Mahaba ya wabunge na fujo za viti maalumu

Mwaka wa nne sasa. Viongozi waliahidi ambayo watafanya. Unakumbuka Rais alikuahidi nini? Mbunge wako kafanya alichoahidi? Kama 2020 wataahidi mapya, vipi kuhusu mambo ya zamani? Kuna mwenye ilani ya vyama husika? Au lawama tu bila kufuatilia walichoahidi?

Nimekupa ‘home work’ kafanyie kazi. Bado muda mfupi kabla ya uchaguzi mwingine. Ni wakati wa kupata ‘Upendo wa Agape’ kutoka kwa mbunge wako. Atakusikiliza kwa heshima na adabu kuliko mke/mumewe. Ndio wakati ambao anavutiwa na mpiga kura kuliko tendo la ndoa.

Bongo ni taifa la vyama vingi, na haki ya kuchagua viongozi tumepewa. Kwanini tuwe na viongozi mizigo, vyama kutoa wabunge kibao wa bwerere ni sahihi? Suala la Viti Maalumu halina msingi kidemokrasia wala uhalali wa kimantiki! Ni masalia ya tamaduni za siasa ya kikoloni.

Tangu zamani, Wafalme au watawala wa kigeni walikuwa wakiteua watu kuwawakilisha maeneo fulani ya kitawala. Watu hao lengo lao kubwa si kutumikia wananchi walio chini yao, bali kuhakikisha maslahi ya kiutawala au ya kiongozi yanalindwa.

Kwanini kundi la walemavu, wanawake na vijana? Wabunge wa kuchaguliwa hawawezi kuwakilisha hayo makundi ya majimbo yao? Kama ni kila kundi, basi tuwe na wabunge kwa makabila madogo kama Wahazabe.

Sikubaliani na hiyo hoja. Kila kitu kinakuja na wakati, kama leo hatuna wanawake wengi bungeni ina maana wakati bado haujafika. Hata jeshini walikuwa wachache tofauti na sasa. Tunateketeza bajeti ambayo ingesaidia makundi hayo bila uwakilishi bungeni.

Nafasi 10 za kuteuliwa na Rais lengo ni zuri. Inategemea na aina ya Rais. Hizo nafasi zingetumika kwa watu wapya wasio na mizizi ya kutosha kisiasa, lakini wanaweza kuwa mawaziri wazuri kama Dk Mpango. Tuliona awamu zilizopita waliteuliwa watu wengi kulipa fadhila.

Kuna wasomi wanaoweza kuongoza wizara nyeti lakini hawataki kugombea ubunge kwa sababu zinazofahamika. Kama matumizi makubwa ya pesa ‘takrima’. Hao ndio walistahili kwenye nafasi 10 za Rais wamsaidie. Tunaweza kupata mawaziri wasio wabunge ili waweze kukaliwa vyema kooni.

Wabunge ni wawakilishi wa wananchi. Viti maalumu wanamwakilisha nani? Kwanini walipwe mshahara na marupurupu wakati tuna wawakilishi wetu kila jimbo? Ukatae ukubali huu ni mzigo tunaobeba bila kutaka. Haya mambo ni ya kupigia kelele yabadilishwe.

Kibaya zaidi vyama vinateua ‘watu mizigo’ kulipana fadhila. Wanagonga meza, kuzomea na kukubali kitu kiitikadi siyo maslahi ya taifa. Msimu wa mahaba ya wabunge na fujo za Viti Maalumu umewadia. Kama tunajenga taifa tuachane na haya mazingaombwe.