MAKENGEZA : Siri ya wazi, siri ya uwazi

Muktasari:

Na kipimo hiki ni muhimu sana maana watu wana akili zao na ili mradi hawajapigwa pasi au kujaziwa mifuko wasiweze kuona ukweli, wanao uwezo mkubwa wa kupima iwapo kilichotendeka ni haki au si haki.

Mambo mengine Bwana. Mtu atoapo msaada, tunaambiwa kwamba hata mkono wa kushoto usijue mkono wa kulia unafanya nini. Ni siri kati yake yeye na mpokeaji.

Ndiyo maana mambo ya kutoa msaada mbele ya runinga na nini, kweli ni msaada lakini thawabu ya msaada haipo tena. Bila shaka, ameongeza heshima yake mbele ya wengine na kuvuna sifa lukuki lakini thawabu kama thawabu hakuna tena.

Lakini haki ni tofauti. Haki haina budi kupatikana waziwazi. Ndiyo maana kuna msemo kwamba, ili haki ikamilike, si tu itendeke lakini ionekane imetendeka. Ndipo hapo watu wataweza kupima iwapo ni haki ya haki au ni haki feki.

Na kipimo hiki ni muhimu sana maana watu wana akili zao na ili mradi hawajapigwa pasi au kujaziwa mifuko wasiweze kuona ukweli, wanao uwezo mkubwa wa kupima iwapo kilichotendeka ni haki au si haki.

Tuelewane hapo. Hatuongelei sheria. Sheria inaweza kuwa ya haki au si ya haki. Marekani enzi za utumwa na ubaguzi wa rangi, utesaji wa watu weusi ulikuwa ni sheria. Watu walikuwa wanauawa kisheria, wananyongwa kisheria, wanateswa kisheria, wanakatwa viungo kisheria. Enzi za ukoloni na huko Afrika Kusini, wenye nchi kila siku walikuwa wanaambiwa watii sheria bila shuruti. Na iwapo walikataa kufuata sheria za ubaguzi waliteswa, walikamatwa na waliuawa kulingana na sheria za huko. Maelfu ya watu waliuawa kisheria. Sheria si lazima iwe ni haki hata kidogo. Haki yenyewe inaweza kuuawa na sheria.

Lakini kwa watu wenye akili timamu, na ambao hawakuwa tayari kutetea uonevu, ilikuwa wazi kabisa kwamba sheria zile hazikuwa sheria za haki. Sheria ilifuatwa lakini haki haikutendeka. Ndiyo maana watu waliungana na kupambana na sheria dhalimu hadi zikaondolewa ili kufufua haki. Lakini, kwa bahati mbaya, sisi ni binadamu siyo binmalaika kwa hiyo daima wanajitokeza watu wengine ambao, ama watavunja haki bila kujali sheria za haki, ama watatunga sheria za kujifaidi wenyewe bila kujali haki pia.

Na wadhalimu hao wanaweza hata kutumia misahafu kutetea udhalimu wao kudai ni haki ya haki si haki feki, lakini bado watu wana akili wanao uwezo wa kupambanua mambo na hawawezi kukubali. Ndiyo maana kuna kitu kinaitwa haki ya asili ambayo sisi tulio wengi tunaijua, ipo ndani ya mishipa yetu na haiwezi kunyamazishwa na ukatili wa sheria.

Ndiyo maana, kadiri haki inavyopotea, amani hupotea pia maana msingi wa amani ni haki. Angalia amani inavyopotea sehemu nyingi za dunia kutokana na kubomolewa kwa haki.

Tanzania, tunashukuru, hatujasumbuliwa sana na hayo lakini mbegu ya chuki, na dhuluma ikishapandwa, na kumwagiliwa hadi ikue, ni vigumu sana kuing’oa tena. Ubaguzi, chuki dhidi ya kundi hili au lile haviwezi kukaa chumba kimoja na haki.

Ndiyo maana, pamoja na wasiwasi wangu juu ya sheria hizi mpya kutumika kubana maoni ya watu, nilitegemea kwamba angalau haki itatendeka na kuonekana dhahiri kwamba imetendeka.

Gazeti likisema uongo, litaonywa kisha litafungwa, liwe ni uongo tawala au uongo pinzani, uongo uliodhamiria au uongo bahati mbaya. Zaidi ya hapo, nilitegemea watajitahidi kuchambua iwapo ni uongo wa bahati mbaya au uongo uliodhamiria. Lakini naona imekuwa kinyume. Nimetafuta Kiswahili cha double standards bila mafanikio lakini nitajaribu kufafanua. Maana yake ni kwamba unatumia vigezo tofauti kulingana na uko upande gani na kuangalia na jicho gani. Labda tuite ndumilakuwili. Katika mizani ya haki, haiwezekani kuwa na vigezo tofauti, hata kidogo. Uongo ni uongo uwe ni pinzani au uwe ni tawala. Matusi ni matusi yawe ni matusi tawala au matusi pinzani. Chuki ni chuki, iwe ni chuki tawala au chuki pinzani.

Kwa hiyo unaweza kutunga sheria kuzuia uongo na matusi lakini ukiwa na vigezo tofauti kwa tawala na pinzani, hii ni sheria isiyo na haki ndani yake na hata kama shuruti ya sheria hutumika kuwatiisha watu, na hata kuwafunga, kuwafukuza kazi n.k., haki inabaki palepale.

Lakini, nikiangalia dunia inavyokwenda, naona undumilakuwili unazidi kutisha na matokeo yake ni mauaji na labda vita mbele ya safari. Viongozi wa dunia wanapounga mkono mawazo ya ubaguzi waziwazi, matokeo yake ni nini? Tumeona huko kwa beberu mkuu. Weusi wangapi wameuliwa hata na polisi kutokana na ubaguzi huo? Na wanaendelea kuuawa licha ya kuumbuliwa siku hadi siku kutokana na undumilakuwili.

Hukumu dhidi ya weusi inakuwa tofauti na hukumu dhidi ya weupe, kutokana na undumilakuwili. Na sasa ugonjwa huu umehamia New Zealand pia, na muuaji alimnukuu kabisa kiongozi wa beberu mkuu.

Haya ndiyo madhara, matokeo ya undumilakuwili. Kwa beberu mkuu kilianza zamani lakini haya mauaji ya sasa nayo yalianza kama mbegu ndogo ya chuki iliyoachwa kukua. Kwa majirani zetu vilevile. Ukipanda mbegu ya chuki, ukiruhusu chuki kukanyaga haki, mwisho wake ni mauaji ya halaiki.