MAISHA &UHUSIANO : Aina tano za wake

Muktasari:

Mmoja anasema mke wangu anafanya hivi na mwingine analia mke wangu hafanyi vile. Huu mkanganyiko umekuwa mkubwa sana na unasababaisha maumivu na migongano kwenye ndoa nyingi.

Mara nyingi kwenye ndoa kumekuwa na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wanaume, na malalamiko haya yanaelekezwa kwenye namna wake zao wanavyoishi au wanavyofanya. Huyu analalamika mke wangu yuko hivi, na yule naye anasema mke wangu yuko vile.

Mmoja anasema mke wangu anafanya hivi na mwingine analia mke wangu hafanyi vile. Huu mkanganyiko umekuwa mkubwa sana na unasababaisha maumivu na migongano kwenye ndoa nyingi.

Mke mwalimu mkuu

Hawa hujiweka kuwa viranja wa familia hatakama mume ndio anayeleta kila kitu. Kila wakati anatamani aonekane yeye ndio kiongozi wa familia. Maranyingi huwafanya wengine wote ni watoto au wanafunzi bila kujali huyu ni mume wake au yule ni mgeni kaja kutembelea familia.

Wanauliza maswali kwenye kila kitu, utaskia, kwanini umefanya hivi, kwanini hiki kiko pale, kwanini hivi kwanini vile na pia wanaweza kutoa adhabu hata kwa waume zao kwa vitu visivyo vya maana kabisa. Utaskia “umeamua kufanya hivyo ee!! Basi utaona.

Mke ngumi

Wake wa namna hii ni wenye kuudhi kila mara na pia mara kwa mara ni wapenda fujo. Anawezakuweka mazingira ya valangati hatakama haukuwa na mpango wa kurusha ngumi ukajikuta mmekunjana, akianza fujo hajali umelala, umepumzika, unaongea na simu, unakula, uko na marafiki, hilo hajali we fahamu tu inakula kwako hadi hasira zake ziishe.

Wanapenda kupayuka sana, atarusha maneno kwa sauti ya juu tena maneno yaliyounganika kama vile taarabu na kama ndio mnaishi uswahilini kila jirani atajua kimenuka kwenu. Akianza kuongea hanyamazi, bora nyuki au mbu masikioni kuliko mke wa aina hii.

Mke ndoo ya taka

Hawa ni wachafu wakati wote na wala hawajipendi kimuonekano, anaweza kuvaa kitu cha gharama lakini bado hauoni kama kavaa kitu. Unawezakumkuta sehemu ya utanashati sanaaa labda ni sherehe ya watu wazito lakini yeye katokelezea kikawaida sanaaaa na wala hajishangai.

Wako kama wamechanganyikiwa. Ni wavivu wa kila kitu isipokuwa umbea a.k.a ubuyu. Hawa hawafanyi kitu, wao kila kitu dada fanya hivi, dada fanya vile. Yani dada au kaka wa kazi kwao ni zaidi ya punda.

Mke mlinzi

Wake wa aina hii wanawabana sana waume zao. Wana wivu sana na waume zao. Kwake kila mwanamke ni tishio dhidi ya mme wake, hawamuamini mwanamke yoyote kukaribiana na mume wake, hata mume anapokutana na mwanamke ambaye ni rafiki wa mke wake anahofia kumwambia mkewe kuwa nimekutana na rafiki yako kwasababu mke atakosa imani kabisa. Mke wa hivi huwaona marafiki wote wa mume wake kuwa ni maadui na wapotoshaji.

Mke mzuri

Huyu ndio yule mke ambaye amezungumzwa kwenye zaburi na vitabu vingine vitakatifu. Anajali, anajua kupenda, anapendeza na anawapenda wa kwake. Ni wa msaada. Anaweza kusimamia shughuli za mumewe asipokuwepo pasipo shida yoyote. Mara zote yeye ni mlinzi na kiongozi wa kiroho kwa watoto na hata familia yote. Ni muelewa sana, mwenye ujasiri na anayejiamini.