Maajabu ya mkulima asiyeona

Muktasari:

  • Pamoja na kutokuwa na uwezo wa kuona, bado anaweza kulima kwa mafanikio akitumia hisia, miguu na mikono katika kuendesha shughuli zake za kilimo

Ukimuona akiwa shambani anavyojituma huwezi kumfikiria kuwa ana ulemavu wa macho. Analima bila kupumzika na hata katika maongezi, huongea huku akiendelea na shughuli zake kama kawaida.

Huyu ni Raphael Bundala anayeishi katika kituo cha watu wasioona cha Agape kilichopo Arumeru mkoani Arusha.

Kwake msemo; “shida si kuzaliwa maskini bali kuishi kimaskini”, una maana kubwa na unabeba ukweli mzito.

Bundala (50) alipata tatizo la mtoto wa jicho akiwa darasa la pili na kutibiwa kwa madawa ya kienyeji, yaliyomsababisha mboni ya jicho kuoza na hatimaye kutoona kabisa.

Anasema kuwa, kutoona hakumnyimi fursa ya kujishugulisha na kilimo na kupata faida kubwa kuliko hata wasio na tatizo lolote.

“Mimi nina tatizo la kutooona, lakini namshukuru Mungu kwani natumia hisia za miguu na mikono katika shughuli zangu zote za kila siku, hasa za kilimo ambacho ni shughuli inayoniingizia kipato kama watu wengine na ninakipenda sana, anasema.

Anaongeza kuwa, akiwa shambani, hutumia miguu sana na mara chache mikono ili kutambua kuwa amelima wapi na wapi bado. Mkulima huyu asiyeona, anatambua ukubwa wa eneo la shamba lake kwa kutumia miguu kupima, na hata kwenye kupalilia mazao yake anajua kuwa hili ni zao na hili ni gugu na kamwe hafanyi makosa.

Alianzaje kulima?

Bundala anaeleza kuwa, wazazi wake walimkuza katika misingi ya kutegemea kilimo. Aidha, alipokuwa akisoma katika shule ya msingi Irente iliyopo Lushoto, walikuwa wakifanya shughuli za kilimo, hivyo kuendelea kumjengea msingi wa kupenda na kuthamini zaidi shughuli hiyo.

Anasema hata alipofanikiwa kujiunga na shule ya sekondari Shinyanga ambapo aliishia kidato cha pili kutokana na uchumi wa wazazi kuwa mbaya, bado alijifunza kilimo.

Maisha baada ya kukosa elimu

Mwaka 1989 wazazi wake walimwozesha mke ambaye pia alikuwa akipenda kilimo, hivyo wakiwa pamoja waliendeleza kilimo cha mahindi, mpunga na karanga kwa ajili ya familia.

Hata hivyo, mwaka 1996 mke huyo alimtoroka na kumwacha peke yake hali iliyosababisha kujiunga na kikundi cha muziki huko Shinyanga na baadaye kwenda nchini Kenya ambapo alikuwa akipiga gitaa katika maeneo mbalimbali.

“Kazi hii ilinipatia kipato kikubwa na baadaye nikaamua kuoa Mkenya ambaye naishi naye mpaka sasa na tumejaliwa kuwa na watoto wanne, ‘’ anasema.

Bundala anaeleza kuwa, kazi za upigaji gitaa zilipungua hivyo maisha nayo yakaanza kuwa magumu. Bahati nzuri alikutana na rafiki yake Mtanzania ambaye aliyemshauri kurudi Tanzania na kuomba kujiunga na kituo kinachowahudumia watu wasioona cha Agape.

Kwa msaada wa rafiki yake huyo aliweza kufika Arusha na kwenda kuomba msaada; alipokelewa na kupewa nyumba pamoja na eneo la kulima, hivyo akarudi tena Kenya kuchukua familia yake na kuanza maisha mapya.

Kilimo na ufugaji

“Baada ya kuanza maisha hapa kituoni, tuliendeleza shughuli za kilimo ambapo tulianza kulima mboga za aina mbalimbali na kufuga kuku,’’ anasema na kuongeza:

‘’Tuliweza pia kutotolesha mayai kwa kutumia mashine, lakini tukashindwa kuendeleza ufugaji huu kutokana na mayai mengi kutoanguliwa.’’

Bundala anaeleza kuwa, mradi wa mboga uliweza kuwaingizia kipato, kwani waliweza kuzalisha na kuuza kwa majirani.

Mpenda kilimo utamjua; Bundala hatosheki na kilimo cha mbogamboga pekee, kwani anasema;

“Si mbogamboga tu, pia tunalima mahindi, maharagwe na mtama. Pia, tumeanza kufuga kuku wachache wa nyama kwa ajili ya kuuza na kujiongezea kipato pamoja na kupata mbolea,” anasema.

Makala haya yaliyoboreshwa ni kwa hisani ya mtandao wa mkulima mbunifu. www.mkulimambunifu.org Bundala anapatikana kwa simu 0764 190 545