Mafunzo haya ya ndoa ni muhimu Zanzibar

Wednesday January 16 2019

 

By Salim Said Salim

Zanzibar hivi karibuni imeanzisha vyuo vinavyotoa mafunzo ya ndoa. Lengo ni kuwatayarisha wanaofunga ndoa kuelewa mambo yanayohusu maisha ya mume na mke.

Mafunzo haya mafupi yanayogusa kwa undani maeneo mbali mbali ya maisha ya mume na mume na mke yanaendeshwa na Ofisi ya Mufti, Zanzibar.

Kwa kweli Ofisi ya Mufti inafaa kupongezwa kwa uamuzi wake huu utakaosaidia wanandoa kila mmoja kujua wajibu wake na panapotekea kutoelewana suluhu ipatikane waendelee na maisha kwa raha na furaha.

Mafunzo haya ni muhimu hasa wakati huu ambapo ndoa zimegeuzwa mchezo wa kitoto ambao kwa kawaida haukeshi, yaani utawaona wanacheza kwa furaha na ghafla hugombana na hata kupigana.

Hapo zamani ilikuwa kawaida Zanzibar kwa maharusi watarajiwa kutayarishwa na familia, juu ya maisha yanayowangojea.

Kwa mtoto wa kike walikuwapo walimu wawili. Mmoja huwa mwanamke anayemzaa au kumjuukuu bi harusi mtarajiwa. Kazi yake huchukua muda mrefu, tokea msichana anapobalehe kumpa mafunzo, kumtayarisha na hadaa na ulaghai wa kiulimwengu anaoweza kufanyiwa na kumharibia maisha.

Hatua ya pili ni kumjenga kidogokidogo kuwa na uelewa mzuri wa masuala ya ndoa kama sheria, dini, utamaduni, matatizo yanayojitokeza kutoka kwa wazazi, ndugu na jamaa za mume na mke na jamii au wanapojaaliwa kupata mtoto.

Huyu bibi anayetoa mafunzo haya anajulikana kama hutoa mafunzo kwa msichana kwa kukaa naye angalu kwa siku moja au mbili kila mwezi.

Mwanamke mwingine ambaye huwa na umri usiopungua miaka 50 hukabidhiwa mtoto wa kike siku chache kabla ya harusi na kukaa na maharusi kwa angalau wiki moja mpaka bwana na bibi wazoeane kama mke na mume.

Kazi yake ni kumweleza msichana atarajie nini siku ile ya kuolewa, ajitunze vipi wakati ule na baadaye. Huyu bibi anaitwa kungwi.

Kwa upande wa pili, kazi ya kumtayarisha bwana harusi mtarajiwa ilikuwa inafanywa na wajomba (ndugu wa mama) au rafiki wa karibu wa wazazi wa mwanaume.

Mjomba au huyo rafiki hukabidhiwa kijana kumsuka na kumpika kwa kumweleza yalio wazi na yaliyojificha katika ndoa na hata kumpa uzoefu wake na wa watu wengine katika maisha ya ndoa.

Kwa bahati mbaya utamaduni huu wa Wazanzibari umeanza kutoweka na athari zake zinaonekana kwa watu wengi kugeuza maisha ya ndoa kama

mchezo wa kitoto, yaani haichukui muda ndoa huvunjika tena sio kwa.

Takwimu za ndoa zilizoparaganyika zinatisha. Kwa mfano takwimu ziliotolewa na Ofisi ya Mufti zilionyesha kutoka 2012 hadi 2016 zilikuwepo kesi 2,841 za kutaka ndoa zivunjwe na mahakama ya Kadhi kutokana na sababu mbalimbali.

Hizi ni kesi ziliofika mahakamani, lakini ndoa ziliovunjwa kimyakimya mitaani si ajabu ni mara tatu au nne ya hizi.

Hii haitoi taswira nzuri na baya zaidi ni mateso na

maumivu wanayopata watoto baada ya wazazi kuachana na kila mmoja kwenda njia yake au baadaye kuishi na mama au baba wa kambo.

Mara nyingi watoto hukosa malezi mazuri na matunzo ya kuwajengea maisha mazuri ya baadaye.

Hivyo, Ofisi ya Mufti imefanya jambo zuri kuanzisha mafunzo haya na yapo matumaini ya hali kubadilika kwa vile mume na mke watakuwa wanaelewa wajibu na majukumu yao na wanavyotarajiwa kuishi

kwa kuvumiliana, kutokubali kuchonganishwa na watu wao wa karibu au mbali na kufahamu shida watakayowapa watoto wakiamua kuachana.

Jambo jingine linalofurahisha ni hatua ya Tume ya Kurekebisha Sheria ya Ndoa ya Zanzibar hivi sasa kukusanya maoni ili iwepo sheria itakayozingatia matatizo ya ndoa yanayojitokeza na kupelekea ndoa nyingi kuvunjia.

Advertisement