Makipa wanaovuna pesa nyingi Ulaya

Moja maeneo magumu kucheza katika soka ni nafasi ya kipa ambayo muda wowote unaweza kubebeshwa zigo la lawama endapo timu yako inaweza kukutana nayo.

Kipindi cha nyuma mchezaji anayecheza eneo hilo alikuwa akichukuliwa poa katika soko la usajili, lakini kwasasa hali ni tofauti, mambo yamebadilika thamani ya kipa mwenye kiwango cha juu lazima ivunje benki ili kumnasa.

Kama unakumbuka, iliwabidi Liverpool kuvunja benki kumsajili Alisson Becker kutoka AS Roma kwa kitita cha Euro73 milioni. Baadaye, Chelsea nayo ilikwenda hatua nyingine mbele kwa kutoa Euro80 milioni kupata huduma ya Mhispania, Kepa Arrizabalaga.Kuingia sokoni kwa Liverpool kulitokana na udhaifu wa aliyekuwa kipa wao namba moja kwa kipindi hicho, Loris Karius alioonyesha kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wafuatao ni makipa watano bora duniani kwasasa ambao kwa kuangalia viwango vyao ambavyo wamekuwa wakionyesha msimu huu 2018/2019 wanaendelea kutesa katika medani ya soka.

Jan Oblak na Ter Stegen-Euro80 milioni

Thamani ya Euro80 milioni iliwaweka sokoni makipa wawili Jan Oblak na Marc-Andre Ter Stegen ambazo zinawapa fursa ya kuwa bora zaidi duniani kwasasa.Oblak alionyesha kuwa mmoja wa makipa bora duniani baada ya kubeba mafanikio ya Atletico Madrid kwa miaka kadhaa mfululizo katika Ulaya.

Baada ya kujiunga na ‘Los Colchoneros’ mwaka 2014, Oblak ameshinda kombe moja la Europa, Supercopa de Espana na UEFA Super Cup, pia aliisaidia klabu yake kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu 2015-16. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26, ana tuzo mbili za kuwa kipa bora ambazo ametwaa kwenye Ligi Kuu Hispania, pia amewahi kujumuishwa kwenye kikosi bora cha Ligi ya Mabingwa Ulaya ndani ya misimu miwili tofauti.

Marc-Andre Ter Stegen alijiunga na Barcelona akitokea Borussia Monchengladbach mwaka 2014 amekuwa kipa namba moja wa timu hiyo tangu msimu 2016-17. Mjerumani huyo amechangia kwa kiasi kikubwa akiwa kwenye milingoti mitatu ya Blaugrana kushinda mataji kadhaa yakiwemo matatu ya La Liga, manne ya Copa Del Rey na moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Kipa huyo mwenye umri wa miaka 26, alikuwa sehemu ya kikosi bora cha UEFA kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu wa 2015-16 na pia alijumuishwa na UEFA kwenye kikosi bora cha mwaka 2018 kutokana na kiwango chake bora.

David de Gea- Euro70 milioni

Anaweza kuwa kipa bora wa muda wote wa Manchester United na hata kuingia kwenye vitabu vya kumbukumbu vya Ligi Kuu England kama akiendelea kuwa katika kiwango bora.

Kwa sasa thamani yake ni Euro70 milioni, ni kipa wa tatu kwa ubora duniani yupo nyuma ya Oblak na Ter Stegen.

Kipa huyo chaguo la kwanza kwenye Taifa Hispania alijiunga na Man United akitokea Atletico Madrid mwaka 2011 kwa ada ya uhamishio iliyoripotiwa kuwa Euro25 milioni. Kiwango chake kilikuwa kwa kasi ndani ya kipindi kifupi.

De Gea amecheza zaidi ya michezo 259 kwenye Ligi Kuu akiwa na mashetani hao wekundu na kutwaa tuzo ya Sir Matt Busby kwa miaka minne.

Mhispania huyo, 28, ameshinda ubingwa wa England , Kombe la Europa, Kombe la FA na Ngao ya Jamii akiwa na Manchester United. David de Gea alikuwa sehemu ya kikosi cha wachezaji 11 bora wa dunia mwaka 2018.

Courtois-Pauni65 milioni

Baada ya kucheza kwa mafanikio Chelsea kwenye Ligi Kuu England (EPL), Thibaut Courtois aliondoka England na kwenda Hispania kujiunga na Real Madrid kwa ada ya uhamisho wa Euro38.8 milioni mwaka jana.

Courtois alicheza mechi 154 ya mashindano yote akiwa na Chelsea ambapo alishinda mataji mawili ya EPL, Kombe la FA mara moja na Kombe la Ligi.

Hakuwa katika ubora wake uliozoeleka kama ilivyokuwa Chelsea, lakini anasimama miongoni mwa makipa bora duniani kutokana na kubebwa kwake na yale aliyofanya mwaka jana ambapo alikuwa kipa bora wa Kombe la Dunia Russia.

Pamoja na kuwa Liverpool ilitumia Euro73 milioni kupata huduma ya kipa wa Kibrazil aliyekuwa AS Roma thamani yake ni Euro65 milioni, kipa huyo bado ana safari ndefu licha ya kuwa kwenye kiwango kizuri ya kuhakikisha klabu yake inakuwa kwenye mikono salama.