Lipo jambo wenyeviti kamati za Bunge kuachia ngazi kimyakimya

Wednesday February 13 2019

 

By Tausi Mbowe, Mwananchi [email protected]

Matukio ya viongozi wa kamati za kudumu za Bunge kujiuzulu ghafla bila kutoa sababu yameendelea kutikisa Bunge la kumi na moja.

Wiki iliyopita Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye alitangaza kujiuzulu uenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Mazingira bila kuweka hadharani sababu za kuachia ngazi huku Katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai akisema mbunge huyo amedai anataka kujikita katika ubunge wake.

Nape anakuwa mwenyekiti wa tano kuachia ngazi kwenye uongozi wa kamati tangu bunge hili lianze baada ya Hawa Ghasia (Mtwara Vijijini) na makamu wake Jitu Soni, Mbunge wa Babati Vijijini kufanya hivyo katika Kamati ya Bunge ya Bajeti, Agosti mwaka jana bila kueleza sababu za uamuzi huo.

Hii ilikuwa baada ya Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara, Dk Dalali Kafumu na makamu wake, Vicky Kamata kujiuzulu Machi 2017, pia bila kutoa maelezo ya uamuzi wake.

Uamuzi wa wenyeviti hao na makamu wao, umekuwa ukiacha maswali yasiyo na majibu huku wengi wakiihusisha na matukio yanayokuwapo wakati huo.

Uamuzi wa Nape

Huku maswali na uvumi ukizagaa kuhusu sababu za Nape kujiuzulu, Mbunge wa Mbozi (Chadema), Paschal Haonga alidai bungeni kuwa “hilo ni shinikizo”, kauli ambayo alilazimika kuifuta baada ya kushindwa kutoa ushahidi alipotakiwa kufanya hivyo.

Kwa mujibu wa Haonga, licha ya kamati iliyokuwa inaongozwa na Nape kusifiwa kwa kazi nzuri, imekuwa na utendaji mbovu, ndiyo maana mwenyekiti ameshinikizwa na kujiuzulu.

Lakini, hata alipochangia mjadala wa kamati yake, Nape hakugusia suala la kujiuzulu kwake badala yake aliwataka wanasiasa wenzake kuweka akiba ya maneno wakati wanapowashutumu wenzao.

“Tujifunze kidogo kuweka akiba ya maneno hasa tunaposhutumiana bila sababu,” alisema.

Ghasia na Nape ambao wote ni wabunge kutoka mikoa ya Kusini wanakumbukwa jinsi walivyolitikisa Bunge kutokana na sakata la korosho mwaka jana, jambo ambalo lilifanya Serikali kuingilia kati na kwenda kununua korosho kwa wakulima.

Rais John Magufuli pia alitamka waziwazi kutofurahishwa na jinsi wabunge wa kusini walivyoshughulikia suala hilo.

Swali la kujiuliza ni kwa nini viongozi hao wote wanajiuzulu kimyakimya?

Nape azungumza

Alipoulizwa na mwandishi wa makala hii kwa njia ya simu sababu za yeye kujiuzulu, Nape alihoji “ Sasa nitakuwa nazungumza kila siku? Nimeshazungumza imetosha chukueni hayo hayo mliyosikia.”

Mwishoni mwa wiki Nape alinukuliwa na kituo cha redio A FM cha Dodoma akisema alichukua uamuzi huo kwa lengo la kujipa nafasi ya kuhudumia jimbo kwa kuwa muda uliobaki ni mdogo kati ya alioomba wa miaka mitano.

“Nimejiuzulu nikafanye kazi jimboni, mijadala yote inayoendelea itakuja tu na niseme kwamba kujiuzulu kwangu kunaweza kuwa na sababu nyingi lakini kubwa mjue ile niliyoandika katika barua na kumpa Spika ni yenyewe, hayo mengine nawaacha watu wajadili,” alisema Nape.

