuko wa uzazi. Sababu za kimuundo wa via vya uzazi pia zinachangia, mfano kwa mwanamke ambaye mlango wake wa kizazi ni mdogo na hauwezi kufunguka kuruhusu kutoka kwa damu, japo tatizo hili ni nadra sana kutokea.