Makada CCM wazidi kupeleka ujumbe uchaguzi 2019/2020

Wednesday April 10 2019

 

By Florah Temba, Mwananchi [email protected]

Wiki iliyopita Jumuiya ya wazazi ya CCM iliadhimisha “Wiki ya Wazazi”. Viongozi mbalimbali wa chama hicho, walisambaa katika maeneo mbalimbali ya nchi kueneza ujumbe wa maadhimisho hayo.

Mkoani Kilimanjaro, kilele cha wiki hiyo kiliadhimishwa Aprili 2, 2019, mbele ya Naibu katibu mkuu wa Jumuiya ya Vijana (UVCCM) Taifa, Galila Wabanhu.

Wiki hiyo yenye kaulimbiu ya “Elimu, malezi na maadili ni msingi wa uongozi Bora, chagua viongozi makini 2019”, iliadhimishwa katika wilaya za Same na Rombo.

Katika maadhimisho hayo, Wabanhu ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC) alizungumza na wanachama katika kikao cha ndani na kupokea wanachama wapya na kama kawaida hakuacha “kukemea usaliti na mamluki ndani ya chama”.

Wabanhu alirudia ujumbe uliotolewa hivi karibuni na mjumbe mwenzake, wa NEC na mwenyekiti wa jumuiya ya wanawake (UWT), Gaudensia Kabaka wa kuonya

mamluki na wasaliti ndani ya chama ambao wamekuwa kikwazo katika uchaguzi mbalimbali.

“Mmesema hapa Same Wazazi wako 13,000, lakini ukiangalia kura alizopata Mbunge wa CCM Same, hazifiki hata nusu, ni kwamba kuna mamluki wengi na wasaliti. Tufike mahali tuwakatae ili kuimarisha chama.

Akiwa Rombo anasema “Kwa hapa Rombo, Jumuiya ya Vijana na Wazazi tunayo wanachama zaidi ya 11,000, sasa tukifikia mahali pa kujiuliza tulishindwaje katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, ambapo tulipoteza Mbunge na kuambulia diwani mmoja katika kata 28, tutabaini kuwa usaliti bado ni mwingi”.

Kiongozi huyo alisisitiza, “kuna mchakato unakuja, tutawaondoa watu ambao wamekuwa wakikaa kwenye chama ili kuonekana, kumbe ni wasaliti. Hatuhitaji CCM ya magwanda, tunahitaji CCM ya damu na moyo”

Aidha alisema ni bora kukawepo na wanachama wachache, ambao wanakipenda chama na kukitumikia kwa moyo na uaminifu, kuliko kuwa na wanachama wengi jina na wa mashati ya kijani bila msaada wowote ndani ya chama.

Akitoa wito, anasema, “ndugu zangu, tuendelee kushikamana ili kuhakikisha tunafika kule tulikokukusudia. Chama chetu bado kina nguvu kubwa, na mahali ambapo tunashindwa, tunagawa wenyewe,” alisema.

Tatizo jingine

Inaelekea tatizo si usaliti pakee. Wabanhu anawaonya pia viongozi wa chama hicho aliosema wamekuwa wakitanguliza uswahiba na kusahau maslahi mapana ya chama.

“Kuna baadhi ya viongozi wa chama ambao ni tatizo. Wamekuwa wakitanguliza mbele uswahiba, udini, ukabila na ukanda na kuharibu. Wenye tabia hiyo wabadilike na kuhakikisha wanaweka mbele maslahi mapana ya chama.”

Kuhusu wenye fedha

Wabanhu anasema chama hicho hakiko tayari kuwalea watu wenye fedha, ambao wamekuwa wakijitokeza na kujipendekeza kwenye chama wakati wa uchaguzi.

Anasema kila aliyekitumikia chama lazima anufaike, na wale ambao wanajifanya wana fedha na kusubiri wakati wa uchaguzi wakijua fedha zao zitawafanya washinde, watambue kuwa muda wao umefika mwisho.