Wachambuzi watoa neno

Wachambuzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa viongozi hao wanaamua kujizulu kutokana na shinikizo kutoka katika ndani ya chama chao.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema anasema Bunge hili limeshuhudia wenyeviti watatu wakijiuzulu kutokana kuchoshwa na kuendeshwa na itikadi.

“Angalia wenyeviti wote walijiuzulu nyakati gani, Dk Dalali Kafumu na makamu wake Vicky walijiuzulu wakati kamati (Viwanda na Biashara) ilipoweka mkakati wa kwenda gerezani kumuona mjumbe mwenzao, Godbless Lema lakini kabla ya tukio hilo halijafanyika wakajiuzulu.

“Hawa Ghasia halikadhalika wakati sakata la mfuko wa fedha za korosho likiendelea kutokota bungeni akajiuzulu na juzi tumeshuhudia Nape akijiuzulu wakati kamati yake ilipaswa kuwasilisha taarifa ya ripoti ya waka 2018,” anasisitiza.

Kwa mujibu wa Mrema, wenyeviti ambao wanaonyesha msimamo na kukataa kuendeshwa kwa kisingizo cha itikadi, ndiyo wanaochukua hatua ya kujiuzulu.

Mrema anasema wabunge wa Chadema walio katika kamati wametoa taarifa katika chama kwamba katika vikao vya kamati walijadili hatua ya Serikali kunyang’anya mashamba wawekezaji, jambo ambalo waliiona halina mustakabali mzuri kwa wawekezaji.

“Ingawa wote (waliojiuzulu) hawatoi sababu lakini ukweli ni kwamba wanachoshwa, kutishwa na kushinikizwa kupitia vyama vyao ili kulinda itikadi badala ya masilahi mapana ya nchi.”

Hata hivyo, Mrema alisema imefika wakati sasa kwa viongozi hao kuweka wazi sababu na watu wanaowashinikiza ili kila mmoja awajue.

“Tunaamini kamati zinaingiliwa, tunataka kumjua ni nani huyo mwenye uwezo na nguvu kiasi hicho. Rais Magufuli juzi amesema yeye haingilii muhimili wowote, sasa huyu anayewaingilia ni nani hasa, wamtaje tumjue.

Mrema anaongeza kuwa kinachoendelea kina athari kubwa na kutishia uhai na uhuru wa Bunge kutokana na wabunge sasa kuogopa kutenda haki.

“Ibara ya 100 ya Katiba inazungumzia kinga na uhuru wa mbunge kujadili bila woga, sasa ukiwatisha itakuaje?” anahoji Mrema.

Anasema kwa sasa Tanzania inashuhudia mambo ambayo mabunge mengine yaliyopita hayakuwahi kuyaona.

Hata hivyo, Katibu wa wabunge wa CCM, Jasson Rweikiza hakubaliani na hoja hizo na kusema suala la kuweka hadharani sababu za kujiuzulu au kukaa kimya ni haki ya mtu mwenyewe.

Kwa mujibu wa Rweikiza, kila mtu ana sababu zake na huwezi kumzuia. “Wapo watu wanaofikia hatua ya kujiua sembuse kujiuzulu?” alihoji Rweikiza ambaye ni mbunge wa Bukoba Vijijini.

Rweikiza anasema kwa Nape hali ni tofauti kwani katika barua yake ya kujiuzulu amebainisha kwamba anataka kupata muda zaidi wa kuwatumikia wananchi wa jimbo lake, jambo ambalo huwezi kuhoji.

Rweikiza anasema hawezi kubashiri sababu za wenyeviti wengine waliowahi kujiuzulu kwa kuwa yeye si mganga wa jadi wala mtabiri wa nyota.

Kuhusu wenyeviti hao kujiuzulu kipindi ambacho kina matukio au hoja katika kamati zao zinazotikisa Bunge, Rweikiza anasema hilo halina ukweli wowote, ni utashi tu wa mtu mwenyewe.

Advertisement