Maalim Seif ataandika historia mpya?

Muktasari:

  • Ujio wa Maalim utakiongezea nguvu za kisiasa chama hicho hususani visiwani Zanzibar ambako kiongozi huyo anatazamwa kama haiba yao.

Ndoa ya miaka zaidi ya 25 baina ya CUF na Katibu mkuu wake Maalim Seif Sharif Hamad ilivunjika rasmi Machi 18, 2019 baada ya Seif kujiengua akiambatana na viongozi waliokuwa wanamuunga mkono na kujiunga na ACT Wazalendo ili kuendeleza mapambano ya kisiasa.

Uamuzi wa Seif kujiengua umefuatia uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kuidhinisha uamuzi wa msajili wa vyama vya siasa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali wa chama hicho.

Awali, upande unaomuunga mkono Seif ulifungua kesi mahakamani hapo kupinga hatua ya msajili kumtambua Profesa Lipumba ambaye alijiuzulu uenyekiti 2015 kabla ya kurejea 2016, hatua iliyozua mgogoro mkubwa ndani ya CUF.

Wakati anatangaza kujiengua CUF, tayari upande wa Lipumba ulikuwa umefanya uchaguzi na kumteua mbunge wa zamani wa Gando, Khalifa Suleiman Khalifa kuwa katibu mkuu mpya wa CUF.

Hakuna ubishi kwamba Maalim Seif ni mwanasiasa mwenye haiba ya aina yake na ndio maana amedumu kwenye siasa kwa miaka mingi akiaminika na mamilioni ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.

Hakukuwa na namna nyingine ya Seif na kundi lake kuendelea kufanya siasa ndani ya CUF kwa kuwa sikuwahi kuamini kuwa anaweza kukaa meza moja na Profesa Lipumba ili kumaliza mvutano ndani ya chama.

Ninaamini chama cha siasa ni jukwaa tu linalobeba matumaini ya watu hivyo, uamuzi wa Seif ni sahihi kwa mantiki ya mwanasiasa yeyote anayetafuta jukwaa la kumwezesha kutafuta nafasi ya kuwatumikia wananchi.

Uamuzi huu umekuja kukiwa kumesalia mwaka mmoja na miezi saba kabla ya Tanzania kuelekea kwenye Uchaguzi Mkuu wa 2020 huku sheria mpya ya vyama vya siasa ikiwa na sharti la mgombea kuwa mwanachama wa chama cha siasa kwa angalau mwaka mmoja. Nathubutu kusema katika hili Seif amecheza kama Pele.

Kwa upande wa CUF, uamuzi huu utakipa wakati mgumu chama hicho kwakuwa kinaondokewa na kiongozi ambaye alikita mizizi ndani yake. Ni wazi kuwa CUF mpya ya Profesa Lipumba na Khalifa inaanza maisha mapya na ambayo yanaweza kuchukua muda mrefu kuleta matokeo chanya na ikiwa hakutakuwa na juhudi za dhati huenda CUF ikafa kifo cha mende kama kilichoikuta TLP ambayo sasa imebaki kuwa chama cha Augustine Lyatonga Mrema pekee.

Ushahidi wa shughuli nzito inayomkabili Lipumba bara na Zanzibar ni hatua ya wanachama wa CUF visiwani Zanzibar na Tanga kuchoma bendera za chama hicho punde baada ya Seif kutangaza kujiunga na ACT Wazalendo. Wanachama wamebadilisha zilizokuwa ofisi za CUF kwa kupaka rangi za ACT, haya si mambo madogo kwenye siasa na ni hayahaya yatakayokuwa kaburi au uhai wa CUF kwa sasa.

CUF itakuwa na kazi mbili, Mosi kujiandaa na uchaguzi na pili kuanza maisha mapya ya kujitambulisha kwa umma bila kuwa na mwanasiasa ambaye alionekana kuwa nembo yake.

Aidha kwa ACT Wazalendo kufanikiwa kushawishi Maalim Seif na viongozi wenzake kujiunga nayo, kunatoa taswira njema ya kisiasa kwa chama hicho kilichoasisiwa miezi michache kuelekea uchaguzi wa 2015. Ninaweza kusema ACT imefanikiwa kufanikisha usajili kabambe.

Ujio wa Maalim utakiongezea nguvu za kisiasa chama hicho hususani visiwani Zanzibar ambako kiongozi huyo anatazamwa kama haiba yao.

Aidha ACT imevuna wanachama mashuhuri kama Ismail Jussa, Ahmed Mazrui, Salim Bimani na wengine ambao kwao Maalim Seif amekuwa nembo muhimu ya kisiasa. ACT inaweza kuwa chama kikubwa visiwani humo na kutoa ushindani mkali kwa CCM na vyama vingine.

Naiona ACT ndani ya Ukawa

Ni wazi hatua inayofuata ni ACT-Wazalendo kukaribishwa ndani ya Muungano wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Hili litakiongezea nguvu chama hicho upande wa Tanzania Bara na hivyo kuwa katika nafasi nzuri ya kuleta ushindani katika uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 na uchaguzi mkuu 2020.

Changamoto

Changamoto ninayoiona ni vyama vya siasa nchini ni kwamba vinaongozwa kwa misingi ya haiba au mtu kiasi kwamba inapotokea vinara wa chama kuondoka vyama hutetereka na hata kufa kabisa. Ndicho kilichotokea NCCR-Mageuzi, ndicho kilichotokea kwa TLP, Je, Lipumba na CUF yake watasalimika?

Swali ninalobaki nalo ni je, Maalim Seif ataandika historia mpya akiwa ACT Wazalendo kama aliyoandika akiwa CCM na CUF ambako kote alishika nafasi za juu za uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Uchaguzi wa mwaka 2019 na 2020 utaongea.

Fredrick Nwaka ni mchambuzi wa siasa na mwanahabari wa RFI Kiswahili +255 745 270 347