UCHAMBUZI: Makosa ya viongozi wetu serikalini ni yenye heri?

Wednesday January 16 2019

 

By Padri Privatus Karugendo

Kwenye miaka ya themanini nchini Ujerumani, niliishi kwenye jumuiya ya watu waliokuwa na theolojia ya kushangilia makosa. Mwanzoni theolojia hii ilinichanganya na kunipunguzia kiwango fulani cha imani yangu.

Baada ya kuishi miaka mitatu ndani ya jumuiya hii na kuielewa theolojia yao, niliipenda na kuikumbatia na imenijenga kiimani hadi leo hii. Awali nilikuwa nimelelewa kwenye utamaduni na theolojia ya kulaumu makosa na kunyosheana vidole.

Mtu akikosea, analaumiwa, anazomewa ananyoshewa kidole, anaadhibiwa, anatumbuliwa na wakati mwingine anatengwa. Kwa hawa, mtu akikosea; anashangiliwa na kupongezwa kwa kuisaidia jumuiya kugundua kasoro zake.

Waliamini kwamba mtu mmoja hawezi kufanya makosa bila kusababishwa na mazingira yanayomzunguka. Kwamba kosa la mtu mmoja linaweza kuwa lina mnyororo wa matukio yanayowagusa wengi ndani ya Jumuiya.

Mtu akikosa uaminifu kwenye ndoa yake, badala ya kumhukumu na kumlaani, wanampongeza kwa kuwasaidia kuonyesha mapungu yaliyo kwenye Jumuiya yao. Hawakai wakatulia mpaka watafute chanzo cha mtu huyo kuisaliti ndoa yake.

Hatimaye, wanagundua kwamba wote wanashiriki kosa hilo; hivyo kwa pamoja wanatafuta njia za kuisaidia ndoa hiyo. Wakifanikiwa; wanasherehekea na kufanya ibada ya kumtukuza Muumba wao. Mfumo huu wa kuyashangilia makosa na kuyatumia kujisahihisha, kuchukuliana, kuvumiliana, kukamilishana na kupiga hatua kwa pamoja.

Si lengo langu kuelezea kwa kirefu juu ya theolojia hii, bali ni kutaka kuona kama sisi Watanzania tunaweza kujifunza kitu kutokana na ‘kosa lenye heri’.

Je, tunaweza kuyatumia makosa yanayojitokeza katika taifa letu, kugundua kasoro tulizonazo kama taifa?

Tumeshuhudia watu wakitumbuliwa, wakibadilishiwa vituo vya kazi na wengine wakitupwa mahabusu. Je, tunajifunza kutokana na makosa yao ili tuweze kusonga mbele kama taifa. Je, tunatafuta chanzo cha makosa na kushindwa kwao? Je, sisi hatuhusiki kwa njia moja ama nyingine katika kushindwa kwao?

Sote tuna vibanzi. Tusiwanyoshee kidole wala kuwalaumu wengine. Ni Watanzania wangapi wangefanya kinyume kama wangepata nafasi ya kufanya hizo kazi?

Ukweli ni kwamba, kosa linapotendeka kunakuwa na kasoro fulani katika jamii husika. Hivyo kosa hilo linasaidia kufichua mengi. Na kama hayo yaliyofichika ni mabaya, hekima inaongoza na njia mpya zinatafutwa, na jamii inasonga mbele. Ndio hapo, kosa linageuka kuwa lenye heri.

Makosa ya viongozi serikalini ni matatizo kama yalivyo mengine katika jamii yetu. Mfano wale wanaowapora maiti wakati wa ajali katika barabara zetu, wengine wanaiba nyaya za umeme na mafuta transfoma, wengine wanahujumu TTCL, wengine wanachimbua mabomba ya maji na kuharibu mtandao wa maji, wengine wanaiba alama za barabarani, wengine wanakata misitu hadi tabianchi inabadilika.

Ni matatizo mengi na yote yanaweza kutusadia kujifunza kutokana na nayo.

Advertisement