“Kwa sasa chama kitawashangaza wengi kwa kuwa kuna maeneo yatarudishwa majina ya watu wa chini kabisa ambao hawakutarajiwa... wengine wamekuwa hodari na kuanza kujitokeza kusaidia kwenye misiba ili waonekane ilhali chama kilikuwapo siku zote na hawajawahi kujitokeza kukisaidia,” alisema .

Wabanhu anatoa ombi: “Msiwalee watu hawa. Na kwa kipindi hiki, tutarudisha hata jina la mtu wa chini kabisa, kwani tunawafahamu vizuri watu wetu, na hatuhitaji Wana CCM wa magwanda, tunahitaji wana chama wa damu wenye kukipenda chama kutoka moyoni.”

Aliongeza kuwa “Waambieni hao wanaojipitisha na magari yao kwa sasa kuvizia ubunge. Wabunge wetu tunawajua. Leo wamekuwa hodari kujitokeza kusaidia kwenye misiba, mbona wakati uchaguzi haujakaribia hawakujitokeza kukisaidia chama?” anahoji na kuongeza lazima tujenge maadili ndani ya chama.

Anasema kuna watu wako katika chama hicho kama sehemu ya kupitisha mambo yao na hawatawavumilia.

“Wakishachaguliwa wanasepa na kukiachia chama mzigo wa lawama kutoka kwa wananchi, hawa hatuwezi kuwavumilia wala kuwalea na kama mtu hawezi kufanya kazi, ni bora tu ahame,” anasema

Kununua kadi

Kada huyo anaonya pia wenye tabia kuwanunulia watu kadi kipindi cha uchaguzi ili washinde kwenye kura za maoni.

“Naomba muache tabia hiyo, kwa sasa chama kiko makini na hakitaweza kumvumilia mtu wa namna hii... Tukikugundua una makundi, na umekuwa unatoa fedha ili uchaguliwe, hatukupi nafasi ndani ya chama. Na kwa sasa mtu akituletea mchezo, tunamnyang’anya kadi yetu, ili aende anakotaka, kwani muda wa kuleana haupo,” anasisitiza.

DC atoa yake

Kikao hafla hiyo alikuwapo pia Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule aliyesema wameendelea kutekeleza ilani ya chama hicho kama vile Rais John Magufuli aanavyodhamiria.

“Utekelezaji unaenda vizuri na miradi mingi ya elimu, afya na maji inaenda vizuri, tatizo lipo kwenye mradi wa umeme vijijini unaotekelezwa na REA. Mkandarasi amekuwa akisuasua katika utekelezaji,” alisema.

“Rea awamu ya tatu umekuwa na changamoto nyingi,. Mkandarasi ameweka nguzo na kuondoka na linaonekana ni tatizo la mkoa mzima, tusaidie kuliwasilisha hili huko juu, litafutiwe ufumbuzi, kwani linafanya wananchi waichukie serikali.

“Tunaendelea kuitekeleza ilani ya chama vizuri, na kufanya yale ambayo hayatawapa hasira wananchi, ili kuiwezesha CCM kushinda katika chaguzi zilizoko mbele yetu ukiwemo wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwakani.”

Katibu wa Wazazi Wilaya ya Same, Halima Ligae anasema wamefanya maandalizi mbalimbali kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa ili kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo.

Alisema moja ya maandalizi waliyoyafanya ni pamoja na kuwabaini watumishi wa serikali ambao hawakiungi mkono chama hicho ili kushauri chama namna ya kuwatumia.

“Katika Wilaya hii tumejipanga vizuri kusimamia uchaguzi wa serikali za mitaa ambao unatarajiwa kufanyika mwaka huu, na tayari tumejiwekea maandalizi, lengo letu likiwa ni kukiwezesha chama kupata ushindi.”

Anasema pia wameendelea kuhamasisha watu wenye mapenzi mema na chama hicho ambao si wanachama kujiunga. Siku hiyo wanachama wapya 40 kutoka vyama mbalimbali vya upinzani walijiunga na chama hicho katika wilaya hizo.

Advertisement