Malkia wa nguvu mrudisha tabasamu kwa waliopoteza

Muktasari:

  • Katika kurasa zake pia zimejaa picha za watu aliowarudishia tabasamu kwa kuwatafutia misaada mbalimbali.

Ukiwa katika Barabara ya Uhuru katika mwa Jiji la Mwanza au ukitokea jengo la CCM Mkoa ukielekea Mlango Mmoja au ukiwa unatoka Salma Cone ukiitafuta Barabara ya Sekou Toure, utakutana na jengo kubwa jeupe lenye maandishi, Flora Lauo.

Ndani ya jengo hilo kuna mavazi, viatu na bidhaa za urembo vinavyometameta kutokana na kuaksi miale ya jua wakati wa mchana. Hivi vitakushawishi zaidi ufike hadi ndani ushuhudie.

Mapokezi wapo ‘wadada’ wawili ambao hata bila ya kukufahamu, wanakukaribisha kwa tabasamu. Neno, karibu, karibu, karibu ni sawa na wimbo uliopangwa kwenye king’ora cha magari ya zimamoto.

Hapo utaulizwa swali la huduma unayoihitaji kwa sauti ya iliyojaa ushawishi.

Lakini hiki sicho kinachomtambulisha Flora Lauo ambaye ni mama wa watoto wawili kwa Watanzania. Ukitembelea ukurasa wake wa Instagram au kutazama kipindi cha Nitete ndipo ilipo taswira ya mwanamke huyu ilipo.

Picha za kutisha na kusikitisha za watu anaowasaidia zinatoa taswira ya kazi ngumu anayofanya.

Katika kurasa zake pia zimejaa picha za watu aliowarudishia tabasamu kwa kuwatafutia misaada mbalimbali.

Pamoja na kutambulika kama mdau wa urembo mkoani Mwanza, Flora amewekeza nguvu katika kusaidia jamii nchi nzima.

Mbali na kuwa alijiingiza katika kusaidia jamii muda mrefu, mwaka 2014 ndipo alipoweza kuirasimisha kuwa moja ya kazi zake kwa kufungua taasisi ya Nitetee Foundation.

“Kazi ya saluni nimeifanya kwa mikono yangu kwa zaidi ya miaka sita na baadaye Mungu akanijalia nikaweza kuanza shughuli za kijamii,” anasema Flora.

Anasema mazingira na maisha aliyoyaishi akiwa mdogo yalimpa moyo wa kuanzisha kitu ambacho alijua ipo siku kingekuwa msaada kwa jamii iliyomzunguka.

“Kwa ugumu ugumu tu nilifungua kituo cha kuwasaidia watoto wagonjwa walioishi kwenye mazingira magumu na mabinti wa kazi walionyanyaswa na waajiri wao.”

Tangu kipindi hicho Flora amekuwa mtumishi mkubwa wa kazi za jamii. Anawasaidia watoto wanaoishi mazingira magumu hususan wagonjwa na mabinti wanaofanya kazi za ndani.

Mafanikio yake

Anasema amefanikiwa kuiendeleza saluni yake na hivyo kutoa ajira na kutoa mafunzo kwa zaidi ya vijana 1,000 kuhusu masuala ya urembo.

Aidha kutokana na bidii ya kukidhi mahitaji anayoyaona kwenye jamii, Flora alidhamiria kufungua kituo cha kulea watoto mwaka 2015. Kituo hiki kimesheheni watoto ambao hawana wazazi na wanaoishi katika mazingira magumu.

Aidha mama huyo wa watoto wawili, anasema kuitwa Muscat nchini Oman kutoa hamasa kwa wanawake, mwanzoni mwa mwaka huu, anahesabu kuwa ni sehemu ya mafanikio yake.

Anaeleza ya kuwa kwa sasa shirika lake ambalo lina vituo vingi limebadilika kuwa taasisi kutokana na mambo ambayo wanayafanya.

Wapi ana pata fedha?

“Hatujawahi kupata ruzuku wala msaada wowote kutoka popote, isipokuwa kuna wale wasamaria ambao pia ni mmoja mmoja. Hao kuna wale wanaoahidi kitu fulani kwa mfano mtu anaweza akaamua kutununulia mashuka na wa kutuletea mipira ya kuchezea,” anasema.

Mara nyingi taasisi ya Nitetee Foundation imekuwa ikishirikiana na The Desk and Chair Foundation iliopo jijini Mwanza katika kuwasaidia wagonjwa kupata tiba.

Safari ya maisha binafsi….

Mwanzoni mwa miaka ya 2000, Flora alibahatika kusoma katika chuo cha urembo kutoka kwa msaada wa kaka yake ambaye wakati huo alikuwa jijini Nairobi, Kenya. Hili lilimsaidia katika kuanzisha maisha yake binafsi.

“Baada ya kuhitimu masomo yangu ya urembo nilijua sasa maisha yatakuwa angalau kidogo maana nilielewa kusuka na mambo mengine kama vile upambaji,” anasimulia

Mwaka huo huo alimaliza kozi ya urembo na kutunukiwa cheti chake, kaka yake aliyekuwa Nairobi aliahidi kumnunulia vyombo kadhaa kwa ajili ya kuazisha ofisi yake, saluni jijini Mwanza.

Anasema jioni ile walizungumza na kaka yake huyo, ilikuwa ya mwisho maana siku iliyofuata, alipokea simu kutoka nyumbani kwao kwamba kaka yao amefariki kutokana na maradhi ya muda mfupi.

“Nilichanganyikiwa, kaka alikuwa msaada na alitambua maisha tuliyoyapitia yeye akiwa mtoto wa kwanza,” anasema Flora.

Shughuli za msiba zilimalizika na ikabidi arudi Mwanza. Alibahatika kuajiriwa kwenye saluni moja na kufanya kazi ya kulipwa kwa siku.

Kufanya kazi ya ususi haikumpa shida wala mawazo maana alifahamu kwamba ipo siku Mungu angemfungulia milango naye akapata ofisi yake mwenyewe.

Kumiliki saluni

Mwaka 2008, mdogo mdogo, Flora alifanikiwa kufungua Salon yake mwenyewe licha ya kwamba ilikuwa haipendezi kama ya muajiri wake.

Alijua mwanzo ni mgumu na hivyo alipambana kadri ya uwezo kuhakikisha kwamba kidogo alichokipata kinaenda kwenye uboreshaji wa ofisi yake mpya.

Changamoto

Changamoto anasema ni nyingi kiasi kwamba hawezi kuzimaliza japo anatumbua namna ya kukabiliana nazo.Kuna wakati anatamani kupumzika lakini inakuwa ni vigumu kutokana na majukumu yaliyo mbele yake.