Lulu Diva; Ukiachana na muziki ni mkulima wa kahawa

Saturday April 13 2019

 

By Nasra Abdallah,Mwananchi [email protected]

Wakati akiwa anaonekana ni mmoja ya wasanii wa kike wenye maisha ya juu nchini, msanii wa Bongo Fleva, Lulu Abbas, amesema haishi kwa kutegemea muziki tu bali ana kazi zingine ikiwemo kulima.

Akizungumza na gazeti hili, Lulu maarufu kwa jina la ‘Lulu Diva’ alisema kama msanii hawezi kutegemea kazi moja kuishi mjini.

Staa huyo amesema amekuwa akijichanganya katika shughuli mbalimbali ikiwemo ya kulima, ambayo humuingizia fedha nyingi.

Alitaja mazao ambayo analima kwa sasa kuwa ni pamoja na mahindi na kahawa.

Pia, kwa upande wa muziki alisema kuna majukwaa mengi ya kuuza kazi za wasanii ikiwemo miito ya simu, mikito, ambazo hizi kama ukizitumia vizuri unaishi.

Alipoulizwa kama anaamini baadhi ya wasanii wenye muonekano mzuri wa sura hubebwa katika muziki, Lulu alisema haamini katika hilo kwani wapo wazuri wengi lakini wameshindwa kutoboa.

Advertisement

“Mimi ukiniambia eti uzuri wa msanii ndio unambeba kimuziki, siamini, kwani kuna wazuri wangapi tumewaona lakini wameshindwa kufurukuta, ni juhudi tu za mtu binafsi,”alisema msanii huyo aliyetambulishwa na kibao cha ‘Usimwache’ kwenye soko la muziki.

Wakati kuhusu kuwa mmoja wa watu waliotajwa katika orodha ya wauza dawa za kulevya, msanii huyu alisema ilimuumiza, lakini anashukuru mwisho wa siku aligundulika hana hatia.

“Moja ya jambo lililoniponza ni kuwa karibu na watu wanaohusishwa na biashara hiyo, lakini kiukweli sijawahi kuifanya biashara hiyo katika maisha yangu, lakini nashukuru nalo lilipita kwani ni moja ya changamoto za kuvuka kutoka hatua moja kwenda nyingine katika maisha,” alisema Lulu.

Advertisement