MAGAMBA: Hifadhi ya asili yenye utajiri wa vivutio mchanganyiko

Thursday December 20 2018

Ofisa utalii wa Hifadhi ya Mazingira Magamba,

Ofisa utalii wa Hifadhi ya Mazingira Magamba, Samiji Mremba akizungumza na wanafunzi wa Sekondari ya Zanaki waliotembelea hifadhi hiyo wiki iliyopita. Picha na Tulizo Kilaga 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Takriban kilomita 25 kutoka katikati ya mji wa Lushoto mkoani Tanga, ipo hifadhi pekee ya asili. Hii ni Hifadhi ya Asili ya Magamba inayopo katika ukanda wa Milima ya Usambara Magharibi.

Hata hivyo, kama zilivyo hifadhi nyingi nchini ambazo hufanana kwa mengi, Magamba iko tofauti, ikiwa na vivutio pia vya kihistoria ikiwemo jengo la ofisi la kale, handaki lililotumiwa na Wajerumani na jiwe lenye historia ya aina yake.

Jambo la kufurahisha ni kuwa, uoto wa asili katika hifadhi hiyo upo mwaka mzima na kwa misimu yote ya mwaka mtalii au mgeni anapoitembelea hukutana na hali ya kijani. Lakini nini siri ya hali hiyo?

Ofisa utalii wa hifadhi hiyo, Samiji Mremba anasema hali hiyo inaifanya Hifadhi ya Asili ya Magamba kujitofautisha na maeneo mengi ambayo hukutana na misimu inayoyafanya kubadilika badilika kila mara. “Ndiyo maana tunasema Magamba ni tofauti. Hapa mtalii anaweza kuja na kufurahia mandhari wakati wowote, wapo (watalii) wanaokuja wakati wa masika wakafurahi na wengine kipindi cha kiangazi nao wakafurahi,” anasema.

Mremba anasema mfumo wa ikolojia ya Magamba unaundwa na hali ya unyevu usiokwisha kwa mwaka mzima na kwamba, hata kama jua litawaka vipi, hifadhi hiyo haibadiliki kirahisi.

Anasema, jambo jingine linalochangia kuwapo kwa hali hiyo ni vijito vya maji na maparomoko ya Mto Mkusu usiokauka ambao pia unatumika kama kivutio cha utalii kwa wageni wanaotembelea eneo hilo kutokana na kupita katika sehemu tofauti zikiwamo zenye udongo na mawe.

“Hii ndiyo hali halisi ya Hifadhi ya Asili ya Magamba kwa ujumla, hata hivyo tunajivunia kuwa na vivutio vingi sana vya utalii, yaani nikisema vingi ni vingi kweli.”

Ofisa huyo anavitaja baadhi ya vivutio hivyo kuwa ni pamoja na handaki lililotumiwa na Wajerumani kama maficho na usalama wao na kufanyia utafiti wa madini ya bauxite ambalo linaaminika kutumiwa zaidi wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia kati ya 1914 hadi 1918.

Mremba anasema, “Ndani ya handaki hilo ukiingia hakujawahi kubadilika. Inaonekana ujenzi ultumika kujenga na hawa jamaa (Wajerumani) ulikuwa bora zaidi maana halina mpasuko wowote, isipokuwa kwa sasa wanyama kama popo ndio wanaolitumia, japo mtalii hashindwi kuingia na kujionea ubora wake.”

Vivutio vingine ndani ya hifadhi hiyo iliyopo chini ya Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), ni mimea na miti zaidi ya 59, ikiwamo ambayo ni adimu na pia inayopatikana katika eneo hilo pekee.

Mrema anasema uhifadhi katika eneo hilo ulianza katika miaka ya 1890 hadi 1905 na kwamba, awali kulikuwa na miti mingi iliyopandwa kipindi hicho.

Vivutio vya kihistoria

Mbali ya mimea na miti ya asili na ile ya kupandwa, ndani ya hifadhi hiyo kuna jengo la ofisi lenye historia inayohusishwa na Wajerumani na majengo mengine machache yapo nje ya hifadhi ambayo yalijengwa na wakoloni hao.

