Madhara watoto kusoma mbali

Dar es Salaam. Ukienda kwenye vituo vya daladala saa 11.00 alfajiri, hutawakosa wanafunzi wakisubiri usafiri kwenda shule.

Bila shaka wanafunzi hao ambao baadhi yao husubiri daladala na wengine mabasi ya shule, huamka saa 10 alfajiri kujiandaa kwa ajili ya safari hiyo.

Miongoni mwa wanafunzi hao huwa ni watoto wenye umri wa kati ya miaka mitatu wanaosoma chekechea hadi miaka 10.

Ni katika kituo cha daladala cha Oilcom, Tabata Segerea, Dar es Salaam, mzazi wa mtoto mwenye umri wa miaka saba, Harriet Isaya anakutana na mwandishi wa habari hizi akiwa na mwanaye.

Anasema mwanaye huamka saa 11.00 kila siku kwa ajili ya maandalizi ya shule. “Kati ya saa 11.45 hadi 12.00 basi la shule huwa linapita, namuonea huruma mwanangu lakini sina namna kwa sababu lazima asome tu kwa kuwa huu ndio mfumo wa Dar es Salaam. Kuamka mapema na kuchelewa kulala,” anasema.

Mtoto huyo, Abraham Andrew anasema, “mama akiniamsha huwa najisikia nimechoka sana, kwa hiyo nikiingia kwenye basi nalala mpaka shuleni.”

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa watoto wengi wanaowahi kuamka kwa ajili ya usafiri ndio wanaochelewa kurejea nyumbani kutokana na kuishi mbali na zilipo shule zao.

Mzazi Pendael Kagoma, anasema baada ya kuhama walikokuwa wakiishi, mwanaye analazimika kubadilisha daladala mara mbili kila siku kwa ajili ya kwenda na kurudi kutoka shule.

Anasema, awali walikuwa wakiishi Gongo la Mboto, lakini walipohamia Tegeta alishindwa kumuhamisha. “Kwa hiyo kila siku mtoto anatoka Tegeta hadi Mawasiliano, akifika huko anapanda tena (gari) mpaka Gongo la Mboto. Namuamsha saa 10 na saa 11 anakuwa tayari kituoni. Anarudi nyumbani saa mbili au saa tatu,” anasema Kagoma.

Mama huyo anasema ameanza kufuatilia uhamisho ili mwanaye anayesoma darasa la sita asome shule iliyopo jirani na nyumbani.

Naye Julieth Sawala anasema aliamua kuanza kumpeleka shule mwanaye ili kutomwamsha alfajiri wakati huchelewa kurudi nyumbani.

“Pia niliona najichosha mwenyewe, kuamka saa 10 kumuandaa mtoto kila siku wakati nami ni mfanyakazi ilikuwa kazi ngumu. Kwa hiyo kila siku naamka saa 12.30 najiandaa na ninamuandaa mwanangu, kisha nampeleka shule nami naenda kazini,” anasema.

Walimu wanasemaje?

Walimu wanasema watoto wanaotoka mbali hufika shule wakiwa wamechoka kimwili na kiakili.

Nicodemus Novatus, mwalimu wa Shule ya Msingi Mwangaza, anasema hali hiyo ni hatari kwa maendeleo ya elimu na mtoto.

“Hata shuleni kwetu wapo watoto wanatoka mbali sana, mtoto huyu hata kisaikolojia anakuwa hajajiandaa kusoma kwa sababu akiingia darasani anakuwa tayari amechoka,” anasema Novatus.

Mwalimu Sharif Kalenga wa Shule ya Msingi Mapambano, anasema kuhama kwa wazazi kutoka sehemu moja kwenda nyingine huku wakishindwa kuwahamisha watoto wao ni sababu ya wengi wao kuamka alfajiri ili wawahi shule.

“Mfano shuleni kwetu kuna watoto wanatoka Kibamba kuja kusoma Sinza, mtoto akifika tu anakuwa ameshachoka, hapo usitarajia ataweza kusikiliza kwa umakini,” anasema Kalenga.

Anasema mtoto anayeamka alfajiri na kuchelewa kulala hata akipewa kazi ya kufanyia nyumbani (home work) hawezi kuifanya vizuri. “Mtoto wa aina hii akija asubuhi atanakiri tu kwa mwenzake ili akusanye daftari, lakini nia ya kumpa kazi ya kufanyia nyumbani inakuwa haijatimia,” anasema.

Athali za kiafya

Wataalamu wa masuala ya afya wanasema ni hatari ikiwa mtoto hapati muda mrefu wa kulala kwa sababu mapumziko humsaidia katika makuzi ya kimwili na kiakili.

Daktari kutoka Chuo Kikuu cha Sayansi Shirikishi, Kituo cha Tiba Muhimbili, Tawi la Mloganzila, Shindo Kilawa anasema upo muda maalumu ambao mtoto anapaswa kuwa amelala ili kupumzisha mwili wake.

Anasema kama hatapata muda mrefu wa kulala anakuwa hatarini kupata matatizo yanayotokana na uchovu.

“Mapumziko ya mtoto yanamsaidia katika ukuaji wake kimwili, kiakili na kisaikolojia. Ubongo wake usipopata muda wa kupumzika ipasavyo ni vigumu kutunza kumbukumbu na hautaweza kujijenga vizuri,” anasema.

Mkurugenzi wa shirika linalojihusisha na masuala ya kisaikolojia kwa watoto, Edwick Mapalala anasema hatua za ukuaji zinategemea namna mtoto anavyopata muda wa kupumzika.

“Saa za mtoto kulala zinatakiwa zisipungue 10 na kama zikipungua unamtafutia maradhi yasiyo ya lazima,” anasema.

Nini kifanyike?

Dk Kilawa anawashauri wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao hawasomi umbali mrefu utakaowalazimu kuamka saa 10.00 alfajiri na kurudi nyumbani usiku wakiwa wamechelewa.

“Hata kwa usalama mtoto asome shule iliyo karibu na makazi yake ili asiteseke, akue vizuri na kusoma. Walau saa za mtoto kulala hazipaswi kupungua nane kila siku,” anasema Dk Kilawa.

Mzazi, Julieth anasema hakuna hasara inayoweza kutokea kwa mzazi kumtafutia mtoto shule ya karibu ili kuondoa mateso ya kumwamsha alfajiri huku akichelewa kurudi nyumbani.

“Suluhisho ni hilo, sasa unakuta mtoto anaishi Ubungo anasoma Mbagala, au anaishi Ubungo anasoma Mbezi kwani huko Ubungo hakuna shule? Kusoma karibu ni msaada mkubwa sana kwa mwanao,” anasema.

Profesa wa Chuo Kikuu cha Marian, Raph Masengi anasema hakuna haja ya kuona ufahari kumsomesha mtoto shule iliyopo mbali na makazi.

“Sasa badala ya kuipenda shule, mtoto ataichukia na mwisho utashangaa anafeli kumbe ufaulu wake unahitaji utulivu wa akili,” anasema Profesa Masengi.

“Mtoto walau basi atembee kwenda na kurudi shule na kama atapanda daladala iwe moja tu. Asikae njiani zaidi ya saa mbili, hii itamsaidia.”