MAKENGEZA : Uduni wa kubuni ni umbuni

Sunday April 14 2019

 

By Richard Mabala

Sijapata fursa ya kufaidi kiplefti ya Ubungo lakini nimesoma juu yake na kuwauliza wengine. Heko yule aliyebuni. Ni mfano mzuri sana wa jinsi ubunifu unavyoweza kukata mzizi wa fitina mara moja. Kabla ya hapo, ni yaleyale ya fasili ya uendawazimu … kuendelea kufanya yaleyale ingawa inaonekana kushindikana.

Wauguzi wetu wa barabara (hata kama wanatuchoma sindano mara nyingine) wamehangaika miaka nenda rudi kudhibiti wingi wa magari kutoka kona zote hadi nilisikia fununu kwamba muuguzi akionekana amezidi uzito anapelekwa pale.

Baada ya mwezi mmoja aliweza kuvaa sare ileile ya miaka kumi iliyopita. Ilikuwa kazi kweli na heko kwao walioongoza magari miaka nenda rudi jua likiwaka, mvua zikipiga.

Hata hivyo, hatimaye, jitihada zao zote zilifanikiwa kupunguza tatizo, lakini haikuliondoa hata kidogo. Mara PAAP jamaa katengeneza kiplefti!

Kiplefti na matatizo yote yamekwisha, angalau kwa sasa na wauguzi ruksa kunawiri tena. Ila, nina wasiwasi kwamba sasa watazunguka kuwadunga watu sindano tena dah!

Hapo nilipenda kutumia mfano huu wa kiplefti kwenye maeneo mengine. Ni wapi zaidi tunaweza kukata mzizi wa fitna? Na kwa nini huu ubunifu unaonekana mara mojamoja tu?

Kwanza ni jambo la kusikitisha kwamba suala la ubunifu linapewa kipaunyuma kabisa katika mfumo wa elimu. Gwiji mmoja wa elimu alisema kwamba sote tunazaliwa na ubunifu wa hali ya juu kisha tunaipoteza polepole na mara nyingi shule ni makao makuu ya kumaliza ubunifu moja kwa moja.

Lakini ubunifu ni msingi wa maendeleo hasa katika dunia ya leo inayobadilika kila kukicha. Eti kazi ya elimu ni kuwaandaa watoto vizuri kwa maisha yao. Miaka arobaini iliyopita, nani aliwaandaa kwa ulimwengu ya vipakatalishi, mitandao ya jamii, bodaboda na simu janja.

Hata kidogo. Tuliwaandaa katika ulimwengu wa jembe, simu za nyumbani zisizofanya kazi na taipuraita.

Ndiyo maana gwiji mwingine wa sayansi, Albert Einstein, alipoulizwa na mama mwenye mtoto wa miaka kumi huyu mtoto asome nini ii awe kama Einstein. Einstein alisisitiza asome hadithi. Mama akajibu, ameshasoma, asome nini zaidi, Einstein akarudia, hadithi tu.

Na kila alipoulizwa akajibu tena, hadithi tu. Kwa nini? Kwa sababu alijua kwamba hata wanasayansi wanahitaji ubunifu. Utafikiriaje mambo mapya kama yote aliyavumbua bila ubunifu. Tunaweka mkazo kiasi gani kwenye ubunifu katika shule zetu. No ubunifu, no maendeleo.

Pili hata kama tungetaka kusisitiza ubunifu, ubunifu huo utapatikana wapi wakati maudhui ya kufundisha ni nyingi mno. Enzi za gugo, kweli tunahitaji kufundisha kila kitu? Watoto wetu watatumia gugo kutafuta maarifa yote wanayohitaji.

Hawana haja ya kukumbuka kila kitu. Ila wanahitaji stadi, na wanahitaji ubunifu ili kutumia stadi zao vizuri. Kwa hiyo, tungekuwa na kiplefti katika mfumo wetu wa elimu, tungegundua kwamba walimu sasa wamekuwa kama hawa wauguzi wa barabarani. Kazi yao kujaribu kuendesha magari ambayo mara nyingi yanakwama licha ya jitihada zao zote. Wangepewa kazi ya kuwafundisha watoto jinsi ya kupata taarifa, na kuchambua taarifa na kuongeza taarifa zaidi wenyewe, ingekuwa rahisi kupunguza maudhui yote yaliyopo kwenye mitaala na kupata nafasi zaidi kwa ajili ya kuchambua na kubuni.

Kwa njia hiyo, watoto wetu kweli wangekuwa tayari kukabiliana na mabadiliko yote ya dunia. Uchambuzi na ubunifu ndiyo misingi ya kuishi na mabadiliko hayo ambayo mfumo wetu wa elimu hauwezi kutabiri kwa sasa.

Ngoja nimalize na kamfano kamoja ka ubunifu katika hali yetu ya sasa. Kwa kuwa tunakosa ubunifu, tunaendelea kuona madarasa mengine yamejaa watoto zaidi ya mia mbili na kudai tu kwamba ni lazima wajenge madarasa mengine wakati serikali haina hela na wananchi hawana hela pia maana wameshachangia madarasa, maabara, zahanati, ofisi ya kijiji, walimu wa ziada, Mwenge na michango mingine isiyohesabika. Tayari wananchi wengi wanakacha mikutano kwa kuwa wanajua madhumuni ya kikao ni kudaiwa mchango mwingine tena.

Kwa hiyo, madarasa hakuna, fedha hakuna hivyo wanafunzi wataendelea kukaa mia mbili kwa darasa na kushindwa kupata kitu kinaitwa elimu. Hapo tunahitaji kiplefti kweli, hasa tukizingatia kwamba hata mikataba ya haki za elimu na za watoto inasema kwamba kila mtoto ana haki ya kupata elimu lakini si lazima elimu hii itolewe shuleni. Hivyo, na nachokoza tu, mtoto atajifunza zaidi iwapo:

Anakaa na wenzake mia mbili kwenye darasa hili moja siku tano katika wiki.

Anakaa na wenzake sitini mara moja au mara mbili katika wiki.

Natabiri kwamba ukiwapima mwisho wa wiki, yule aliyekaa katika darasa na wenzake sitini au chini ya hapo mara moja au mbili atakuwa amepata zaidi kuliko yule aliyekaa na wenzake mia mbili wiki nzima. Na hapo angalau tutakuwa tumetafuta kiplefti badala ya kung’ang’ania kufanya yaleyale tena na tena bila mafanikio

Nawakaribisha waishiwa wenzangu, tujadiliane juu ya kiplefti zinazohitajika katika mfumo wetu wa elimu tujikwamue. Tumekaa katika jam muda mrefu mno.

Advertisement