Kwa mujibu wa Mremba, jengo la ofisi linalotumika hivi sasa lilijengwa wakati wa ukoloni kwa kutumia miti, udongo na mabati na hivyo kuwa miongoni mwa vivutio vyenye uhusiano na historia ya Wajerumani katika eneo hilo.

“Hili jengo kama unavyoliona limedumu kwa miaka mingi sana, kipindi hicho lilitumika na sasa tunalitumia kama ofisi ingawa hivi karibuni tutahamia katika jengo jipya ambalo tumejenga, lakini hiyo haindoi historia yake,” anasema.

Ofisa misitu anayeshughulika na uhifadhi, Elly Ngemera anasema jirani tu na hifadhi hiyo lipo jengo lililowahi kutumiwa kama makazi ya familia ya Mjerumani na liko katika hali nzuri.

Jengo hilo kwa mujibu wa Mremba, pia ni miongoni mwa vivutio vya kihistoria vinavyowafanya wageni kuvutiwa na hifadhi hiyo, lakini hivi sasa linamilikiwa na wazee wa kijiji cha Magamba.

Anasema pia kuna utalii wa vipepeo vya aina tofauti ambavyo huonekana kwa nyakati tofauti tofauti, wanyama aina mbega weupe na wadudu wa aina mbalimbali.

“Siyo hao tu, lakini kuna vinyonga wenye pembe, mito zaidi ya 20, lakini pia kwa watalii kuna njia ndogo ndogo za kupita zinazowafanya kuyaona vizuri zaidi mandhari ya hifadhi hii.”

Wageni wanaotembelea

Ngemera anasema wageni wanaoitembelea hifadhi hiyo wanatofautiana, wakiwamo watalii, watafiti na pia wanaokwenda kwa ajili ya mapumziko mafupi.

“Kwa mfano, wageni wa ndani wao wanakuja kila mara, hawa ni pamoja na wanafunzi na watafiti. Hawa kwa kweli hawana muda maalumu,” anasema.

Hata hivyo, Mremba kwa upande wake anasema watalii kutoka nje mara nyingi wana miezi na nyakati zao wanazoitembelea hifadhi hiyo.

“Uzoefu unaonyesha kwamba Waisrael wao wanapenda sana kuja mwezi wa pili, Februari, lakini Wazungu kutoka kule Ulaya wao ni Juni, Julai na kuendelea,” anasema ofisa huyo na kwamba, kwa mwaka wanapokea takriban watalii 200 huku asilimia 70 wakiwa ni wageni kutoka nje ya nchi.

Mmoja wa watalii wa ndani, Elizabeth Mnisi anasema upekee aliouona katika Hifadhi ya Magamba ni ule wa kuwa na vivutio vingi mchanganyiko tofauti na maeneo mengine. “Kuna maporomoko, kupanda vilima, wanyama kama mbega na miti mingi ya kipekee, yaani ukitoka katika hifadhi hii akili inakuwa imetulia kwa ajili ya kufanya jambo zuri la kimaisha maana inakuwa imetulia,” anasema Elizabeth, ambaye pia ni mwanafunzi wa Sekondari ya Zanaki iliyopo Dar es Salaam.

Ofisa habari wa TFS, Tulizo Kilaga anasema, “Kwa nini usipende kufika maeneo haya, kwanza panafikika kwa urahisi lakini vilevile hakuna gharama kubwa kufika hapa. Unaweza kuja hata kwa bajaji kutoka Lushoto mjini ukatembea na kufurahia mandhari kisha ukarudi mjini.”

Uhifadhi

Kuhusu uhifadhi, ofisa misitu anayeshughulika na uhifadhi, Ngemera anasema shughuli za uhifadhi hazijaathirika katika kipindi cha miaka ya hivi karibuni kutokana na elimu iliyotolewa kwa jamii.

“Zamani watu walichoma ovyo misitu walipoandaa mashamba yao, lakini hivi sasa hali ni tofauti baada ya kuwapa elimu na pia kuunda kamati kwa kila kijiji vinavyotuzunguka,” anasema.

Advertisement