Malembo alivyoiona fursa ya ufugaji samaki kwenye vizimba

Muktasari:

  • Ni mradi anaosema utamgharimu kati ya Sh50 milioni hadi Sh100 milioni na kwamba aina hiyo ya ufugaji ni njia bora ya kupambana na uvuvi haramu

Tanzania ina ukubwa wa kilomita 942,600 za mraba na asilimia 6.55 ya eneo hilo imefunikwa na maji ambayo yanatoa mavuno ya samaki yanayofikia tani 350,000..

Kiasi hicho kwa kuwa nchi ina uwezo wa kuvua tani 750,000 iwapo uvuvi utafanyika kwa ufanisi. Lakini shughuli za uvuvi hufanywa na wavuvi wadogo kwenye maji baridi na katika ukanda wa bahari ya Hindi ambao huchangia takriban asilimia 95 ya samaki wote wanaozalishwa nchini.

Hata hivyo, sekta ya uvuvi inakabiliwa na changamoto kubwa ikiwa pamoja na uvuvi haramu, zana duni na uwekezaji mdogo katika sekta hiyo unaosababisha kuvuliwa kwa samaki wachache.

Lakini kuna njia bora za ufugaji zinazoweza kuzalisha samaki wengi bila ya kuwa na madhara kwa samaki walio katika maeneo ya asili kama bahari, ziwa na mito ambako wavuvi hurahisisha kazi yao kwa kuvua kwa kutumia baruti au nyavu ndogo ambazo haziruhusiwi.

Paul Malembo ni mmoja wa wajasiriamali hao ambaye anakusudia kuwekeza kati ya Sh50 milioni hadi Sh100 milioni ili kufuga samaki kwenye vizimba kando ya ziwa Victoria mkoani Mwanza.

Katika mazungumzo na Mwananchi jijini Dar es Salaam, Malembo anaeleza faida tano za kufuga samaki kwenye vizimba.

Swali: Nini hasa kimekuvutia kuwekeza kwenye uvuvi wa aina hii?

Jibu. Kwanza aina ya ufugaji wenyewe, teknolojia hii ya vizimba ilikuwapo kwa siku nyingi, lakini kwa sasa inachukua nafasi kubwa

kutokana na faida zake.

Kilichonivutia mimi ni mahitaji ya samaki nchini kuwa makubwa kuliko upatikanaji.

Tanzania tuna mahitaji makubwa ya samaki ukilinganisha na uvuvi uliopo. Tunahitaji ya zaidi ya tani 300,000 za samaki jambo ambalo kwangu ni fursa kubwa. Ndiyo maana nikaamua kuwekeza huko. Kwa hiyo, natumia mfumo huu kwa kuwa changamoto zake ni chache.

Swali: Umesema mfumo huu una faida, ni zipi hizo?

Jibu: Vizimba vina changamoto chache ukilinganisha na mabwawa kufugia samaki. Kwa mfano, eneo la mita sita kwa sita na kina cha mita nne linachukua samaki 9,000 hadi 12,000.

Changamoto nyingine iko kwenye upatikanaji wa hewa ya okisijeni. Ile kupwa na kujaa kwa maji kwenye ziwa na bahari kunatengeneza oksijeni moja kwa moja, lakini kwenye mabwawa lazima utafute njia nyingine ya kuongeza hewa hiyo. Watu wanatumia mafundi wa ujenzi kujenga mabwawa ya samaki, wakati kunahitajika utaalamu zaidi kwa sababu kuna wakati samaki wanataka kwenda chini zaidi.

Kwa hiyo kwenye mabwawa maji yanatakiwa yaingie na kutoka, lakini kwenye vizimba haina haja na vilevile samaki anaishi maisha ya asili kuliko kwenye bwawa. Hata uvunaji kwenye vizimba ni rahisi kuliko kwenye bwawa. Halafu chakula utakacholisha kinaliwa kwa zaidi ya asilimia 90 kwa kuwa ni mfano wa tembe (pellets). Kwa hiyo kilichonivutia ni faida kubwa itakayopatikana kwenye vizimba.

Swali: Unatarajia kufuga samaki wa aina gani?

Jibu: Nataka kufuga sato, lakini baadaye nitajikita zaidi kwenye sangara, japo kwa muda mrefu sangara hawajazoeleka kufugwa wala kupelekwa maabara ili kuzalisha mayai.

Mimi kwa utafiti mdogo nilioufanya, sangara anaweza kufugika kama atalishwa samaki wadogo, baada ya miezi miwili anakuwa amefikisha kilo nane hadi 10. Kwa hiyo ufugaji huo hautakuwa wa kuzalisha vifaranga, bali ni kumchukua na kumnenepesha. Sangara anapotaga mayai anakwenda kina kirefu cha maji. Kama Serikali na wadau na hasa taasisi za utafiti watamfanyia utafiti sangara na kufanikiwa kuzalisha mayai, faida yake ni kubwa kwa sababu wana soko kubwa nchi za Ulaya.

Swali: Ni utafiti gani ulioufanywa kwa sangara?

Jibu: Si utafiti wa kisayansi, bali ni mazoea tu na nimeleta wazo kwamba natamani kufanya huo mradi. Nawaalika watafiti ili wamfanyie utafiti sangara ili kupata manufaa makubwa.

Swali: Kuna changamoto zozote unakumbana nazo?

Jibu: Changamoto zipo, kwa sababu huu mradi unahitaji mtaji mkubwa. Kwanza kupata vibali tu vinaweza kutumia Sh10 milioni, ambavyo ni kibali cha kijiji, kibali cha mazingira, Mamlaka ya Bonde la ziwa na kibali kutoka Taasisi ya utafiti wa Uvuvi (Tafiri)

Swali: Umeshafanya tathimi ya uwekezaji na faida utakayopata?

Jibu: Ndiyo, katika kila kizimba natarajia kuweka sato 9,000 ambao nitawakuza kwa miezi sita hadi nane. Hivyo natarajia kufuga samaki 45,000 ambao kila mmoja akiwa na kilo moja nitamuuza kwa Sh8,000 hadi 10,000.

Swali: Je, mradi huu utawasaidiaje wavuvi wengine?

Jibu: Huu mradi nataka niutumie kama shamba darasa kwa wavuvi wengine. Serikali kwa sasa inapambana na uvuvi haramu. Ni kama vile wafugaji wanavyoshauriwa kupunguza mifugo ili wapate mazao mengine. Mimi nitawashauri wavuvi watumie njia hii kuzalisha samaki wengi kwa wakati mmoja kuliko kutumia njia haramu.